Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Atupele F. Mwakibete, ameahidi kushirikiana na mamlaka za barabara kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya miundombinu ya barabara isiyopitika, huku akichangia Sh milioni moja kuunga mkono ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Mhanga, Kata ya Kimara.
Mwakibete ametoa ahadi hiyo Novemba 11, 2026, wakati akiendelea na ziara ya kutembelea Kata za Kimara na Dabaga, ambapo pia amefanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokwamisha maendeleo yao.
Katika ziara hiyo, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Itonya, ambao unaendelea vizuri, huku shule hiyo ikitarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza Januari 2027.
Akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Kidabaga na Mhanga, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza shughuli za maendeleo, sambamba na kuwataka kuacha vitendo vya uchomaji moto misitu na badala yake kulinda mazingira.
Kuhusu changamoto ya barabara, Mwakibete amesema atawasiliana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ili kujadili na kutafuta suluhisho la barabara zinazokuwa hazipitiki, hasa wakati wa mvua, hali inayosababisha usumbufu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Katika hatua nyingine, akijibu kilio cha wananchi wa Kijiji cha Mhanga kuhusu ukosefu wa zahanati, Mwakibete ametoa Sh milioni moja kusaidia ujenzi wa zahanati inayotekelezwa na Kanisa, hatua inayolenga kuongeza kasi ya mradi huo na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Aidha, amewahimiza wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaogharimu Sh 150,000, akieleza kuwa usajili huo ni muhimu katika kuwawezesha kupata huduma za afya kwa uhakika na kupunguza changamoto za gharama za matibabu.


.jpeg)
.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...