
Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) unaifanya kata hiyo kuelekea kuwa kama ‘Masaki Ndogo’, kutokana na ujenzi wa barabara za lami na mifereji ya kisasa katika mitaa mbalimbali.
Msawa ameyasema hayo Novemba 13, 2026, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi akiongozana na Kamati ya Siasa ya CCM ya kata hiyo pamoja na wenyeviti wa mitaa, ambapo alieleza kuwa ujenzi wa mifereji unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 10, huku barabara zikitarajiwa kukamilika Januari 2027.
Alisema kukamilika kwa awamu ya tatu ya mradi huo kutaiwezesha Kigamboni kunufaika na miradi mingine ikiwemo soko la kisasa la Mjimwema, uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu eneo la Machava na ujenzi wa bwawa Kichangachui kwa ajili ya kudhibiti maji yanayotiririka na kusababisha changamoto kwa wananchi.
Aidha, aliishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo, akisema kasi ya maendeleo inayoshuhudiwa sasa katika kata hiyo haijawahi kutokea.
Msawa pia aliitaka Kampuni ya Group Six International (GSI) kuongeza kasi ya ujenzi wa mifereji ili ikamilike kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua na kuwaondolea wananchi adha ya mafuriko.
Katika hatua nyingine, aliwahakikishia wakazi wa Magenge ya Juu na maeneo jirani kuwa barabara yenye urefu wa kilomita 1.6, kuanzia Mkunguni kupitia Konabaa, Tuamoyo na Raleo hadi kuungana na Machava, itawekewa lami ili kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Wakati huohuo, aliwataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Paul Makonda kuzingatia maadili mema na kujikita katika masomo badala ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi wa mafanikio yao kitaaluma.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Kata ya Kigamboni, Juma Kitumbe, amesema wanatarajia miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuleta manufaa kwa wananchi, huku akiwataka wakazi wa Kigamboni kuendelea kukiamini CCM katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...