Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewataka wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni hapo kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ili kuchochea maendeleo ya Taifa.

Aidha, amewataka wahitimu hao kuzingatia misingi ya uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa wanapoingia katika soko la ajira, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha mchango wa elimu katika maendeleo ya Taifa.

Balozi Omar ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya 52 ya chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa Watanzania, hivyo ni wajibu wa wahitimu kuhakikisha wanatumia maarifa na ujuzi walioupata kwa manufaa ya Taifa.

Ameutaka uongozi wa IFM kuendelea kuboresha mitaala na mifumo ya ufundishaji ili iendane na mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya soko la ajira lenye ushindani mkubwa.

Pia, amesisitiza kuwa chuo hicho kinapaswa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 katika mipango yake ya muda mfupi na mrefu, hususan katika kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kuchangia utekelezaji wa malengo ya dira hiyo.

"Jamii ina changamoto nyingi ambazo wataalamu wetu wanapaswa kuzitumia kama fursa za kuzitatua kwa kubuni teknolojia na mifumo mbalimbali itakayorahisisha maisha ya watu," amesema.
Katika hatua nyingine, Balozi Omar amekubali kufanyia kazi ombi la chuo hicho la kupatiwa matumizi ya baadhi ya majengo ya Serikali yaliyokuwa yakitumika kabla ya taasisi husika kuhamia katika maeneo mengine.

Vilevile, ameahidi kushughulikia ombi la kuongeza watumishi ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la wanafunzi, kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa IFM, Profesa Henry Chalu, amesema chuo hicho kitaendelea kuimarisha mifumo ya elimu inayolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema IFM pia kinaendelea kuhamasisha tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto zilizopo katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Profesa Chalu amesema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho imeendelea kuongezeka kila mwaka, ambapo kwa mwaka wa masomo 2026 imefikia jumla ya wanafunzi 10,000.

Ameeleza kuwa katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 4,536 wamehitimu masomo yao katika kampasi za Dar es Salaam na Zanzibar, huku wanawake wakiwa asilimia 43 ya wahitimu wote.

Amesisitiza kuwa chuo hicho kitaendelea kusimamia misingi ya elimu inayowawezesha wanafunzi kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika mazingira halisi ya kazi na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...