Na Said Mwishehe,Michuzi TV


SERIKALI imesema dhamira yake ni kutokomeza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030, huku ikiwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesq Palamagamba Kabudi, amesema kilele cha maadhimisho kitafanyika Desemba 1, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Convention Centre, Dodoma. Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.

“Maadhimisho ya mwaka huu yataenda sambamba na jubilee ya miaka 25 ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), iliyoanzishwa mwaka 2001. Sherehe za kitaifa zitaanza Novemba 29 Dodoma, zikiwa na maonesho ya wadau, huduma za afya na elimu.”

Amesema kuanzia Novemba 24 hadi Desemba 1, shughuli pia zitafanyika katika kanda saba za TACAIDS: Mashariki, Kati, Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Magharibi na Kaskazini. Mawaziri na naibu mawaziri watashiriki, na mikoa yote itaadhimisha siku hiyo.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI, Tuendelee Kuimarisha Upatikanaji".

Pia amesema hadi Desemba 2025, asilimia 92.7 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wamepima na kujua hali zao, asilimia 99.5 ya wanaojua hali zao walikuwa wakipata ARV, na asilimia 98.2 ya walio kwenye dawa walikuwa wamefubaza VVU.

“Kati ya mwaka 2010 na 2025, maambukizi mapya yalishuka kutoka watu 98,754 hadi 33,511, na vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka 55,833 hadi 25,995. Maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yalipungua kutoka asilimia 9.1 hadi 6.2,”amesema Prof.Kabudi.

Akifafanua amesema vijana wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 33.3 ya maambukizi mapya, na asilimia 77.7 yao ni vijana wa kike. Aliwataka vijana kujikinga na kujua hali zao.

Amesema Serikali itaimarisha uwekezaji wa rasilimali za ndani na kushirikisha sekta binafsi, ili mabadiliko ya ufadhili wa kimataifa yasiathiri huduma za kinga, upimaji na matibabu.

Pia ametoa rai kwa wananchi wasimnyanyapae mtu anayeishi na VVU. "Ushindi dhidi ya UKIMWI unawezekana ikiwa tutafanya kazi kwa pamoja," amesema.









Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...