Na Victor Masangu, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameitaka RUWASA mkoani humo kuimarisha utoaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, akisisitiza kuwa taasisi hiyo inapaswa kuweka mbele maslahi ya wananchi na kuhakikisha wanapata huduma hiyo kwa uhakika.

Aidha, Nyongo ameitaka RUWASA kuwa wabunifu katika uendeshaji wa huduma za maji kwa kuweka mikakati ya kuongeza mapato na kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea Serikali pekee kugharamia shughuli zake.

Nyongo ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha mameneja wa RUWASA kutoka wilaya zote za Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wa mkoa, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Amesema Mkoa wa Pwani una wawekezaji wengi wanaohitaji huduma ya maji safi na salama, ambao wanaweza kuwa sehemu ya kuongeza mapato ya taasisi hiyo kupitia utoaji wa huduma.

Ameeleza kuwa pamoja na Serikali kuendelea kuwekeza katika miradi ya maji, mahitaji ya huduma hiyo bado ni makubwa, hivyo RUWASA inapaswa kuimarisha mikakati ya kuwahudumia wananchi na wawekezaji.

Katika hatua nyingine, Nyongo amemtaka Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkuranga kutafuta suluhu ya changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo yake ili wananchi waondokane na utegemezi wa vyanzo vya maji visivyo salama.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Upendo Lugongo, amesema upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa vijijini mkoani humo umefikia asilimia 84.3.

Amesema RUWASA inaendelea kutekeleza Programu ya 1575 inayolenga kufikisha huduma ya maji katika vijiji 13 katika mwaka wa fedha 2026/2027, kati ya vijiji 22 vilivyo kwenye programu hiyo.

Amevitaja vijiji hivyo kuwa katika Halmashauri za Rufiji (1), Kibiti (3), Kisarawe (3), Mkuranga (3) na Mafia (3).

Aidha, amesema RUWASA inaendelea kutekeleza miradi 36 ya maji katika hatua mbalimbali, huku ikiandaa utekelezaji wa miradi mipya 24.

Amebainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, RUWASA Mkoa wa Pwani imetengewa Sh bilioni 14.64, ambapo Sh bilioni 5.51 zitatumika kutekeleza miradi 36 inayoendelea na Sh bilioni 9.13 zitaelekezwa katika miradi mipya 24.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...