Na Mwandishi Wetu, Kigoma

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Ofisi ya Mkoa wa Kigoma, limekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kuzama kwa boti iliyodaiwa kuwa imebeba watu 40 katika Ziwa Tanganyika.

TASAC imesema taarifa hizo ni za uzushi na hazina ukweli, huku ikifafanua kuwa taarifa iliyotolewa na Ofisi hiyo Septemba 23, 2026, ilihusu tukio la meli nyingine iliyokuwa ikijulikana kwa jina la MV MJP, iliyokuwa imeondoka Bandari ya Kigoma kuelekea maeneo ya Mto DRC.

Kwa mujibu wa taarifa ya TASAC iliyotolewa jana, Septemba 25, 2026, meli hiyo iliondoka Bandari ya Kigoma majira ya saa mbili usiku wa Septemba 22, 2026, ikiwa na mzigo mchanganiko wenye uzito wa tani 492.838, abiria 34 na mabaharia 15.

TASAC imeeleza kuwa ilipokea taarifa kuhusu meli hiyo Septemba 23, 2026, na kufanya mawasiliano na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhusu ajali hiyo.

“Mpaka kufikia leo tarehe 25 Septemba 2026 saa 2:26 alasiri, mabaharia wote 15 tayari wameokolewa na jitihada za kuwatafuta watu wengine zinaendelea,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, TASAC imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na mamlaka za DRC kufuatilia tukio hilo na endapo kutakuwa na taarifa nyingine, umma utajulishwa kupitia njia rasmi za mawasiliano.

Shirika hilo pia limezitaka vyombo vya habari kuthibitisha taarifa zake kwa mamlaka za Serikali kabla ya kuzisambaza, ili kuepusha taharuki na hofu miongoni mwa wananchi.

TASAC imewahimiza wananchi wanaohitaji taarifa sahihi kuhusu usalama wa usafiri majini kutumia vyanzo rasmi vya TASAC na mamlaka husika.

Vilevile, TASAC imevitaka baadhi ya vyombo vya habari vilivyochapisha taarifa hiyo kurekebisha kupitia mitandao ya kijamii kuhusu tukio hilo ili kutoleta taharuki kwa umma.

-Afurahishwa mazingira mazuri ya Future World Vocation Istitute,aahidi kupeleka vijana kusoma


Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam Bakari Shingo ametoa mwito kwa madereva wote nchini kuhakikisha wanarudi darasani kuongeza ujuzi utakaowezesha kuendesha vyombo vya moto kwa usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

Amesisitiza kuna tofauti kubwa ya magari ya miaka ya nyuma na sasa hivyo kwa madereva ili kwenda sambamba na kasi ya teknolojia inayotumika kutengeneza magari njia pekee ya madereva kuifanya kazi hiyo kwa weledi na umakini ni kuhakikisha wanarudi darasani kwani hakuna njia mbadala.

Akizungumza Septemba 25,2026 alipotembelea Chuo cha Ufundi Stadi Future World Vocation institute kilichopo Chanika kwa Ndevu jijini Dar es Salaam ambapo pia akiwa katika chuo hicho amepata nafasi ya kuzungumza na mamia ya madereva wanaoendelea na mafunzo ya udereva ili kuuhisha leseni.

“Nimepata nafasi ya kupata elimu kuhusu masuala ya udereva.Ujue unapokuwa mwakilishi wa wananchi unapata mambo mbalimbali na kuna jambo nililetewa na madereva wenye leseni ya C plain ambao wengi wanaohoji kwanini warudishwe kusoma wakati walipochukua leseni daraja C plain walisoma kozi zote za daraja E,D na waliambiwa kozi zote za madaraja ya chini zimo ndani ya C plain.

“Nikiri baada ya kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Future World Vocation Institute Robert Mkolla amenieliemisha kuhusu nafasi ya madereva kurudi darasani hivyo nami naungana naye kuwaambia madereva warudi chuo kusoma udereva ili kuuhisha leseni zao lakini pia kuyafahamu kwa undani magari yenyewe jinsi ya kuyaendesha lakini na sharia za usalama barabarani kwa ujumla.”

Akieleza zaidi Shingo amesema yeye ni dereva tangu enzi za leseni za vitabu na kwamba magari yaliyokuwa wakiyaendesha wakati ule sio yaliyopo sasa kwani kila siku teknolojia inabadilika na hakuna mahali unaweza kupata teknolojia mpya ya magari yaliyopo zaidi ya chuoni.

