Na Said Mwishehe,Michuzi TV.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt.Ashanti Kijaji, ametoa rai kwa Watanzania kushirikiana na askari wa uhifadhi kulinda misitu na rasilimali za taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Dkt.Kijaji alisema alisema hayo Oktoba 20,2026 alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maandalizi ya AFCON inayowezeshwa na Tourism Development Levy (TDL), ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza namna askari wa hifadhi wanavyolinda mazingira na uhifadhi.

“Ushirikiano kati ya wananchi na askari wa uhifadhi ni muhimu katika kulinda misitu, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhakikisha rasilimali za asili zinaendelea kunufaisha taifa na vizazi vijavyo.”

Waziri Kijaji amesema askari wa uhifadhi wanapaswa kuungwa mkono katika kutekeleza majukumu yao badala ya kuzuiwa au kufanyiwa vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao.

“Askari wanaolinda hifadhi zetu hawa ni watoto wetu Watanzania. Tuwalinde, tuwape ushirikiano na kuwawezesha kufanya kazi yao ipasavyo. Tusikwamishe juhudi zao za kulinda rasilimali za taifa,” alisema.

Pia amewataka wakulima na wafugaji kuheshimu sheria na taratibu za matumizi ya ardhi, akisisitiza umuhimu wa kuepuka kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa kinyume cha utaratibu.

Ameonya kuwa uharibifu wa misitu unaweza kusababisha madhara makubwa ya kimazingira, yakiwamo kuharibika kwa ardhi, kupungua kwa upatikanaji wa maji na kuenea kwa jangwa.

“Unaweza kulima mwaka mmoja au miwili, lakini jangwa likienea, madhara yake yanaweza kulikumba taifa zima,” amesema Waziri Kijaji.

Amefafanua misitu ina mchango mkubwa katika kuhifadhi vyanzo vya maji, kulinda udongo na kudumisha mazingira yanayowezesha shughuli za kilimo na uzalishaji mwingine.

“Uhifadhi wa misitu ni muhimu katika kulinda maisha ya wananchi na kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazotegemea rasilimali za asili.Mapato yanayotokana na rasilimali za taifa yanaweza kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa barabara na miundombinu ya maji.

Amesisitiza kulinda misitu si jukumu la askari wa uhifadhi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania, akiwataka wananchi kushiriki katika juhudi za kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya taifa.

Amewataka Watanzania kutambua kuwa misitu ni urithi unaopaswa kutunzwa ili vizazi vijavyo viendelee kunufaika na rasilimali hizo.

Pia amewapongeza askari wa uhifadhi kwa juhudi zao za kulinda rasilimali za taifa na kuwataka waendelee kutekeleza majukumu yao kwa weledi, huku wakishirikiana na wananchi kuimarisha uhifadhi wa misitu nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Petro Magoti amewapongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) katika Wilaya hiyo kutokana na kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda hifadhi ya Pugu Kazimzimbwi na maeneo mengine ya uhifadhi huku akisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana kulinda hifdhi na mazingira.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...