Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa nchi za Afrika na zile za Ghuba (GCC+) kuimarisha ushirikiano katika uhamaji wa wafanyakazi ili kuhakikisha unakuwa salama, wenye haki, unaozingatia taratibu na wenye manufaa kwa pande zote.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 06 Oktoba 2026, katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Doha kuhusu Uhamaji salama wa Wafanyakazi
Amesema ahadi za kisiasa zinapaswa kugeuzwa kuwa sera, makubaliano na programu zinazotekelezeka zitakazoboresha maisha ya wafanyakazi wahamiaji, familia zao, waajiri na uchumi wa nchi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kulinda haki za wafanyakazi, kuboresha mifumo ya uajiri, kuimarisha mikataba ya pande mbili kuhusu ajira na kutumia takwimu sahihi katika kupanga sera za uhamaji wa wafanyakazi.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na nchi za Ghuba( GCC+) kwa kuzingatia misingi ya manufaa ya pamoja na uwajibikaji wa pamoja.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Kazi wa Qatar, Mhe. Dkt. Ali bin Samikh Almarri; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu; Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana na Uwezeshaji Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir Mrembo; Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Awesi Mohamed, pamoja na Taasisi mbalimbali za kimataifa, wajumbe kutoka nchi zaidi ya 33, zikiwemo nchi za Afrika, Nchi Wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC+), Jordan na Lebanon.
















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...