
Na Mwandishi Wetu, Kigamboni
ZAIDI ya wananchi 2,000 wenye matatizo mbalimbali ya macho wamepatiwa matibabu bure na kugawiwa miwani kupitia kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika katika Kituo cha Afya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo, Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, amesema huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kipato cha chini ambao wasingeweza kumudu gharama za matibabu ya macho, ambazo zinaweza kufikia kati ya Sh. 400,000 na 500,000 kwa mtu mmoja.
Amesema huduma hizo zimepatikana kupitia msaada wa Serikali ya Kuwait kwa kushirikiana na taasisi ya Majay Foundation, kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Kigamboni na maeneo jirani kupata huduma za afya bila malipo.
Dotto amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali, akisema hatua hiyo imechangia upatikanaji wa misaada inayowanufaisha wananchi wenye uhitaji.
Amesema kambi hiyo haikuhudumia wakazi wa Kata ya Kigamboni pekee, bali pia wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, yakiwemo Pembanazi, Kisarawetu na Vijibweni, baada ya taarifa za huduma hizo kusambazwa katika maeneo mbalimbali.
Ameongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), pamoja na kuunga mkono shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika.
Kwa upande wake, Daktari Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kigamboni, Peter Nyang’anyi, amesema kambi hiyo imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 2,000 waliopata huduma mbalimbali, zikiwemo vipimo vya macho, miwani, ushauri wa kitaalamu, matibabu na upasuaji kwa wagonjwa waliohitaji huduma hiyo.
Amesema baadhi ya matatizo ya macho yanaweza kutokana na changamoto za kuzaliwa nazo, ambazo wakati mwingine huhusishwa na mambo mbalimbali yanayotokea wakati wa ujauzito.
Aidha, amewataka wananchi kuzingatia elimu ya afya, kutumia lishe bora, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuwahi hospitalini wanapobaini changamoto za kuona.
Naye Daktari wa Macho na Mratibu wa Huduma za Macho katika Manispaa ya Kigamboni, Josephine Ngonyani, amesema sekta ya huduma za macho inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo gharama kubwa za matibabu, wingi wa magonjwa ya macho na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu matatizo hayo na maeneo sahihi ya kupata matibabu.
Amesema kambi hiyo pia imetoa elimu kuhusu ugonjwa wa presha ya macho (Glaucoma), ambao umekuwa ukizungukwa na dhana potofu katika jamii, huku baadhi ya watu wakiuhusisha na imani za kishirikina badala ya kuutambua kama tatizo la kiafya linalohitaji uchunguzi na matibabu ya kitaalamu.
Mmoja wa wananchi walionufaika na huduma hizo, Catherine Mwenda, amesema awali alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya jicho la kushoto, lakini hali yake imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu kutoka kwa madaktari.
"Nilipata taarifa kuwa kuna huduma za upimaji na matibabu ya macho bure hapa, nami nikafuatilia na hatimaye nikapata huduma nzuri sana. Kwanza wanatujali sisi wazee na tumekuwa tukihudumiwa vizuri," amesema Catherine.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...