Pia amesema amefurahishwa uwepo wa chuo hicho ndani ya Jimbo la Ukonga na hivyo amemuahidi Mkuu wa Chuo hicho kwamba atahakikisha anapeleka vijana wa jimbo Hilo kujifunza fani mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.

“Nimekuwa na utaratibu wa kusomesha vijana katika vyuo mbalimbali vya ufundi na mpaka sasa vijana 700 wanaendelea na mafunzo kupitia fedha za mfuko wa Jimbo,fedha za Mbunge pamoja na fedha za marafiki wa Mbunge.

“Hivyo nitazungumza na chuo hiki ili vijana ninaowafadhili wajiunge na masomo kwa ajili ya kupata ujuzi. Mimi hapa nina fani tano na zote nazifanya kwa ufasaha mkubwa na ndio maana kabla ya kuwa Mbunge nilikuwa nimeajiajiri,”amesema.

Pia Shingo ametumia nafasi hiyo kuwashauri madereva bodaboda nao kuona haja ya kujifunza fani zenye ujuzi kwani udereva bodaboda una mwisho na kwamba uwepo wa chuo hicho maeneo ya Chanika umefanya kiwe karibu na wananchi.

Kuhusu chuo hicho amesema amevutiwa na mandhari mazuri ya kufundishia akitoa mfano kwa madereva wanaojifunza kuendesha magari madogo ndani ya chuo kuna uwanja mkubwa wa kujifunzia kabla ya kutoka nje ,

Pia amefurahishwa na uwezo wa walimu wanaofundisha fani mbalimbali katika chuo hicho ikiwemo ya udereva urembo na malezi ya watoto wanatumia mbinu za kisasa za kifundisha huku akitoa rai kwa chuo hicho kutoa kozi zake katika kiwango cha kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Future World Vocation Institute Mkola amesema amefurahishwa na ujio wa Mbunge Shingo na kwa nafasi yake anayo majukwaa mengi ambayo atayatumia kuelimisha jamii ya wana Jimbo la Ukonga na maeneo mengine kuhakikisha wanapeleka vijana wao katika chuo hicho kupata ujuzi wa fani mbalimbali.

“Tumezungumza na Mbunge kuhusu nafasi yetu kama chuo katika kuhakikisha tunatoa kozi zitakazowezeha vijana wanajiajiri badala ya kusubiria kuajiriwa.Tunaomba ukawe balozi wetu,”amesema na kusisitiza kuna vijana wengi ambao wanamaliza darasa la saba na kidato cha nne ambao badala ya kujiunga na vyuo kupata ujuzi wameamua kuwa dereva bodaboda.

Amesema vijana wanapaswa kufahamu kuwa pamoja na kuwa madereva bodaboda lakini wanayo nafasi ya kusoma na fani nyingine zitakazowezesha kujiajiri .”Hatuwezi kuacha vijana wote wawe waendesha bodaboda lazima tuwashawishi wasome na kozi nyingine kwa ajili ya faida yao na taifa kwa ujumla.”








Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amewakumbusha wachimbaji wadogo mkoani Geita kuchukua tahadhari dhidi ya uwepo wa Mvua kubwa za El Nino zinazotarajia kunyesha hivi karibuni nchini.

Akifungua mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo wa madini mkoani Geita, amesema kuwa ni vizuri wachimbaji hao kuchukua tahadhari mapema ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa mvua hizo.

"Niwatake wachimbaji wote kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kufuatilia taarifa za utabiri wa Hali ya Hewa toka Mamlaka ya Hali ya Hewa, ili kuchukua tahadhari mapema. Uchimbaji wetu ni wa "underground" hivyo, ni muhimu kujiridhisha kabla ya kuanza kufanya uchimbaji. Na endapo ikatokea madhara ya aina yoyote, basi ni vyema taarifa zitolewe mapema OSHA na Mamlaka zingine husika." alisema Mhe. Deus.

Aidha, waziri huyo aliwakumbusha wachimbaji hao kutumia elimu walioipata na Vifaa Kinga vya mfano walivyopatiwa ili kuendelea kukumbushana umuhimu wa matumizi ya Vifaa Kinga na Kuchukua tahadhari.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema mafunzo hayo ni muendelezo na maelekezo ya mheshimiwa waziri katika kuyafikia makundi mbalimbali na kuyapatia elimu ikiwemo wachimbaji wadogo. Mafunzo kama hayo tayari yamekwishafanyika katika Wilaya za Bukombe na Namungo mkoani Lindi.

