Na Oscar Assenga, Tanga.

WANANCHI wanaosumbuliwa na ugonjwa wa mabusha na ngirimaji mkoani Tanga wanatarajiwa kunufaika na huduma za uchunguzi na upasuaji bila malipo kupitia kambi maalumu zitakazoanza Novemba 16 hadi 30, mwaka huu.

Kambi hizo zitafanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Handeni Vijijini kuanzia Novemba 16 hadi 22, 2026, na Hospitali ya Wilaya ya Muheza kuanzia Novemba 23 hadi 30, mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amewahimiza wananchi wenye changamoto hizo kujitokeza kwa wingi ili kupata uchunguzi na matibabu, akisisitiza kuwa huduma zote zitatolewa bila malipo.

Amesema Serikali imeandaa kambi hizo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya na kuwafikia wananchi wanaoishi na madhara ya magonjwa hayo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabusha na ngirimaji ni miongoni mwa madhara yanayosababishwa na maambukizi ya vimelea vinavyoenezwa na mbu walioambukizwa, hali inayoweza kusababisha kuziba kwa mfumo wa limfu na kuvimba kwa sehemu mbalimbali za mwili.

Imeelezwa kuwa kwa wanaume, ugonjwa huo unaweza kusababisha mkusanyiko wa maji katika mfuko wa korodani, hali inayojulikana kama ngirimaji, huku kwa wengine ukisababisha kuvimba kwa miguu, mikono na matiti kwa wanawake.

Dkt. Burian amesema madhara ya magonjwa hayo hayaishii katika afya pekee, bali pia huathiri shughuli za kiuchumi, ustawi wa familia na maisha ya kijamii ya waathirika.

Hata hivyo, amesema huduma za upasuaji zinaweza kusaidia kupunguza ukubwa wa uvimbe na kuboresha maisha ya watu wanaokabiliwa na changamoto hizo.

Amebainisha kuwa tangu kuanza kwa kambi maalumu za matibabu hayo mwaka 2009, jumla ya wagonjwa 14,454 wamepatiwa huduma nchini kote, wakiwamo 1,517 kutoka Mkoa wa Tanga.

Katika kambi hizo, wananchi watapata elimu kuhusu magonjwa hayo, uchunguzi wa awali pamoja na huduma za upasuaji kwa wale watakaobainika kuhitaji matibabu hayo.

Akisisitiza kuhusu upatikanaji wa huduma hizo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema gharama zote za uchunguzi na matibabu zitagharamiwa na Serikali, hivyo wananchi hawatapaswa kulipia huduma watakazopatiwa.

Aidha, amewataka wananchi wenye changamoto hizo kuepuka kutumia njia zisizo salama za matibabu na badala yake kujitokeza hospitalini, bila kuogopa wala kuona aibu kutokana na unyanyapaa.

Pia amewaomba viongozi na wataalamu wa afya katika ngazi zote kuanzia mkoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa kushirikiana kutoa elimu na hamasa ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kunufaika na huduma hizo.

Kambi hizo zitatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na wadau wengine wa afya.

Dkt. Burian amesisitiza wito kwa wananchi wenye dalili au changamoto za magonjwa hayo kujitokeza katika vituo vilivyopangwa ili kupata uchunguzi na matibabu ya kitaalamu bila gharama yoyote.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...