Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amepongeza Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na Benki ya CRDB PLC kwa kuingia makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuimarisha soko la biashara ya kaboni nchini na kuvutia uwekezaji katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Masauni ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya NCMC na Benki ya CRDB iliyofanyika jijini Antalya, Uturuki.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuunganisha uwezo wa Serikali kupitia NCMC katika kusimamia na kuratibu biashara ya kaboni pamoja na utaalamu wa CRDB katika huduma za kifedha na uwekezaji.

Ameeleza kuwa Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 imeitambua biashara ya kaboni kuwa sekta muhimu katika kuvutia uwekezaji wa kijani, kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Aidha, ameitaka CRDB kubuni mifumo bunifu ya kifedha ikiwemo mikopo ya vifaa, dhamana na nyenzo nyingine zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya kaboni na kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji.

Hata hivyo, Masauni amesisitiza kuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya kaboni haupaswi kuchukuliwa kama kibali cha utekelezaji, akieleza kuwa miradi yote lazima izingatie sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na Serikali.

Ameongeza kuwa biashara hiyo inapaswa kuzingatia haki za binadamu, kulinda jamii zinazozunguka maeneo ya miradi, kuhifadhi mazingira na kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya kiuchumi na kijamii, yakiwemo ajira na uhamishaji wa teknolojia.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kitaasisi na udhibiti wa biashara ya kaboni ili kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na manufaa ya sekta hiyo yanawafikia Watanzania.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...