Na Hellen Mtereko, Mwanza
WAHITIMU wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa jijini Mwanza, wameaswa kutumia elimu na ujuzi walioupata kuwa wabunifu, kutatua changamoto za jamii na kuchangamkia fursa zilizopo ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Novemba 27, 2026, na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Amina Makilagi, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Omari, wakati wa Mahafali ya 40 ya chuo hicho, duru ya pili, yaliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
Makilagi amesema wahitimu wanapaswa kuwa mabalozi wa maarifa na maadili katika jamii, huku wakitumia elimu waliyoipata kujiajiri, kuajiri wengine na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
Amesisitiza kuwa wahitimu hawapaswi kusubiri fursa ziwafuate, bali wanapaswa kuzitafuta, kuzitumia na pale wanapokosa wazitengeneze kwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni.
"Msisubiri fursa zije kwenu, nendeni mkazione na kuchangamkia fursa zilizopo na endapo mtazikosa zitengenezeni kwa kutumia elimu na maarifa mliyoyapata hapa chuoni," amesema Makilagi.
Aidha, amewakumbusha kuwa thamani ya elimu yao haitapimwa kwa vyeti walivyopata, bali kwa mchango wao katika kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Hozen Mayaya, amesema kituo hicho kinajivunia kuhitimisha masomo kwa jumla ya wahitimu 2,966, wakiwemo wanaume 1,191 na wanawake 1,775, waliokamilisha masomo katika fani mbalimbali.
Amesema wahitimu wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuwajengea maarifa, ujuzi na umahiri unaohitajika katika maeneo yao ya kitaaluma na kitaalamu.
Profesa Mayaya ameeleza kuwa mafunzo hayo yametekelezwa kupitia mitaala inayozingatia mfumo wa elimu na mafunzo yanayojengwa katika umahiri (Competence-Based Education and Training), unaowawezesha wanafunzi kupata maarifa ya kinadharia darasani na kuyathibitisha kupitia mafunzo ya vitendo uwandani na katika maeneo ya kazi.
Aidha, amesema kupitia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwa ufadhili wa Wizara ya Fedha, kituo hicho kimefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Hosteli Na. 1 yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 204, iliyogharimu Sh bilioni 2,035,800,406.32.
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo zinazowezesha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya chuo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake, Yahya Kabelele, aliyehitimu Shahada ya Kwanza ya Mipango ya Maendeleo ya Mikoa, amesema jamii inapaswa kutarajia matokeo chanya kutoka kwa wahitimu hao, akieleza kuwa elimu waliyoipata itakuwa nyenzo muhimu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Amina Makilagi akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha Balozi Khamisi Omari kwenye mahafali ya 40 ya Chuo Duru ya Pili katika Kituo cha mafunzo Kanda ya Ziwa MwanzaBaadhi ya wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wakiwa ukumbini
Wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa Mwanza wakifurahia kuhitimu
Mkuu wa Wilaya ya Magu Amina Makilagi akitoa cheti kwa mmoja wa wahitimu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini MwanzaPicha ya pamoja






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...