Awaasa kuwa Waadilifu, kuheshimu watu, kutumia teknolojia kwa busara...
Awashauri kutokimbilia mafanikio ya haraka
Afurahishwa na kupongeza maboresho ya miundombinu ya Shule hiyo kama mmoja wa Wanafunzi waliosoma hapo

Na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake kutumia vema maarifa waliyopata kutoka katika shule hiyo kama mwanzo wa safari na si kikomo cha ndoto.

Mhe. Masaju alieleza hayo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza alipokuwa akitoa hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza shule ambayo naye alisoma katika safari yake ya kitaaluma.

“Leo nimesimama kama mmoja wa watu ambao safari yao ilipita katika shule hii. Sitaki mnaponisikia mseme tu kwamba mwanafunzi wa zamani wa Lake amefika katika nafasi hii. Nataka mjifunze jambo pana zaidi: safari ya maisha hujengwa kwa hatua, kwa watu wanaotusaidia, kwa maamuzi tunayofanya na kwa juhudi tunazoweka kila siku. Msifikiri kwamba lazima muanze mkiwa na kila kitu. Anzeni kwa kutumia vizuri kile mlicho nacho, muda wenu, nafasi ya kujifunza, ushauri mnaopewa na vipaji mlivyonavyo,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao kuendelea kujifunza, kuwa waadilifu, kutobadili misingi yao kwa faida ya muda mfupi, kuheshimu watu, kutumia teknolojia kwa busara, kuipenda Tanzania kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu sheria, kulinda mali za umma na kutatua matatizo ya jamii.

“Msisubiri mazingira yawe kamili ndipo mfanye bidii. Jengeni uwezo wenu katika mazingira mliyopo, huku mkiboresha mazingira hayo kwa manufaa ya wengine,” amesisitiza Jaji Mkuu na kusema kwamba, angependa siku zijazo, asikie simulizi za wahitimu wa leo: walioboresha huduma za afya, waliobuni teknolojia, walioanzisha biashara na ajira, waliotetea haki, waliofundisha vizazi vipya na walioleta mabadiliko chanya katika jamii zao. Hizo ndizo simulizi zinazojenga heshima ya taasisi.

Ameongeza kuwa, Kidato cha Nne ni hatua muhimu, lakini si mwisho wa elimu wala mwisho wa kujijenga. Ni mlango unaofunguka kuelekea hatua nyingine. Amesema, “baadhi yenu mtaendelea na Kidato cha Tano na Sita; wengine mtachagua mafunzo ya ufundi na stadi; wengine mtajiandaa kwa njia nyingine za kujifunza na kujenga taaluma. Njia zinaweza kutofautiana, lakini wajibu ni mmoja: kuendelea kujifunza na kujitengeneza.”

Aidha, amewakumbusha wahitimu hao kutokimbilia kutafuta mafanikio yanayoonekana kabla hawajajenga msingi wa mafanikio ya kweli kwakuwa Dunia ya sasa inaweza kumfanya kijana aamini kwamba mafanikio ni kuonekana, kuwa maarufu au kupata fedha haraka. Amesema, huo si msingi salama wa maisha kwani mafanikio ya kudumu yanahitaji maarifa, ujuzi, nidhamu, uvumilivu, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayewaangalia.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewaasa Wahitimu hao wa Kidato cha Nne kumcha Mungu na wawe na dhamira inayowaongoza kutenda yaliyo mema huku akinukuu Biblia Takatifu, katika Mithali 4:13, inayohimiza kuishika elimu na Qur’ani Tukufu, katika Suratul Al-Alaq (96:1–5), inatukumbusha umuhimu wa kusoma na kujifunza ambapo mafundisho hayo yanatuelekeza kuona elimu kama wajibu na neema inayopaswa kutumiwa kwa busara. Vilevile, amewataka kuwaheshimu wazazi, walezi na walimu wao na kusisitiza kuwa heshima si udhaifu; ni alama ya ukomavu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao kutosubiri Taifa liwaite viongozi ndipo waanze kuonesha uongozi hivyo, amewasisitiza kuanza kuongoza maisha yao kwa nidhamu, kwa kuwa waaminifu, kwa kuwaheshimu wengine na kwa kutimiza wajibu wao kwakuwa Uongozi huanza kabla ya cheo.