Bi. Mwenda amesema, wachimbaji wadogo wanakabiliwa na Vihatarishi vingi kutokana na aina ya uchimbaji wanaofanya, ndio maana OSHA iliamua kuyafikia makundi hayo na kuwapa elimu pamoja na kuwapatia PPE kwa lengo la kuhimiza matumizi ya Vifaa Kinga wakati wakitekeleza majukumu yao.

Washiriki wa mafunzo ambao wametoka katika mkoa wa Kimadini wa Mbogwe na Geita pamoja na wachimbaji toka nchi jirani ya Uganda, wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutambua na kuvidhibiti Vihatarishi sehemu za kazi pamoja na Huduma ya Kwanza.

Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Uganda nchini Tanzania, mwakilishi wa ubalozi huo, Brigedia Jenerali Julius Mbaine, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umefungua fursa ya kubadilishana uzoefu na kutambua maeneo ambayo Tanzania na Uganda zinaweza kushirikiana katika sekta ya madini.

“Sekta ya madini inatoa jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano. Ubalozi wa Uganda nchini Tanzania uko tayari kusaidia kuimarisha uhusiano wa kitaasisi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, hususan katika kukuza uwekezaji, biashara na mnyororo wa thamani wa madini.” Amesisitiza Brigedia Jenerali Julius.

Amesema mazungumzo yaliyofanyika kati ya ujumbe wa Uganda na wadau wa madini Geita yamewapa nafasi ya kuelewa zaidi sekta hiyo nchini Tanzania na kutambua maeneo ya maslahi ya pamoja.

Ushiriki wa wachimbaji wadogo wa Uganda katika maonesho hayo unalenga kuwawezesha kujifunza kutoka kwa wadau wa Tanzania na kuona namna teknolojia na maarifa yanavyoweza kutumika kuboresha shughuli za uchimbaji.

Kwa Upande wake Mbunge wa Geita Mjini Mhe. Mha. Chacha Mwita Wambura, amepongeza juhudi za OSHA katika kuendelea kusimamia Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini. Amesema kuwa yeye kama mdau wa uchimbaji wa madini anatambua umuhimu wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kutokana na maeneo hayo kuwa na vihatarishi.

Mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo yameandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya 9 ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini, yanayofanyika Mkoani Geita.







Na Oscar Assenga ,TANGA.

CHUO cha Mabaharia Dar es Salaam (DMI) kimewataka wadau wa sekta ya usafirishaji wa majini kushirikiana katika utafiti, mafunzo na ushauri elekezi ili kuandaa wataalamu wenye weledi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa na Makamu Mkuu wa DMI anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Wilfred Kileo, wakati akielezea ushiriki wa chuo hicho katika maadhimisho yaliyofanyika mkoani Tanga.

Profesa Kileo alisema DMI imeshiriki katika maadhimisho hayo kutokana na uhusiano wa moja kwa moja uliopo kati ya shughuli za chuo hicho na sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji.

Alisema chuo hicho kinahusika na utoaji wa elimu na mafunzo ya ubaharia, utafiti pamoja na ushauri elekezi katika masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo.

“Tupo hapa kuwaunga mkono na kuwahamasisha watu wanaohusika na vyombo vya usafirishaji majini, pamoja na watafiti katika masuala ya baharini, kushirikiana nasi ili kujenga Taifa lenye wataalamu wenye weledi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira,” alisema.

Alisema ushiriki wao pia ni sehemu ya kuunga mkono kauli mbiu ya kuhamisha sera kwenda kwenye utekelezaji, huku akiishukuru Serikali kwa kuandaa maadhimisho hayo mkoani Tanga.

Profesa Kileo alisema maadhimisho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuufanya umma wa Tanga kufahamu zaidi shughuli zinazofanywa na DMI, hususan katika kuandaa wataalamu wa sekta ya majini.

UBAHARIA SI KAZI YA KUZAMIA

Aidha, Profesa Kileo alisema bado kuna mtazamo finyu kwa baadhi ya wananchi kuhusu taaluma ya ubaharia, jambo ambalo linahitaji kubadilishwa kupitia elimu na uhamasishaji.

Alisema zamani kulikuwa na dhana kwamba ubaharia ni kazi inayohusisha zaidi watu wanaozamia majini, lakini ukweli ni kwamba taaluma hiyo inahitaji elimu na mafunzo ya kitaalamu yenye viwango.

“Baharia ni mtaalamu aliyeiva katika taaluma na ana viwango vyake vya elimu na mafunzo. Hii ni taaluma ya kiwango cha juu inayohitaji maandalizi maalumu,” alisema.

Alisema DMI imekuwa ikifanya kampeni mbalimbali katika shule kwa lengo la kuwahamasisha wanafunzi kupenda na kujiunga na masomo yanayohusiana na ubaharia.

