Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma umetoa elimu ya vipimo sahihi kwa maafisa usafirishaji ili kuwajengea uelewa wa umuhimu wa kuhakiki vipimo wanaponunua bidhaa mbalimbali kwa niaba ya wananchi, zikiwemo gesi ya kupikia, nyama, vyakula na nafaka, hatua inayolenga kulinda haki za walaji na kupunguza udanganyifu katika biashara.

Akizungumza Novemba 17, 2026, wakati wa kutoa elimu hiyo Kaimu Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Edward Patrick, amesema maafisa usafirishaji ni wadau muhimu katika kufikisha elimu ya vipimo sahihi kwa jamii kutokana na nafasi yao ya kuunganisha wauzaji na walaji katika shughuli za kila siku, amesema wanapaswa kuhakikisha wanashuhudia upimaji wa bidhaa wanazonunua ili kujiridhisha kuwa kiasi wanachopokea kinalingana na kile walicholipia.

Amesema changamoto ya upungufu wa bidhaa kama gesi na nyama inaweza kupungua iwapo maafisa hao watahakikisha wanapimiwa bidhaa wanaponunua badala ya kuamini maelezo ya wauzaji pekee, aidha amewataka kukagua mizani inayotumika kuhakikisha ina stika ya WMA inayoonesha kuwa imehakikiwa, imewekwa katika hali sahihi na iko tayari kutumika kabla ya upimaji kuanza.

Patrick amesema WMA inaendelea kupanua wigo wa utoaji elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo wanafunzi kupitia klabu za vipimo shuleni na madiwani, ili kuwajengea wananchi uelewa wa haki zao na umuhimu wa kutumia vipimo sahihi, ameongeza kuwa Wakala unaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaokiuka sheria za vipimo, ikiwemo kuwafikisha mahakamani na kuwatoza faini, kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja anazingatia matumizi ya vipimo sahihi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji Mkoa wa Dodoma, Baraka Obadia Mbuye, amesema elimu hiyo imewajengea uelewa kuhusu wajibu wao katika kuhakikisha bidhaa wanazonunua kwa niaba ya wateja zinakuwa na vipimo sahihi, amewataka maafisa usafirishaji kuwa makini wanaponunua bidhaa, kushuhudia upimaji na kukagua alama za uhakiki wa WMA kwenye mizani na vifaa vya kupimia mafuta katika vituo vya mafuta ili kujiridhisha na usahihi wa vipimo.

Naye Msemaji Mkuu wa Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Simon Elias Mangula, ameishukuru WMA kwa kuwashirikisha katika elimu hiyo, akisema madereva wana nafasi muhimu ya kusaidia kulinda haki za wananchi kutokana na kushiriki mara kwa mara katika manunuzi ya bidhaa mbalimbali, hata hivyo, ameiomba WMA kuongeza ukaguzi katika masoko ya vijijini ambako wakulima wanakabiliwa na changamoto za vipimo wanapouza mazao yao, pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi za bodaboda na bajaji katika kufikisha elimu hiyo kwa jamii.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Wakala wa Vipimo na maafisa usafirishaji ni muhimu katika kujenga jamii inayozingatia vipimo sahihi, huku akiwataka madereva wa bodaboda na bajaji kuwa waaminifu wanapotekeleza maagizo ya wateja, kuhakikisha bidhaa zinapimwa kwa usahihi na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha hasara kwa wananchi, Utekelezaji wa elimu hiyo unatarajiwa kusaidia kuongeza uelewa wa walaji, kupunguza malalamiko na kuimarisha haki katika shughuli za manunuzi na biashara.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...