Na Mashaka Mhando, Tanga

SERIKALI kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeanza maandalizi ya kufanya sensa maalumu ya vyombo vyote vya majini Tanzania Bara ili kuwezesha mipango sahihi ya maendeleo, usalama, na huduma za uokozi.

Sensa hiyo ya kimkakati itahusisha vyombo vyote vya majini bila kujali ukubwa au eneo vinapofanyia shughuli; ikiwemo meli, boti, mashua, mitumbwi, pamoja na karakana zinazojihusisha na ujenzi wa vyombo hivyo.

Akizungumza na kituo hiki, Ofisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Tanga, David Chilagi, amesema zoezi hilo linalenga kuibua idadi halisi, maeneo vilipo, pamoja na aina ya vyombo vinavyotumika katika shughuli za usafirishaji na uvuvi.

"Tunapotambua idadi halisi ya vyombo na maeneo vilipo, tunakuwa na uwezo wa kujua wapi tunapaswa kuongeza elimu ya usalama, wapi tunahitaji kuimarisha huduma za utafutaji na uokozi, na wapi wananchi wanahitaji kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo," amesema Chilagi.

Kwa Mkoa wa Tanga, zoezi hilo litafanyika katika maeneo mbalimbali yenye vyombo vya majini, huku likipanuliwa pia kwenye mikoa jirani ikiwemo Kilimanjaro (Bwawa la Nyumba ya Mungu) na Manyara (Mto wa Mbu), ili kuhakikisha hakuna chombo kinachorukwa iwe kipo baharini, mtoni, ziwani au kwenye mabwawa.

Kwa upande wake, Mtakwimu kutoka NBS, Meshack Alfred, amesema ushiriki wao utasaidia kupatikana kwa takwimu rasmi na sahihi za kisekta kuhusu usafirishaji majini, ambazo zitatumika moja kwa moja katika kufanya maamuzi na mipango ya maendeleo ya Serikali.

Ameongeza kuwa takwimu hizo zitasaidia pia kubaini mahitaji halisi ya wavuvi na wadau wengine, huku akisisitiza kuwa NBS itahakikisha ubora na usahihi wa taarifa zitakazokusanywa.

Kufuatia hatua hiyo, TASAC na NBS zimetoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya majini, wavuvi, na wadau wote wa sekta hiyo kutoa ushirikiano kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi wakati wa zoezi hilo, ili kuiwezesha nchi kuwa na kanzidata (database) inayoonyesha uhalisia wa sekta ya usafiri majini.








Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...