Kwa mujibu wa Profesa Kileo, kampeni hizo zinalenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji wa majini na kuwaandaa mapema kwa masomo yatakayowawezesha kufikia taaluma hiyo.

BILIONI 10 VYA VIFAA VYA MAFUNZO

Katika hatua nyingine, Profesa Kileo alisema maandalizi ya wataalamu wenye ushindani yanahitaji uwepo wa vifaa maalumu vya kujifunzia na kufanya mafunzo kwa vitendo.

Alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika vifaa vya mafunzo, ambapo DMI imepata uwekezaji wa karibu Sh bilioni 10 kwa ajili ya vifaa vitakavyowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

Alisema vifaa hivyo ni muhimu kwa sababu vinawapa wanafunzi nafasi ya kufanya mazoezi yanayofanana na mazingira halisi watakayokutana nayo wanapokwenda kufanya kazi baharini.

“Tunapoandaa wataalamu wenye ushindani, elimu hiyo inahitaji ushirikiano pamoja na vifaa maalumu vya kufanya mafunzo kwa vitendo. Vifaa hivi vinawawezesha wanafunzi kufanya vitu halisi ambavyo watakwenda kukutana navyo baharini,” alisema.






MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa utoaji wa huduma za matibabu ya saratani kwa wanachama wa NHIF, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hizo za kibingwa nchini.

Makubaliano hayo yamesainiwa katika hafla iliyofanyika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene C. Isaka, kwa niaba ya Mfuko huo, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Zeenat Sulaiman, aliyesaini kwa niaba ya Taasisi ya Aga Khan.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Dkt. Isaka amesema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za NHIF za kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wanachama wake, hususan huduma za kibingwa zinazohitaji utaalamu na teknolojia maalumu.

Dkt.Isaka,amesema NHIF inaendelea kupanua wigo na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanachama wake, sambamba na kuongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma hizo kupitia mtandao wa watoa huduma wa Mfuko.

“NHIF inaendelea kuboresha wigo na ubora wa huduma zinazopatikana kwa wanachama wake na kuongeza wigo wa vituo vinavyotoa huduma hizo. Kusainiwa kwa makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya saratani kupitia mtandao wa watoa huduma wa Mfuko,” amesema Dkt. Isaka.

Ameongeza kuwa makubaliano hayo yanaendeleza historia ya ushirikiano baina ya taasisi hizo mbili na yamekuja wakati ambao Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa usawa na kwa wakati.

NHIF imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ushirikiano na watoa huduma mbalimbali wa afya nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wanachama wake, kuboresha ubora wa huduma na kuhakikisha matibabu yanatolewa kwa ufanisi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki,Dkt. Zeenat Sulaiman amesema Hospitali ya Aga Khan inathamini ushirikiano huo na NHIF, akieleza kuwa makubaliano hayo yanaimarisha dhamira ya taasisi hizo mbili ya kushirikiana katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

“Ushirikiano huu unaonesha umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kushirikiana katika kuimarisha huduma za afya. Tutaendelea kutumia utaalamu, teknolojia na uzoefu wetu katika kutoa huduma za saratani kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu,” amesema Dkt. Sulaiman.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, wanachama wa NHIF watanufaika na huduma za matibabu ya saratani kwa wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam,Mwamza na kliniki 14 ikiwemo huduma za tiba kwa mionzi na tiba kwa kemikali.

Aidha, wanachama wa NHIF watapata fursa ya kuhudhuria kliniki za matibabu ya saratani katika hospitali hiyo na kupata huduma hizo kwa kuzingatia taratibu, masharti na miongozo ya Mfuko.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza wigo wa vituo vinavyotoa huduma za matibabu ya saratani kwa wanachama wa NHIF, huku ikiwapa fursa ya kupata huduma za kibingwa kutoka kwa wataalamu wenye uzoefu na kutumia teknolojia zinazohitajika katika matibabu ya ugonjwa huo.
Na Mwandishi wetu, Geita


MAMLAKA ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) imeshiriki maonyesho ya kitaifa ya tisa ya teknolojia ya madini yanayofanyika mjini Geita kwa kuitaka jamii kujiunga na VETA ili kupata ujuzi.

Mkufunzi wa bidhaa za ngozi kutoka chuo cha VETA Dakawa Morogoro, Hamidu Shabani akizungumza na waandishi wa habari ameiasa jamii kujiunga na VETA ili wapate ujuzi.

