*Aitaka IFM kuzalisha wataalamu wa Dira ya 2050.Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb). amewataka wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kujiepusha na vitendo vya rushwa na matumizi ya dawa za kulevya wanapoingia katika soko la ajira, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha mchango wa elimu katika maendeleo ya Taifa.
Balozi Omar ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya 52 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa Watanzania, hatua inayohitaji wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kwa manufaa ya Taifa.
Aidha, amekitaka chuo hicho kuendelea kuboresha mitaala na mifumo ya ufundishaji ili iendane na mabadiliko ya teknolojia pamoja na mahitaji ya soko la ajira lenye ushindani mkubwa.
Amesisitiza kuwa IFM kinapaswa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 katika mipango yake ya muda mfupi na mrefu, hususan katika kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kutekeleza malengo ya dira hiyo.
"Jamii ina changamoto nyingi ambazo wataalamu wetu wanapaswa kuzitumia kama fursa za kuzitatua kwa kubuni teknolojia na mifumo mbalimbali itakayorahisisha maisha ya watu," amesema.
Katika hatua nyingine, Balozi Omary amekubali kufanyia kazi ombi la chuo hicho la kupata matumizi ya baadhi ya majengo ya Serikali yaliyokuwa yakitumika kabla ya taasisi hizo kuhamia katika maeneo mengine.
Pia, ameahidi kufanyia kazi ombi la kuongeza watumishi ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la wanafunzi, kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa IFM, Profesa Henry Chalu, amesema chuo hicho kitaendelea kuimarisha mifumo ya elimu inayolenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Amesema chuo hicho pia kinaendelea kuhamasisha tafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto zilizopo katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Profesa Chalu amesema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho imekuwa ikiongezeka kila mwaka, ambapo kwa mwaka wa masomo 2026 kimefikia jumla ya wanafunzi 10,000.
Ameongeza kuwa katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 4,536 wamehitimu katika kampasi za Dar es Salaam na Zanzibar, huku wanawake wakichangia asilimia 43 ya wahitimu wote.
Amesema IFM kitaendelea kusimamia misingi ya elimu inayowawezesha wanafunzi kutumia maarifa waliyoyapata katika mazingira halisi ya kazi na kutatua changamoto zinazokabili jamii.



.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...