Tamthilia mpya ya Rehani, inayowakutanisha wasanii Aunt Ezekiel na Kobisi, inatarajiwa kuanza kurushwa Oktoba 19, 2026, kupitia St Swahili, huku ikiahidi kuleta uhalisia wa maisha ya Kitanzania.

Mtayarishaji wa tamthilia zilizopata umaarufu nchini za Komborela, Saluni ya Mama Kimbo na Zahanati ya Kijiji, Abdul Juma, amesema tamthilia mpya ya Rehani ni mwanzo wa safari mpya katika tasnia ya filamu na tamthilia nchini, akiahidi kuwasilisha kazi yenye ubora, uhalisia na maudhui yanayogusa maisha ya Watanzania.

Tamthilia hiyo inayozalishwa kwa ushirikiano na Kampuni ya StarTimes Limited kupitia chapa yake ya St Swahili, itaanza kurushwa Oktoba 19, 2026, kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, ikiwa na maudhui mbalimbali yanayolenga kuburudisha, kuelimisha na kufundisha jamii.

Juma amesema Rehani imewashirikisha wasanii mbalimbali wenye uwezo mkubwa wa kuigiza, wakiwemo Aunt Ezekiel, anayeigiza mhusika wa Mwajabu, pamoja na Kobisi, ambao kwa pamoja wanatarajiwa kuipa tamthilia hiyo mvuto wa kipekee.

Amesema mafanikio ya utayarishaji wa tamthilia hiyo yametokana kwa kiasi kikubwa na ushirikiano alioupata kutoka kwa Aunt Ezekiel, ambaye amekuwa mstari wa mbele kumtia moyo na kumsaidia kuhakikisha mradi huo unakamilika.

"Kipekee nitoe pongezi kwa dada yangu Aunt Ezekiel. Amekuwa mtu wa kwanza kunishika mkono na kunipa moyo kuhakikisha Rehani inafanyika, hadi kufikia hatua ya kutoa fedha zake mwenyewe kwa ajili ya kutengeneza kipande kifupi cha video (Demo)," amesema Juma.

Ameongeza kuwa kazi zake za awali zimekuwa na mafanikio makubwa, ikiwemo kutwaa tuzo mbalimbali, hivyo ana matumaini kuwa Rehani itaendeleza mafanikio hayo kutokana na ubora wa utayarishaji wake, maudhui ya Kitanzania na kuzingatia uhalisia wa maisha ya kila siku.

Kwa upande wake, Meneja Masoko wa StarTimes, David Malisa, amewahakikishia watazamaji wa St Swahili kuwa tamthilia hiyo itapatikana kupitia vifurushi vyote, kuanzia kifurushi cha chini kabisa, ili kuwapa nafasi watazamaji wengi zaidi kufurahia burudani hiyo.

Malisa amewataka wateja wa StarTimes kulipia vifurushi vyao mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza katika huduma za malipo na mitandao, na hivyo kuhakikisha hawakosi vipindi vya tamthilia hiyo mpya.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...