NA MWANDISHI WETU

CHINA imesema mradi wa ufufuaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) unatarajiwa kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo kutoka tani 200,000 za sasa hadi tani milioni 2.4.

Imeelezwa mradi huo unatarajiwa kupunguza muda wa usafirishaji kwa karibu theluthi mbili, hatua inayolenga kuimarisha usafirishaji na kukuza shughuli za kiuchumi katika ukanda huo.

Akizungumza katika uzinduzi wa ziara ya waandishi wa habari wa China na Tanzania ya kutembelea reli ya TAZARA, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa Tanzania, Zambia na China.

Alisema ziara hiyo yenye kaulimbiu “Kuhuisha Mustakabali, Kushirikiana Katika Ustawi” imeandaliwa katika kuadhimisha miaka 50 tangu reli hiyo ianze rasmi kutoa huduma, imekuwa alama ya urafiki na mshikamano kati ya nchi hizo China, huku ikichangia ukombozi, uhuru na maendeleo ya nchi za Afrika.

Chen alisema mradi huo hautaishia katika kuboresha usafiri pekee, bali pia utaimarisha mawasiliano ya kikanda, kupunguza gharama za usafirishaji kwa nchi zisizo na bandari na kukuza maendeleo ya kilimo cha kisasa, miundombinu pamoja na maeneo ya viwanda.

Aidha alisema hatua hiyo inalenga kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na reli hiyo na kuifanya TAZARA kuwa kitovu kipya cha ukuaji wa uchumi.

Pia Chen alizitaka taasisi za habari za China na Tanzania kutumia ziara hiyo kuandika na kuonesha maendeleo ya mradi, historia ya reli hiyo na mabadiliko ya maisha ya wananchi wanaoishi kandokando ya reli.

Alisema vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kujenga uelewa na kuimarisha urafiki kati ya wananchi wa nchi hizo kupitia taarifa zinazotokana na ushuhuda na uchunguzi wa moja kwa moja.

"China itaendelea kushirikiana na Tanzania na Zambia kuendeleza roho ya TAZARA, kutekeleza mradi wa ufufuaji wa reli hiyo na kujenga Ukanda wa Ustawi kwa lengo la kukuza mshikamano, ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika", alisema.

Naye, Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Uchukuzi Benjamin Adam Mbimbi alisema hiyo ufufuaji wa reli hiyo unalenga kuongeza uwezo wake wa kusafirisha mizigo ili kuimarisha biashara ya kikanda na kukuza maendeleo ya kiuchumi.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Zambia na Kampuni ya Uhandisi na Ujenzi wa China (CCECC).

Mbimbi alisema mradi huo utahusisha ukarabati wa miundombinu ya reli, mifumo ya mawasiliano na uashiriaji na upatikanaji wa vichwa vya treni na mabehewa, kwa lengo la kuifanya TAZARA kuwa reli ya kisasa, yenye ufanisi, uhakika na uwezo wa kujiendesha kibiashara.

Alisema ufufuaji huo utaimarisha ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza gharama za usafirishaji na kuunganisha masoko ya Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nchi nyingine za Kusini na Kati mwa Afrika.

"Serikali itaimarisha pia miundombinu ya bandari, vituo vya makasha na uratibu kati ya TAZARA, Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na wadau wengine wa usafirishaji.

Aidha, Mbimbi aliitaka sekta ya habari Tanzania na China kutumia ziara hiyo kuelimisha umma kwa kutoa taarifa sahihi na zenye uwiano kuhusu maendeleo ya mradi huo, akisisitiza kuwa ufufuaji wa TAZARA ni uwekezaji wa kimkakati utakaosaidia biashara, ajira, ushirikiano wa kikanda na ustawi wa wananchi.

Naye, Hamisi Shimye ambaye ni Mratibu wa Taasisi ya Habari Development, alisema ufufuaji na uboreshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) unatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha mageuzi ya kiuchumi barani Afrika kwa kuongeza ufanisi wa usafirishaji, kukuza biashara ya kikanda na kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.

Alisema mradi huo una fursa kubwa ya kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema TAZARA haipaswi kuangaliwa kama miundombinu ya kusafirisha mizigo pekee, bali kama nyenzo ya kimkakati ya kuunganisha uchumi wa nchi mbalimbali na kufungua fursa mpya za maendeleo.

Alisema makubaliano ya ufufuaji wa reli hiyo yaliyohitimishwa Septemba 29, 2025, kati ya Tanzania, Zambia na China, yanahusisha uwekezaji unaokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 1.4 chini ya mkataba wa uendeshaji wa miaka 31.

Kwa mujibu wa Hamis, mradi huo unahusisha ukarabati wa takribani kilomita 1,860 za reli, ununuzi wa vichwa vipya 34 vya treni, mabehewa 760 ya mizigo na mabehewa 16 ya abiria, pamoja na kuboresha mifumo ya mawasiliano na uendeshaji.

Alisema kukamilika kwa mpango huo kutakuwa na umuhimu mkubwa katika kupunguza gharama za usafirishaji, kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo ya nchi jirani na kuimarisha biashara baina ya nchi za Afrika.

Alisisitiza kuwa fursa zinazotokana na TAZARA zinapaswa kutumika kukuza viwanda vya ndani, hususan vya kuchakata madini na mazao ya kilimo, badala ya kuendelea kusafirisha malighafi kwenda nje bila kuongeza thamani yake.

"Maendeleo ya reli hiyo yanapaswa kuambatana na uwekezaji katika maeneo ya viwanda, maghala, vituo vya biashara na huduma nyingine za kiuchumi zitakazozalisha ajira kwa vijana." Alisema

Aidha, alieleza kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika unapaswa kwenda zaidi ya ujenzi wa miundombinu na kujikita katika uhamishaji wa teknolojia, mafunzo ya kitaalamu, ubunifu na kujenga uwezo wa Waafrika kusimamia na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Alisema mafanikio ya TAZARA hayapaswi kupimwa kwa idadi ya treni zitakazonunuliwa au kilomita za reli zitakazokarabatiwa pekee, bali pia kwa ajira zitakazozalishwa, viwanda vitakavyoanzishwa, gharama za usafirishaji zitakazopungua na mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi.

Hivyo, alisema Tanzania na Zambia zinapaswa kuitumia reli hiyo kama daraja la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kukuza ustawi wa wananchi wa nchi hizo na Afrika kwa ujumla.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...