WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupanua elimu ya amali nchini, akisema uwekezaji huo unalenga kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kujitegemea.
“Hii ni hatua kubwa sana, na inalenga kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa na ujuzi,” amesema.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 13, 2026), alipotembelea Shule ya Sekondari ya Amali ya Mkoa wa Njombe, inayojulikana kama Njombe Technical, iliyopo Mlangali, wilayani Ludewa.
Amesema katika kipindi cha miaka minne hadi mitano, Serikali imejenga shule za amali zaidi ya 100. Pia, amesema shule za uhandisi zimefikia 29, mojawapo ikiwa Njombe Technical.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la shule na kusikiliza maelezo ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wa fani ya umeme kuhusu mafunzo yao kwa vitendo.
Amewahakikishia wanafunzi kuwa Serikali itaendelea kukamilisha upatikanaji wa vifaa vya mafunzo na ujenzi uliobaki, baada ya Kiranja Mkuu, Yusufu Masumbuko Malulu, kueleza upungufu wa vifaa, hususan katika fani za umeme na uashi.
“Kwa hatua itakayofuata itakuwa ni ya kuhakikisha vitendea kazi vyote vinapatikana,” amesema Dkt. Mwigulu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.6 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, ambao umefikia asilimia 75.
Shule hiyo ilianza kupokea wanafunzi Januari 2026, ikiwa na wanafunzi 83 na walimu 17. Inatoa mafunzo katika fani sita za umeme wa majumbani, ufundi ujenzi, ufundi bomba, umeme wa jua, ushonaji na uchomeleaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mlangali, akieleza matumaini kuwa sehemu iliyobaki inaweza kukamilika katika bajeti mbili zijazo.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Njombe, Mhandisi Kipembawe Msekwa, amesema kilomita 1.5 kati ya kilomita 4.55 zimekwishajengwa, huku mkandarasi akiwa amepatikana kwa ajili ya kujenga kilomita nyingine 1.3 katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Dkt. Mwigulu pia amepanda mti wa parachichi katika eneo la shule, ambapo jumla ya miti 64 imepandwa kwa ajili ya kuanzisha bustani ya zao hilo.













.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)




