Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Halmashauri ya Mji wa Kondoa, akikagua miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, huku akitoa wito wa kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa.

Akiwa Kata ya Itaswi, Mhe. Senyamule alikagua ujenzi wa Bwawa la Itaswi lenye thamani ya shilingi bilioni 5.7, huku akisisitiza kukamilishwa kwa mradi huo ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo. Meneja wa TARURA Wilaya ya Kondoa, Ndugu Majid Mtili, alisema utekelezaji wa mradi umekuwa wa kasi ndogo kutokana na mkandarasi kupokea fedha kwa awamu.

Katika Kijiji cha Potea, Kata ya Pahi, Mkuu huyo wa Mkoa alikagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Potea inayotarajiwa kukamilika Novemba 2026 kwa gharama ya shilingi milioni 540 na kuanza kupokea wanafunzi Januari 2027. Aidha, katika Kata ya Serya, Halmashauri ya Mji wa Kondoa, aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Serya itakayogharimu shilingi milioni 302 na kuanza kutumika Januari 2027.

Akizungumza na wananchi wa Itaswi, Mhe. Senyamule alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za kijamii, akitaja ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Haire wenye thamani ya shilingi milioni 98, Shule ya Msingi Chubi yenye thamani ya shilingi milioni 100 pamoja na mikopo ya asilimia 10 yenye jumla ya shilingi milioni 24.5 kwa vikundi vitatu.

Kuhusu mvua kubwa zinazotarajiwa, Mhe. Senyamule amewataka wananchi kuzingatia taarifa na ushauri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), hususan wanaoishi mabondeni na maeneo hatarishi, huku akisisitiza kuwa tahadhari hizo zisitumike kama sababu ya kuacha shughuli za kilimo. “Ni afadhali kuhama mapema kabla mvua hazijaanza kama unakaa bondeni kwani ni njia ya maji. Natoa wito kwa wananchi wote kuanza kuchukua tahadhari".

Mhe. Senyamule pia amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wakati wa mvua, akisisitiza kuwa wananchi wasijaribu kuvuka maeneo yenye maji yanayotiririka.

Amesema Serikali imeendelea na maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua, ikiwemo kuweka utaratibu wa kutumia majengo ya shule kama maeneo ya hifadhi inapobidi, huku wananchi wakitakiwa kuhamia maeneo salama pindi hali inapohitaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Fatma Almas Nyangasa, amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maandalizi dhidi ya mvua zinazotarajiwa kwa kutembelea kata, vijiji na mitaa mbalimbali.

Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Ndugu Shabani Milao, amesema Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya minada, ikiwemo vyoo na huduma za maji.









Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...