Jane Mwakyoma,
MKUU wa mkoa wa Rukwa Charles Makongoro amezitaka Halmashauri zote nne za mkoa wa Rukwa kuzingatia utaratibu wa uandikishaji wananchi katika mfuko wa Bima ya Afya kwa wote ili kuhakikisha wananchi wengi wanajiunga na kunufaika na huduma za matibabu kupitia mfuko huo.
Akitoa wito huo wakati wa uzinduzi rasmi wa Bima ya Afya kwa wote awamu ya pili, uliyofanyika stendi ya mabasi soko matora Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga,Makongoro alisema uandikishaji wa wananchi katika mfuko wa Bima ya Afya kwa wote uzingatie mahitaji na malengo yaliyokusudiwa na serikali kufikia dira ya 2050.
Pia alisema vituo vya Afya vinatakiwa kuhakikisha mahitaji ya dawa na vifaa tiba yanakadiliwa kwa usahihi na utafiti ufanyike kuhakikisha dawa zilizoisha muda wake zinachukuliwa hatua kabla hazijaondolewa na muda wake kuisha na kuagiza katika bohari ya dawa(MSD).
" huduma bora haziwezi kupatikana bila dawa wala vifaa tiba lazima muwe makini kuhakikisha dawa na vifaa tiba zinapatikana kulingana na mahitaji" alisisitiza Makongoro.
Aidha aliwataka NHIF kuhakikisha madai yanawasilishwa kwa usahihi,wakati na kulipwa kwa wakati ili kuviwezesha vituo vya Afya na Hospitali kuagiza dawa na vifaa tiba kwa wakati.
Awali mganga mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Robert Nelson Lwebangila alisema huduma ya bima ya Afya kwa wote kwa wananchi waliojiunga na Bima hiyo awamu ya kwanza imesaidia wananchi kupata msamaha wa matibabu ikiwa ni pamoja na gharama zamatibabu kupungua.
Alisema awamu ya pili ya uandikishaji wananchi katika Bima ya Afya itakwenda kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kupata msamaha huo wa matibabu.
Pia alisema kwa sasa wanapata faida kutokana na wananchi kutumia Bima ya afya ambapo wanapata mapato kupitia mfuko wa Bima ya Afya kwa wote na kuwataka wananchi ambao bado hajajiandikisha kujiandikisha ili kupata Bima ya Afya kwa wote.
Kwa upande wao wananchi walionufaika na Bima ya Afya walimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo ya kuwawezesha wananchi kujiandikisha katika mfuko wa Bima ya Afya kwa wote itakayowasaidia kupata matibabu kirahisi.
Walisema awali kabla ya kupata bima ya Afya walikuwa wanashindwa kutibiwa kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa lakini kwa kupata bima hiyo inakwenda kutatua changamoto ya kushindwa kupata huduma za matibabu.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...