Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameitaka Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, fursa za biashara na uwekezaji, pamoja na umuhimu wa ushiriki wao katika uchaguzi na uongozi wa Chemba.
Mhe. Senyamule ametoa wito huo wakati wa mazungumzo na ugeni kutoka TNCC, ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bw. Oscar Kissanga, yaliofanyika ofisini kwake , jengo la Mkapa, Jijini Dodoma.
Amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuwawezesha wafanyabiashara kutambua na kutumia fursa zilizopo, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kupata uwakilishi madhubuti wa maslahi yao, sambamba na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Ni muhimu TNCC kuendelea kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali, kuwajengea uelewa kuhusu fursa za biashara na uwekezaji na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uongozi na uwakilishi wa maslahi yao,” amesema Mhe. Senyamule.
Mkuu huyo wa Mkoa amepongeza juhudi zinazofanywa na TNCC katika kuwafikia wafanyabiashara na kuwataka kuendelea kuimarisha huduma hizo, hususan kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma, ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika fursa za kiuchumi na uwekezaji.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TNCC, Bw. Oscar Kissanga, amesema Chemba inaendelea kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali nchini, kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu fursa za biashara na uwekezaji, huduma zinazotolewa na Chemba, uchaguzi na umuhimu wa wafanyabiashara kushiriki katika uongozi na uwakilishi wa maslahi yao.
Amesema wafanyabiashara wanahimizwa kujiunga na TNCC na kutumia Mfumo wa Kidijitali wa Tanzania Chamber Portal (TCP) ili kupata huduma mbalimbali za Chemba kwa njia ya kidijitali.
Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma, kurahisisha mawasiliano na kuwawezesha wafanyabiashara kutumia fursa zinazotolewa na Chemba kwa ufanisi zaidi.




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...