Na Jane Mwakyoma, Rukwa
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka familia nchini kujiwekea mipango ya kukabiliana na maafa kabla hayajatokea ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari zake yanapotokea.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo, Oktoba 13, 2026, katika Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Athari za Maafa.
Amesema mipango ya kukabiliana na maafa inapaswa kuanzia ngazi ya familia, huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kudhibiti vihatarishi na kuimarisha mifumo ya kukabiliana na majanga.
Alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, “Ustahimilivu Unaanzia Nyumbani,” inasisitiza umuhimu wa familia na jamii kujiandaa mapema ili kupunguza athari za maafa ambayo yamekuwa yakisababisha vifo, uharibifu wa mali na kuacha majonzi kwa waathirika.
Dkt. Nchemba alieleza kuwa ni muhimu jamii kupewa elimu na mbinu za kisasa pamoja na kutumia maarifa ya jadi yanayofaa kulingana na mazingira husika ili kuongeza uwezo wa kuzuia na kukabiliana na maafa.
Alisisitiza pia umuhimu wa Serikali na wananchi kushirikiana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, akieleza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa.
Akizungumzia mifano ya maafa yaliyowahi kuikumba Tanzania, alitaja maporomoko ya ardhi yaliyotokea Hanang na Mbeya, mafuriko pamoja na ajali mbalimbali ambazo zimeathiri maisha ya wananchi na kusababisha hasara kubwa.
Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Athari za Maafa huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha juhudi za kupunguza vihatarishi vya maafa na kujenga jamii zenye uwezo wa kukabiliana na athari zake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya maandalizi ya shughuli za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Wiki ya Vijana.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alisema maandalizi ya shughuli hizo yamefikia asilimia 100.
Aliongeza kuwa Wiki ya Vijana imetumika kuwajengea vijana uwezo wa kujiamini, kuwa wabunifu na kutambua fursa za maendeleo zilizopo katika maeneo yao.
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...