Hamidu amesema VETA inazidi kupiga hatua kubwa kwani wameongeza kampuni ya Ujuzi ICL kampuni tanzu inayomilikiwa na VETA.

"VETA hivi sasa wanafunzi wanajifunza utengenezaji na uuzaji wa bidhaa za ngozi, mfano viatu, mikanda na mikoba," amesema Hamidu.

Amesema uuzaji wa bidhaa zote zinazotengenezwa na wabunifu kutoka vyuo vya VETA nchini kupitia duka linaloitwa 'Ujuzi Shop' lililopo kwenye maonyesho hayo na viwanja vya VETA Dodoma makao makuu.

Amewakaribisha wananchi wa Geita na washiriki wa maonyesho hayo kufika kwenye banda la VETA na kuuliza maswali na kupata maelezo ya kina juu ya uelewa kuhusu VETA.

Mmoja kati ya wakazi wa Manispaa ya Geita, Elias Makelemo amesema amefika banda la VETA na kuvutiwa na namna utengenezaji wa bidhaa za ngozi ulivyo.

Makelemo amesema bidhaa za VETA za ngozi ikiwemo viatu, mikoba na mikanda ni imara iliyotengenezwa kwa ustadi mkubwa mithili ya bidhaa kutoka bara la Ulaya kumbe imetengenezwa na VETA.


NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dennis Londo amewataka wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam kutumia fursa ya uwepo wa tamasha la Kariakoo Festival kukuza biashara, uwekezaji na kutumia fursa ya masoko ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kukuza masoko ya bidhaa zao.

Mhe Londo ameyasema hayo leo Septemba 25, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizindua rasmi tamashahilo kwa msimu wa tatu na kuongeza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa wa takribani asilimia 70 kufanikisha Dira ya Nchi kwa Mwaka 2050 kwenye eneo la uunganishaji wa biashara na ongezeko la mnyororo wa thamani.

Mhe Londo amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Soko la Kariakoo kwani linachangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa nchi, soko la ajira na mzunguko wa fedha na injini ya biashara.

Akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo ya Masoko ya Kariakoo Bw.Jossam Mzava amesema umoja wa wafanyabiashara wa soko hilo umeweza kuwaunganisha wadau wote kwenye sekta ya biashara ndani na nje ya nchi kwa maslahi mapana ya kukuza mapato hapa nchini.

Tamasha hilo lililobeba kaulimbiu ya; 'Bei shwaa shwaaa' ikimaanisha bei imepunguzwa linawakutanisha wafanyabiashara mbalimbali kwa lengo la kujadili fursa mbalimbali na namna wanavyoweza kutumia masoko ya ndani na nje.

Katika hatua nyingine, Mhe Londo ameziagiza taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuanza kushiriki tamasha hilo ili kutoa fursa kwa wafanyabiashara kupata huduma na elimu juu ya upatikanaji wa leseni, ushindani wa kibiashara na nembo za ubora.








TABORA, Tanzania 

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Ndg. Rabia Abdalla Hamid, amesema Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 ni jumuishi na inalenga kutekeleza mahitaji na matarajio ya makundi yote ya kijamii nchini.

Rabia amesema hayo leo, Septemba 25, 2026, wakati akiendelea na ziara ya CCM katika Mkoa wa Tabora yenye lengo la kusikiliza, kuzungumza na wananchi pamoja na kutafuta majawabu ya changamoto zinazowakabili.

Katika ziara hiyo, Rabia amekutana na wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ambao walipata fursa ya kuwasilisha changamoto zao na kutoa maoni kuhusu masuala yanayogusa maisha yao na maendeleo ya maeneo yao.

Amesema CCM imeweka katika Ilani yake ya 2025–2030 mipango inayolenga kuhakikisha makundi yote ya kijamii yanashirikishwa na kunufaika na juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo.

“Ilani ya CCM ya 2025–2030 ni jumuishi kwa makundi yote ya kijamii. CCM itatekeleza ahadi zote ilizowaahidi wananchi,” amesema Rabia.

Amesema Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha kwa vitendo dhamira ya kutekeleza ahadi zinazotolewa kwa wananchi, akisisitiza kuwa kila kundi la kijamii lina nafasi na umuhimu katika kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.

Rabia amesihi wananchi kuendelea kutoa maoni na kuwasilisha changamoto zao kupitia viongozi wa CCM na Serikali ili ziweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa mipango na vipaumbele vilivyowekwa.

Amesema CCM itaendelea kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha majawabu yanapatikana kwa lengo la kuboresha maisha yao na kuimarisha maendeleo ya Taifa.