Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
TANZANIA imepanga kuharakisha utekelezaji wa mpango wa kuifanya Tanga kuwa kitovu cha nishati cha Afrika Mashariki, kupitia uendelezaji wa miundombinu ya kuhifadhi, kusafirisha na kusambaza mafuta pamoja na uwekezaji katika viwanda vinavyozalisha bidhaa zitokanazo na mafuta.
Mpango huo ni miongoni mwa maeneo saba muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi yaliyokubaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wakati wa ziara ya kitaifa ya Rais Samia nchini Uganda iliyofanyika Novemba 18 na 19, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ziara hiyo, leo Novemba 24, 2026 Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mpango huo unalenga kuifanya Tanzania isiwe nchi ya kupitisha mafuta pekee, bali pia kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi zinazohusiana na nishati, viwanda na biashara.
Amesema makubaliano hayo yanahusisha kuendeleza miundombinu ya kuhifadhi mafuta, kusafirisha mafuta, kusambaza bidhaa za mafuta na kuimarisha huduma za usafirishaji na ugavi, pamoja na kushirikiana katika uzalishaji wa mbolea, plastiki, kemikali za viwandani na bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta.
Amesema uwekezaji huo unatarajiwa kufungua fursa za ajira kwa vijana katika ujenzi, uhandisi, uendeshaji wa mitambo, huduma za usafirishaji, matengenezo ya vifaa na shughuli nyingine za viwandani, huku wajasiriamali wakipata nafasi za kutoa huduma na bidhaa zitakazohitajika wakati wa ujenzi na uendeshaji wa mitambo hiyo.
Katika ziara hiyo, viongozi hao pia walipokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao umefikia asilimia 93.9 ya utekelezaji, huku wakielekeza kazi zilizobaki kukamilishwa haraka ili kuruhusu kuanza kwa usafirishaji wa mafuta.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa za shughuli za uendeshaji, matengenezo, usalama, usafirishaji na huduma za ugavi, pamoja na kuchochea uwekezaji na shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na bomba hilo.
Ameeleza kuwa maeneo mengine yaliyokubaliwa katika ziara hiyo ni kuendeleza reli ya kisasa (SGR) katika njia ya Isaka, Lusahunga, Murongo, Kikagati hadi Mpondwe yenye urefu wa kilomita 620, kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria kupitia Bandari ya Port Bell nchini Uganda, kuondoa vikwazo vya biashara, kuchochea uwekezaji katika viwanda na kuimarisha ushirikiano wa nishati, ikiwemo kuunganisha mifumo ya umeme ya kilovolti 400 katika njia ya Umulenzi, Masaka, Ibadakuli hadi Shinyanga.
Amesema utekelezaji wa makubaliano hayo utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na uzalishaji, kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania nchini Uganda na kuongeza fursa za ajira na biashara, akisisitiza kuwa mafanikio ya ziara hiyo yatapimwa kwa namna makubaliano hayo yatakavyotekelezwa na kuleta manufaa kwa Watanzania.



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...