Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Harriet Rushekya, amewataka wadau wa sekta ya utalii na usafiri kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kutumia fursa za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kuitangaza Tanzania na kuongeza idadi ya watalii nchini.

Rushekya amesema mashindano makubwa ya kimataifa ya michezo yanaweza kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania, kuvutia wageni na kuwahamasisha kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka na Maonesho ya TASOTA Server Connect 2026, ameupongeza Umoja wa Mawakala wa Usafiri Tanzania (TASOTA) kwa kuandaa jukwaa hilo linalowaunganisha wadau kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kukuza biashara katika sekta ya usafiri na utalii.

Amesema mabadiliko ya teknolojia, yakiwemo matumizi ya akili unde (AI) na mifumo ya kidijitali ya kuhifadhi huduma za utalii, yanafungua fursa mpya za biashara, huku yakihitaji wadau kuimarisha uwezo wao ili kukabiliana na ushindani wa soko la kisasa.

Rushekya ameitaja Tanzania Destination Booking Platform, inayojulikana kama Travel Companion, kuwa miongoni mwa jitihada zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za utalii, kuboresha uzoefu wa wageni na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.

Amesisitiza kuwa pamoja na kutumia teknolojia kutangaza utalii, ni muhimu kulinda mazingira, kuhifadhi urithi wa utamaduni na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha utalii unakuwa endelevu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TASOTA, Talib Talib, amesema jumuiya hiyo inaendelea kuandaa mikutano na maonesho kwa lengo la kuwaunganisha mawakala wa usafiri na wadau wengine, kuwawezesha kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano yatakayosaidia kukuza biashara zao.

Talib amesema maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo HM, Galadina, Selcom na Shirika la Ndege la Air Tanzania, na kutoa fursa kwa mawakala wa usafiri kukutana na watoa huduma, kujenga ushirikiano wa kibiashara na kupanua wigo wa huduma kwa wateja.

Kuhusu AFCON, amesema TASOTA inaendelea kutathmini fursa zinazoweza kujitokeza kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafiri na utalii wakati wa mashindano hayo.

Amesema jumuiya hiyo inalenga kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuweka mikakati itakayowawezesha mawakala wa usafiri kunufaika na fursa hizo, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata nafasi za kushiriki na kunufaika.

Talib ameongeza kuwa TASOTA ina nafasi ya kuwasaidia wanachama wake kupata taarifa muhimu za kibiashara kupitia mahusiano yake na wizara na taasisi mbalimbali, ikiwemo TTB, ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi na kutambua fursa mpya sokoni.

Naye Meneja na mchambuzi wa mifumo ya tiketi za ndege nchini Tanzania, Omari Hamisi Kazimoto, amesema wadau wa sekta ya usafiri wa anga na utalii wameanza kujiandaa kupokea wageni wanaotarajiwa kuhudhuria AFCON.

Amesema mashindano hayo yanaweza kuongeza mahitaji ya tiketi za ndege, malazi, usafirishaji na huduma nyingine, hivyo kutoa fursa kwa mawakala wa usafiri, kampuni za ndege, hoteli na wafanyabiashara wengine kupanua shughuli zao.

Kazimoto ameeleza kuwa ongezeko la wageni linaweza kuchochea safari za ndege kati ya miji mbalimbali itakayohusishwa na shughuli za mashindano hayo na kuongeza mzunguko wa biashara katika sekta ya usafiri na utalii.

Amesisitiza kuwa maandalizi ya mapema na uboreshaji wa huduma ni muhimu ili kukidhi mahitaji ya wageni na kuhakikisha fursa zitakazotokana na mashindano hayo zinawanufaisha wadau wengi zaidi.

Kwa pamoja, wadau hao wameeleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano, matumizi ya teknolojia na maandalizi ya huduma bora ili kutumia AFCON kama fursa ya kuitangaza Tanzania, kukuza utalii na kuchochea maendeleo ya uchumi.

TASOTA imesema itaendelea kuandaa mikutano na maonesho ya kila mwezi kwa lengo la kuimarisha mtandao wa wadau, kuongeza upatikanaji wa taarifa za kibiashara na kuwawezesha mawakala wa usafiri kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo.












Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...