WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia elimu na ujuzi walioupata kuanzisha shughuli za kiuchumi na kubuni njia za kutatua changamoto mbalimbali za jamii badala ya kutegemea ajira pekee.

Amesema mabadiliko katika soko la ajira yanawahitaji wahitimu kuwa wabunifu, kujiamini na kuthubutu kutekeleza mawazo yao, badala ya kukata tamaa wanapokabiliwa na changamoto.

Dkt. Mwigulu ametoa rai hiyo leo (Jumamosi, Novemba 28, 2026) wakati akihutubia Mahafali ya 12 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo, Tabora (AMUCTA), yaliyofanyika mkoani Tabora.

Amesema tofauti na miaka ya nyuma, ambapo baadhi ya wanafunzi walikuwa wakipata nafasi za ajira kabla hata ya kuhitimu masomo, hivi sasa idadi ya wahitimu imeongezeka na ushindani katika soko la ajira umekuwa mkubwa.

Amesisitiza kuwa hali hiyo haipaswi kuwakatisha tamaa vijana, bali iwahimize kutumia maarifa na ujuzi wao kujitengenezea fursa za kiuchumi na kushiriki katika kutatua changamoto zinazokabili jamii.

Amewataka wahitimu kutoruhusu hofu au kukata tamaa kuwazuia kutekeleza mawazo yao ya ubunifu kabla hata ya kuyajaribu, akisema wanapaswa kuwa na uthubutu na uvumilivu katika kufikia malengo yao.

Waziri Mkuu pia amewataka wahitimu kuondokana na mtazamo wa kujidharau au kuamini kwamba hawawezi kupata ajira bila kuwa na watu wanaowafahamu katika taasisi zinazotoa nafasi za kazi.

“Nataka kila mmoja wenu ajiamini. Ukijikadiria kadirio la chini wewe mwenyewe, mwingine akikutazama hakuoni. Jiamini,” amesema.

Akielezea uzoefu wake, Dkt. Mwigulu amesema aliwahi kuomba nafasi ya kazi ya mchumi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati akiwa bado hajakamilisha masomo yake ya shahada ya uzamili, licha ya tangazo la kazi hiyo kuhitaji mwombaji mwenye uzoefu wa angalau miaka mitatu.

Amesema aliamua kuomba nafasi hiyo na kufanya mtihani wa maandishi, ambapo alifaulu na kuitwa kwenye usaili wa ana kwa ana.

Ametumia mfano huo kuwasisitiza wahitimu kutojiondoa katika ushindani wa kupata fursa kutokana na hofu ya kushindwa au dhana kwamba hawana uwezo wa kushindana na wengine.

Aidha, amewahimiza wahitimu kutambua thamani ya elimu waliyoipata na kuendelea kujifunza ili kuongeza uwezo wao wa kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Amesema wahitimu wanapaswa kutumia maarifa yao kwa manufaa ya jamii na Taifa, huku wakizingatia umuhimu wa kuwa wabunifu katika kutafuta njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amekipongeza Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo kwa mchango wake katika kuandaa wataalamu wa elimu maalum na jumuishi, akisema taaluma hiyo ina umuhimu katika kuongeza fursa za elimu kwa watu wenye mahitaji maalum.

Amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika utoaji wa huduma za elimu na itaendelea kushirikiana nazo katika kuimarisha ustawi wa jamii.

Awali, Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo, Padri Profesa Juvenalis Asantemungu, amesema chuo hicho kinaendelea kuimarisha utoaji wa elimu maalum na jumuishi ili kuongeza idadi ya wataalamu wenye uwezo wa kuhudumia watu wenye mahitaji maalum.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 714 wanatunukiwa stahiki mbalimbali za kitaaluma, wakiwemo 676 wa Shahada ya Elimu ya Mahitaji Maalum.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...