NA DENIS MLOWE, ARUSHA
WABUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika ujenzi wa uwanja wa kisasa mkoani Arusha, unaotarajiwa kutumika katika maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Wabunge hao walitoa pongezi hizo wakati walipotembelea eneo la ujenzi wa uwanja huo jijini Arusha, ambapo walipata fursa ya kujionea mradi huo na kujadili umuhimu wake katika kukuza michezo, utalii na uchumi wa Tanzania pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wenzake, Mbunge wa EALA, Cosato Chumi, alisema ujenzi wa uwanja huo ni hatua kubwa inayodhihirisha uwezo wa Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati pale dhamira na rasilimali zinapowekwa katika kufikia malengo ya taifa.
“Kwa kweli ni jambo kubwa, si jambo dogo. Huu ni uthibitisho kwamba Watanzania tukiamua tunaweza,” alisema Chumi.
Alisema maandalizi ya AFCON yanatoa fursa muhimu kwa Tanzania kuimarisha miundombinu ya michezo na kuweka mazingira yatakayoiwezesha nchi kuendelea kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa hata baada ya michuano hiyo kumalizika.
Chumi alisisitiza kuwa uwanja huo haupaswi kutumika kwa kipindi cha AFCON pekee, bali unapaswa kuwa kituo cha kudumu cha kuandaa mechi za kimataifa, mashindano ya klabu na matukio mengine makubwa ya michezo yatakayovutia timu na mashabiki kutoka mataifa mbalimbali.
Alisema ni muhimu kwa wadau wa michezo kuanza kupanga mapema namna ya kutumia miundombinu hiyo, ikiwemo kuandaa mashindano ya klabu kutoka Afrika Mashariki na Kati na kualika timu kubwa za bara la Afrika.
Alitaja uwezekano wa kuzialika klabu zenye majina makubwa kama Gor Mahia na AFC Leopards za Kenya, Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini, pamoja na Vipers na URA za Uganda, ili kushiriki mechi za kirafiki na mashindano yatakayoongeza ushindani wa soka katika ukanda huo.
Alisema hatua hiyo itazipa klabu za Tanzania fursa ya kupima uwezo wao dhidi ya timu zenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa, huku ikisaidia kuboresha viwango vya wachezaji na kuinua ubora wa soka la ndani.
Aidha, alieleza kuwa uwanja huo unaweza kuwa chachu ya kukuza utalii wa michezo mkoani Arusha, kutokana na uwezo wa kuvutia wageni, mashabiki na wadau wa soka ambao watatumia huduma mbalimbali za kitalii na kibiashara wakati wa mashindano.
Alisema kuongezeka kwa wageni kutafungua fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara, watoa huduma za malazi, usafiri, migahawa na biashara ndogondogo, huku vijana wakipata nafasi za ajira katika sekta zinazohusiana na michezo.
Chumi alitoa wito kwa Serikali, wabunge, vyama vya michezo na sekta binafsi kushirikiana kuandaa mikakati ya kuhakikisha uwanja huo unatumika kwa tija na kuendelea kuingiza manufaa kwa taifa kwa miaka mingi.
Alisema ni wajibu wa wadau kuanza kufikiria namna ya kuandaa mashindano ya kimataifa mara baada ya AFCON, badala ya kusubiri hadi michuano hiyo imalizike ndipo waanze kutafuta matumizi mengine ya uwanja huo.
Chumi alisema uwekezaji unaofanyika katika miundombinu ya michezo ni fursa ya kuendeleza vipaji vya vijana na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kushiriki na kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa.
Ujenzi wa uwanja huo ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda. Mashindano hayo yanatarajiwa kutoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza mwonekano wa Afrika Mashariki katika ramani ya soka la Afrika.
Wadau wa michezo wanatarajiwa kunufaika na miundombinu hiyo kupitia maandalizi ya mashindano, mafunzo na shughuli nyingine zinazohusiana na michezo, huku matumizi endelevu ya uwanja yakitarajiwa kuwa muhimu katika kuhakikisha uwekezaji huo unaendelea kuleta matokeo chanya hata baada ya AFCON.
Ziara ya wabunge wa EALA inaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukuza michezo na kutambua fursa zinazoweza kupatikana kupitia uwekezaji wa miundombinu, hususan katika kuimarisha soka, utalii na shughuli za kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...