Na Victor Masangu, Kibaha

ZAIDI ya wananchi 30,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani, wamepatiwa huduma za msaada wa kisheria bila malipo kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, awamu ya pili.

Huduma hizo zimewawezesha wananchi kupata usaidizi katika kutatua changamoto mbalimbali za kisheria, ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kupata elimu na ushauri kuhusu masuala ya kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa kampeni hiyo, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Kasilida Chimagi, amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, huku wengi wakijitokeza kupata huduma hizo.

Amesema katika zoezi la kusikiliza kero za wananchi, wamebaini changamoto mbalimbali, hususan migogoro ya ardhi, ambapo wamekuwa wakitoa ushauri na elimu ya kisheria ili kuwasaidia wananchi kupata ufumbuzi wa matatizo yao.

"Tangu tuanze kampeni hii ya msaada wa kisheria, tunaendelea vizuri na tumefanikiwa kuwapatia huduma zaidi ya wananchi 30,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha," amesema Chimagi.

Kwa upande wao, baadhi ya wanawake walionufaika na kampeni hiyo, akiwemo Judith Mwasha, wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo, wakisema imekuwa mkombozi katika kuwasaidia wananchi kupata haki zao na kutatua changamoto zinazowakabili.

Naye Eva Ombela, ambaye anakabiliwa na changamoto ya kutelekezwa na mume wake akiwa na watoto watatu, amesema ana matumaini kuwa kampeni hiyo ya awamu ya pili itamsaidia kupata haki zake za msingi.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, awamu ya pili, ilizinduliwa rasmi mkoani Pwani Oktoba 28, 2026, na Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Ulega, ikiwa na lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...