MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kutoa elimu kwa madereva wanaosafirisha mizigo ya mpito (transit) kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi nyingine ili kuwajengea uelewa wa sheria na taratibu za forodha na kuhakikisha mizigo inafika katika nchi husika bila kukiuka masharti ya usafirishaji.
Kaimu Naibu Kamishna wa Udhibiti na Ushurutishaji wa TRA, Anangisye Mtafya, amesema baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika usafirishaji wa mizigo hiyo zinatokana na baadhi ya madereva kutofahamu taratibu wanazopaswa kuzifuata, hali inayoweza kusababisha mizigo kuingizwa nchini kinyume cha sheria.
Mtafya ameyasema hayo Novemba 11, 2026, wakati TRA ilipokutana na madereva wa magari yanayosafirisha mizigo ya transit jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwapatia elimu kuhusu sheria na taratibu za usafirishaji wa mizigo hiyo.
Amesema kumekuwa na matukio ya baadhi ya madereva kushawishiwa na watu wasio waaminifu kumwaga mizigo ya transit ndani ya nchi badala ya kuipeleka katika nchi zilizokusudiwa, jambo linalosababisha changamoto kati ya madereva na waajiri wao.
Amesema vitendo hivyo vina athari mbalimbali, ikiwemo kupoteza mapato ya Serikali kutokana na bidhaa kuingia nchini bila kulipiwa kodi, kuhatarisha afya za wananchi pale bidhaa kama chakula na dawa zinapoingia sokoni bila kupitia taasisi zinazohusika na udhibiti wake, pamoja na kuathiri ushindani wa kibiashara.
Aidha, amesema uingizaji huo wa bidhaa unaweza kuhusishwa na vitendo vya utakatishaji fedha, hivyo ni muhimu kwa madereva kufahamu wajibu wao na kuzingatia taratibu za forodha katika safari zao.
Akizungumzia umuhimu wa elimu hiyo, Mtafya amesema dereva atakayebainika kuhusika na kumwaga mzigo wa transit anaweza kuwajibishwa kwa kulipa faini, huku gari lililotumika kusafirisha mzigo huo likiwa katika hatari ya kutaifishwa kwa mujibu wa sheria. Pia, dereva anaweza kufikishwa mahakamani.
Amesema utoaji wa elimu hiyo ni endelevu na TRA itaendelea kuwafikia madereva katika vituo mbalimbali vinavyopitisha mizigo ya transit nchini.
Ametaja vituo hivyo kuwa ni pamoja na Rusumo, Mutukula na Kabanga, huku akieleza kuwa watarejea Tunduma kutokana na wingi wa mizigo inayopita katika kituo hicho. Aidha, TRA itaendelea kutumia vipeperushi kuwafikishia madereva na wadau wengine elimu kuhusu taratibu za usafirishaji.
Kwa upande wake, dereva wa malori, Nelson Impinzile, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu makosa ya kiforodha ambayo awali hakuwa na uelewa nayo, ikiwemo kuongeza mizigo kwenye mzigo wa transit na kushusha mizigo katika maeneo ambayo hayajaidhinishwa.
Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa makosa hayo yanaweza kusababisha madereva kulipa faini kubwa au kufungwa, hivyo ameiomba TRA kuendeleza mafunzo hayo mara kwa mara ili kuwajengea uelewa wa kutosha.
Naye Mwenyekiti wa Madereva Wanawake Tanzania, Naetwe Ihema, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu taratibu za usafirishaji, ikiwemo muda na mazingira yanayofaa kwa dereva kusimama au kuegesha gari wakati wa safari na umuhimu wa kuhakikisha nyaraka za gari zinaendana na taarifa zilizoandaliwa na mamlaka za forodha.
Ihema, anayewakilisha madereva wanawake wa mabasi, malori, meli, SGR, pikipiki, mitambo na madereva wa viongozi, ameiomba TRA kuendeleza elimu hiyo kupitia redio, televisheni na magazeti ili kuwafikia madereva wengi zaidi.
Amesema madereva wana muda mchache wa kupata taarifa sahihi kutokana na majukumu yao ya kila siku, hivyo utoaji wa elimu mara kwa mara utawasaidia kuongeza uelewa na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu.


.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...