Akiizungumzia Shule ya Sekondari Lake, Jaji Mkuu amesema anaiheshimu na kusisitiza Lake isiwe shule inayojivunia tu watu waliopita hapo bale iwe shule inayowaandaa watu ambao Taifa litajivunia kesho. “Kila mhitimu anayekuwa muadilifu, kila mtaalamu anayefanya kazi kwa ubora, kila kiongozi anayewajibika na kila kijana anayebuni suluhisho jipya, anaongeza ukurasa katika historia ya Lake,” amesisitiza.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewakumbusha watu mbalimbali waliomaliza katika shule hiyo na katika shule nyingine nchini kuwa na utaratibu wa kuzitembelea shule walizosoma. Amesisitiza kwa kusema, “Tunaporejea mashuleni tulikosoma, tunapata fursa ya kutoa shukrani na kukutana na wale waliochangia kutujenga.”

Jaji Mkuu amesema, amerudi shuleni hapo akiwa na dhamira ya kutoa shukrani, kutambua mchango wa shule hiyo na, muhimu zaidi, kuwaambia wanafunzi wa leo kwamba ndoto zao zinaweza kuwapeleka mbali zaidi ya mipaka wanayoiona sasa.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameushukuru Uongozi wa Shule hiyo kwa kumualika na kumpa nafasi ya kurejea katika Shule ya Sekondari Lake mahali pa kumbukumbu, malezi na sehemu ya safari ya maisha yake na wengine wengi waliopita katika shule hiyo. Ameomba shule hiyo iendelee kung’aa, si kwa historia yake tu, bali kwa ubora wa watu inaowaandaa kwa ajili ya Tanzania.

“Nimepokea mwaliko huu kwa heshima kubwa. Lakini niseme wazi: kwangu mimi, leo si siku ya kutembelea shule nyingine tu; ni siku ya kurejea mahali ambapo sehemu ya safari yangu ya maisha ilianzia. Kabla ya vyeo vyetu, kabla ya ofisi zetu, kabla ya majukumu yetu kitaifa na kabla ya heshima tuliyokuwa nayo, tulikuwa wanafunzi. Nasi pamoja na Madaraka yetu tulikuwa vijana wenye safari mbele yetu, wenye mambo ya kujifunza, wenye ndoto na wenye wajibu wa kufanya bidii,” amesema Mhe. Masaju.

“Ningependa niwaambie jambo moja mapema: msinitazame leo kwa kuona tu cheo nilichonacho. Nitajeni pia kama mmoja wa wanafunzi waliowahi kukaa madarasani hapa, kusoma, kufundishwa na kuandaliwa kwa maisha. Cheo ni dhamana ya leo; lakini historia ya mtu hujengwa hatua kwa hatua, na mara nyingi hatua hizo huanzia katika madarasa kama haya,” ameeleza.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekiri kupokea kwa furaha taarifa ya wazo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Lake (Lake University) ambapo amewapongeza viongozi na wadau wa shule kwa kuwa na ndoto hiyo. Amesema, Taasisi inayothubutu kufikiria hatua inayofuata inaonesha kuwa haitaki kuishi kwa kutegemea historia pekee; inataka kushiriki katika kuandika historia mpya.

“Nimeelezwa pia kuhusu changamoto ya eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya mradi huo. Changamoto hiyo isitumike kuzima ndoto, bali iwe nafasi ya kutathmini upya mpango. Hata hivyo, ndoto ya chuo kikuu inahitaji maandalizi ya kitaalamu na ya muda mrefu: upembuzi yakinifu, mahitaji ya jamii na soko la ajira, maeneo ya kitaaluma yatakayopewa kipaumbele, uwezo wa kifedha, miundombinu, rasilimali watu, usimamizi na utii wa taratibu za mamlaka husika,” amesisitiza.

Ameushari uongozi wa shule hiyo uandae mpango kabambe wa hatua kwa hatua, ukiangalia mahitaji ya sasa na ukuaji wa taasisi kwa miaka mingi ijayo. Eneo la chuo lisitazamwe kwa mahitaji ya leo pekee; litazamwe kwa uwezo wa kupanuka, usafiri, huduma, mazingira na mahitaji ya wanafunzi na wafanyakazi. Ndoto kubwa inahitaji maandalizi makubwa, lakini utekelezaji wake uanze kwa hatua zinazopimika.

Kadhalika, ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kuwekeza katika walimu, maabara, maktaba, teknolojia, michezo, ushauri nasaha na mazingira salama ya kujifunzia na si kuwekeza katika majengo pekee bali wawekeze pia kwa watu, mifumo na maadili yanayofanya majengo hayo yawe na maana.

Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma amesema jumla ya Wanafunzi 76 wamehitimu kidato cha nne, 30 Wanawake na 46 Wanaume.

Mwalimu Bunuma amemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwa heshima na fadhila kubwa ambayo amefanya kwa uongozi wa shule hiyo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu.

“Tunajua una majukumu mengi na katika shughuli zako ikiwa ni pamoja na familia, bado umetupa kipaumbele siku hii ya leo, na umetupa hadhi kubwa ya kitaifa, wewe ambaye ulikuwa mwanafunzi wa shule hii, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wengine waliosoma hapa na wamehudhuria mahafali ya leo,” amesema Mkuu wa Shule huyo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Taaluma, Mwalimu Bunuma ameishukuru Bodi ya Wamiliki ya Shule hiyo kwa kuboresha mazingira mazuri yanayohamasisha wanafunzi kujifunza na kufundisha. “Tumepata ushindi wa daraja la kwanza, la pili, la tatu pekee kwa mwaka 2025. Kidato cha nne na cha sita ufaulu wetu ni asilimia 100. Kwa mfano mwaka 2025, kidato cha nne daraja la kwanza tulikuwa na wanafunzi 44, daraja la pili wanafunzi 33, daraja la tatu wanafunzi 4. Kidato cha sita daraja la kwanza walikuwa ni wanafunzi 20, daraja la pili walikuwa ni wanafunzi 36, na daraja la tatu walikuwa ni wanafunzi 10,” amesema.

Katika Mahafali hayo Kadhalika Jaji Mkuu alipata wasaa wa kutembezwa katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo ikiwemo Maabara, Maktaba na sehemu nyingine kadhaa ambapo alijionea maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika shule hiyo. Kadhalika, Mhe. Masaju amekutana na Mwalimu aliyemfundisha Somo la Kemia (Chemistry), Mwalimu Kiran Mody ambapo ameonesha furaha baada ya kukutana na Mwalimu huyo.

Miongoni mwa Viongozi waliosoma katika shule hiyo ni pamoja na Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Dkt. Stegomena Tax, aliyekuwa waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, lakini pia alikuwa katibu mtendaji wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Angelina Mabula na wengine kadhaa.

Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Wahitimu, Wanafunzi na Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora igizo la uendeshaji wa Mahakama ya Mazoezi (Moot Court).

Matukio katika picha ya Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza. Mhe. Masaju alikuwa Mgeni Rasmi wa Mahafali hayo yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.


Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza wakiwa katika Mahafali yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba yake wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.




Sehemu ya Wazazi, Walezi pamoja na Wageni Waalikwa wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.


Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Mwanza, Mhe. Ephery Kisanya akizungumza jambo wakati wa Mahafali hayo.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akisalimiana na aliyekuwa Mwalimu wake wa Somo la Kemia, Mwalimu Mstaafu wa Shule ya Sekondari Lake, Kiran Mody.



Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akipokea zawadi kama ishara ya upendo kutoka Uongozi wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza.

Sehemu ya Viongozi wa Shule ya Sekondari Lake wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Lucas Bunuma.



Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stagomena Tax akizungumza jambo wakati wa Mahafali hayo.


Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma akitoa neno wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake jijini Mwanza.


Katibu wa Baraza la Uongozi wa Shule akitoa neno.


Igizo la Uendeshaji Mahakama ya Mazoezi (Moot Court) likifanywa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lake wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.


Burudani kutoka kwa Wanafunzi wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake.



Burudani kutoka katika Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiangalia moja ya vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Shule ya Sekondari Lake.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi waliosoma (Alumni) katika Shule ya Sekondari Lake ambao ni pamoja na Mhe. Dkt. Stergomena Tax (wa tatu kushoto), Mwalimu Lucas Bunuma (wa kwanza kushoto). Aliyesimama wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni.


Jaji Mkuu akipata maelezo alipotembelea Maabara ya Shule ya Sekondari Lake tarehe 02 Novemba, 2026 alipoalikwa kuwa Mgeni Rasmi wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake kuhudhuria Mafahali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo tarehe 02 Novemba, 2026.




Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiwa katika picha za pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne pamoja na baadhi ya Viongozi wengine walioshiriki katika Mahafali hayo.


Sehemu ya picha za Makundi wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake.






(Picha na MARY GWERA, Mahakama)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...