NA DENIS MLOWE, IRINGA


SERIKALI imesema inaendelea na taratibu za kibajeti ili kupeleka fedha kiasi cha Sh bilioni 4.67 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga Complex katika Manispaa ya Iringa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, aliyetaka kujua ni lini fedha hizo zilizotengwa zitafika katika jimbo hilo ili kuanza kwa ujenzi wa soko hilo.

Katika swali lake, Mbunge Ngajilo amesema Iringa Mjini imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya maeneo rasmi ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo, hali iliyowahi kusababisha migogoro, migomo na maandamano ya wamachinga.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitambua changamoto hiyo na kuahidi kupatikana kwa soko kubwa na la kisasa, jambo lililorejesha matumaini na utulivu miongoni mwa wafanyabiashara hao wanaosubiri utekelezaji wa mradi huo.

Akijibu, Dkt. Dugange amesema serikali tayari imepata eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo, imefanya tathmini na usanifu wa mradi ambao unakadiriwa kugharimu Sh bilioni 4.67, huku taratibu za kibajeti zikiendelea ili fedha hizo ziweze kupelekwa mapema na kuanza kwa ujenzi.

Aidha, Dkt Dugange amempongeza Ngajilo kwa usimamizi na uwakilishi wake kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa, akieleza kuwa hivi karibuni alifanya ziara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika manispaa hiyo na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara, vitega uchumi na masoko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Dugange amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatumia asilimia tano ya mapato ya ndani inayotengwa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo, ikiwemo ujenzi wa maeneo na vibanda bora vya kufanyia biashara.

Akitolea mfano eneo la Magufuli Bus Terminal jijini Dar es Salaam amesema limeanza kutekeleza mpango wa kujenga vibanda vidogo na vya kisasa kwa ajili ya wamachinga na wafanyabiashara wengine wadogo.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha hizo ili kuhakikisha zinatumika kwa lengo lililokusudiwa, ikiwemo ujenzi wa masoko na maeneo rafiki ya biashara katika halmashauri zote nchini.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...