Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imetangaza fursa mbili kubwa za uwekezaji kwa sekta binafsi, zikihusisha mradi wa kuhudumia eneo la viwanda la Nala na mradi wa kupunguza upotevu wa maji unaofikia asilimia 35.5.
Akizungumza katika mkutano wa Wahariri wa vyombo vya habari uliokuwa umeandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi(PPPC)Mhandisi Yohana Msangula kutoka Kitengo cha Maendeleo ya Miundombinu DUWASA amesema lengo ni kuwafikia wananchi wengi zaidi wa Dodoma.
Amesisitiza wawekezaji na wananchi wa kawaida wote wanapaswa kunufaika na uwekezaji huo huku akifafanua DUWASA inahudumia Dodoma mjini pamoja na miji ya pembezoni ya Kibaigwa, Bahi, Chamwino na Kongwa.
“Mamlaka ilifanya utafiti wa kina kabla ya kuingia moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi hiyo miwili,”amesema na kuongeza eneo la kwanza ni eneo la viwanda la Nala, lenye takriban viwanda 33 katika ekari 771.
Pia amesema eneo hilo halina miundombinu ya kutosha ya maji, jambo linalokwamisha shughuli za wawekezaji waliopo.
Amefafanua DUWASA imekuwa ikipokea maombi makubwa kutoka kwa wawekezaji, ambapo mmoja anaweza kuomba asilimia 10 hadi 20 ya maji yote yanayozalishwa na mamlaka hiyo.”Ombi la aina hii ni nje ya uwezo wa DUWASA, ndiyo maana sekta binafsi imeonekana kuwa suluhisho linalofaa.
“Kwa makadirio ya sasa, mahitaji ni mita za ujazo 20,000, sawa na lita milioni 20 hadi 24 kwa siku, kutokana na wawekezaji waliopo pekee. Mradi huo una vipengele viwili vikuu, ambavyo ni usambazaji wa maji safi na uchakataji wa maji taka.”
Kwa mujibu wa usanifu wa awali, mradi unahitaji uwekezaji wa takriban Shilingi Bilioni 14 bila VAT. Miundombinu itakayojengwa ni pamoja na visima 13, matanki mawili makubwa ya lita milioni 5 kila moja yatakayowekwa mlimani, na tangi la lita milioni 10 karibu na eneo la viwanda.
Pia kutajengwa mtandao wa kukusanya maji taka na mtambo wa kuyachakata wenye uwezo wa mita za ujazo 20,000 kwa siku. Maji yatakayochakatwa yatatumika kwa kilimo na uhifadhi wa mazingira.
Msangula ameongeza mwekezaji hahitaji kuweka Sh.bilioni 14 zote kwa mara moja, kwani uwekezaji unaweza kufanyika kwa awamu. Kwa sasa DUWASA inahudumia kiwanda kimoja kikubwa kwa kutumia visima viwili, hivyo upanuzi unaweza kwenda sambamba na mahitaji.
Ametaja faida kuu tatu kwa wawekezaji ni wateja wa uhakika kwa kuwa viwanda vipo na Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji Dodoma, mapato kutoka vyanzo viwili yaani mauzo ya maji safi na ada ya uchakataji wa maji taka, na gharama ndogo za uendeshaji kwa sababu mfumo umesanifiwa kutumia mteremko wa asili badala ya pampu nyingi.
Amesema mradi wa pili ni wa kupunguza upotevu wa maji na kuongeza makusanyo. Kwa sasa DUWASA inapoteza asilimia 35.5 ya maji yake, na lengo ni kushusha hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2031.
“Uchunguzi umebaini asilimia 75 ya upotevu huo ni wa kibiashara, yaani maji yanamfikia mteja lakini hayalipiwi kutokana na mita mbovu au wizi. Asilimia 25 pekee ni upotevu wa kimwili unaotokana na mabomba kupasuka.
“Ili kuthibitisha uwezekano wa mradi, DUWASA na wadau waliwekeza Sh.milioni 29 kununua mita janja katika eneo dogo la majaribio (DMA). Matokeo yalikuwa makubwa, kwani sasa mamlaka inapata faida ya ziada ya Sh.milioni 44 kila mwezi kutokana na maji yaliyokuwa yanapotea.
“Kutokana na mafanikio hayo, DUWASA imeanzisha Mfuko wa Mzunguko, ambapo faida ya milioni 44 huwekwa kwenye akaunti maalum na kutumika kununua mita nyingine kwa maeneo mengine. Mpango wa jumla ni kubadilisha mita 50,000 za wateja.
Mhandisi Msangula amewaomba wawekezaji kuleta teknolojia nzuri ya mita za kisasa, akisema wateja na vyanzo vya maji vipo, na malipo yanahakikishwa kwa kuwa mteja hulipia kabla ya kutumia maji.
Amesema hiyo ni biashara yenye uhakika, na akawakaribisha wadau wote wenye nia kufika ofisi za DUWASA kupata taarifa za kina za usanifu wa awali.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...