Na MWANDISHI WETU

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Khadija Ally Said, amewataka wanachama wa jumuiya hiyo kuwaeleza wananchi kuhusu maendeleo makubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Aidha amesema jumuiya hiyo inatambua mchango mkubwa wa kila mwanachama katika ushindi wa CCM uliomweka Rais Dk. Samia, madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana hivyo ni wakati wa kushikamana kuhakikisha Chama kinaendelea kushika hatamu.

Khadija amesema hayo jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kukabidhi tuzo maalumu za kutambua mchango wa jumuiya hiyo ngazi ya kata 23 za majimbo ya Segerea na Ilala na kuwashukuru wanachama kwa ushindi mkubwa wa CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.

"Kwa niaba ya Rais Dk. Samia, tunawashukuru sana wote walioshiriki kikamilifu kufanikisha ushindi huu. Tunajua mlijitoa kwa hali na mali kuhakikisha Chama kinashinda. Tunawakabidhi tuzo hizi kutambua mchango wenu mkubwa katika jumuiya ya Chama chetu,"amesema Khadija.

Amewataka wanachama wa jumuiya hiyo, kuyazungumzia mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambao Rais Dk. Samia, ameendelea kuyafanya hususan uboreshaji wa sekta ya elimu, miundombinu ya barabara, huduma za afya, maji, michezo na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

"Mambo haya mnayaona. Yazungumzieni wananchi wayajue. Rais Dk. Samia, anafanya mambo makubwa kuhakikisha nchi hii inasonga mbele kimaendeleo,"amesema Khadija.

Aidha amewaasa wanachama wa jumuiya hiyo kushikamana na kuwa na umoja badaya ya kuendeleza makundi yaliyotokana na uchaguzi mkuu uliopita au uchaguzi wa ndani ya Chama unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Khadija alieleza Jumuiya ya Wazazi Tanzania, imeendelea kuimarika na kuwa jumuia kinara ndani ya CCM hivyo ni muhimu wanajumuia kuwa na umoja, kupendana na kuepuka kutengezeana majungu yasiyo kuwa na tija.

Awali, Mwewnyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala, Mohamed Msophe, aliwataka wanachama wa CCM na wana jumuiya hiyo kufanya kazi kwa moyo kumsaidiai Mwenyekiti Rais Dk. Samia.

"Kila mmoja wetu awe balozi bora. Tukawe na sauti ya kukisemea Chama chetu. Tuyaseme yale yote mema na mazuri yanayofanywa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia.. Tusiruhusu Chama chetu kisemwe vibaya. Kazi aliyoifanya rais inaonekana kila mahali," ameeleza Msophe.

Msophe pia amemshukuru Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam, Khadja kwa kuilea jumuiya hiyo na kwamba katika uongozi wake imeimarika maradufu.

"Tunashukuru kwa tuzo hizi muhimu tulizokabidhiwa. Pia umeunganisha jumuiya na umeendelea kuilea kwa upendo na hekima,"amesema Msophe.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...