"KILIMO"
Showing posts with label KILIMO. Show all posts
Zaidi ya wananchi 200 wametembelea banda la Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) katika maonesho ya kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani mkoani Tanga, kujifunza aina mbalimbali za mbegu bora, sifa zake na namna ya kuzitumia ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, alipotembelea banda hilo, Afisa Masoko wa ASA, Suzan Ludovick, amesema wananchi wamepata elimu kuhusu aina za mbegu zinazouzwa na taasisi hiyo, ubora wake pamoja na maeneo yanayofaa kwa kilimo chake kulingana na hali ya hewa.

Amesema ASA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbegu zinazoweza kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mbegu ya mahindi aina ya T105, ambayo ina uwezo wa kustahimili mazingira yenye maji mengi, hatua inayoweza kuwasaidia wakulima kupunguza athari za mvua nyingi zinazoweza kujitokeza katika msimu wa kilimo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, amepongeza teknolojia mbalimbali za kilimo zilizooneshwa katika maonesho hayo, akieleza kuwa matumizi ya teknolojia na mbegu bora ni miongoni mwa njia muhimu za kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi, hususan wakulima, kutumia fursa za maonesho hayo kujifunza teknolojia mpya na kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi bora katika shughuli zao za kilimo.






Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inapenda kuwataarifu wadau wote
wanaojihusisha na uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa mbegu zinazomilikiwa na
Taasisi kuwa ni wajibu wao kuhakikisha wanazingatia taratibu za haki miliki, ikiwemo

kusaini mikataba rasmi ya matumizi (Licensing Agreements) na kulipa mirabaha stahiki kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 30 vikisomwa pamoja na Kifungu cha 40 cha Sheria ya Haki Miliki za Ugunduzi wa Mbegu za Mimea (Plant Breeders' RightsAct), pamoja na Kanuni ya 33(b) ya Kanuni za Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania, 2023, TSN. 448 la tarehe 30 Juni 2023.

Kwa mantiki hiyo, TARI inatoa wito kwa wazalishaji, wasambazaji, wauzaji, kampuni, taasisi na mtu yeyote anayejihusisha au anayetarajia kuanza kuzalisha, kusambaza au kuuza mbegu au teknolojia nyingine yoyote inayomilikiwa na TARI, kuwasiliana na

Taasisi ndani ya kipindi cha siku thelathini (30) na kipindi hicho cha siku 30 kikiisha, TARI itachukua hatua za kisheria dhidi ya wadau wote watakaoshindwa kutekeleza wito huu. Lengo la tangazo hili ni kuwataka wadau:

. Kujisajili

i. Kuhakiki na kuhuisha taarifa zao
i. Kusaini mikataba rasmi ya matumizi ya teknolojia na mbegu za TARI; na
İv. Kuweka utaratibu sahihi wa ulipaji wa mirabaha kwa mujibu wa Sheria na Kanuni.
Taarifa hili imetangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Namba.18012 la tarehe 9

Oktoba, 2026.
Taarifa ziwasilishwe kwa anuani ifuatayo:
Mkurugenzi Mkuu,

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),
Na Byera Deus, Bukoba

WATAFITI na wataalamu wa zao la migomba kutoka nchi tisa barani Afrika wamefanya ziara nchini Tanzania kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika utafiti, uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora za migomba.

Ziara hiyo imefanyika katika mikoa ya Arusha na Kagera, ambapo wataalamu hao wametembelea mashamba ya wakulima na kujionea namna wanavyotumia aina mpya za migomba iliyofanyiwa utafiti, ikiwemo FIA na Taribani 1-14, ambazo zimeonesha uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili uzalishaji wa zao hilo, zikiwemo magonjwa, wadudu na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wataalamu hao ni sehemu ya Mtandao wa Utafiti wa Zao la Migomba (BBN) unaowakutanisha watafiti kutoka Tanzania, Comoro, Nigeria, Rwanda, Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya na Ghana.

Mratibu wa Zao la Migomba ambaye pia ni Meneja wa Utafiti wa Mazao na Utunzaji wa Mazao baada ya Mavuno kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Shimwela, amesema mtandao huo ulianza shughuli zake mwaka 2024 kwa lengo la kuimarisha utafiti na upatikanaji wa mbegu bora za migomba zinazoweza kuendana na mazingira mbalimbali na kuwasaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema ziara hiyo imewapa wataalamu fursa ya kufanya vikao vya pamoja, kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuendeleza tafiti zinazolenga kupata aina za migomba zenye tija zaidi kwa wakulima na wazalishaji wa ndizi barani Afrika.

“Tumekuja pamoja kujadili namna ya kuimarisha utafiti wa migomba, lakini pia kuona kwa vitendo namna wakulima walivyopokea aina za migomba zinazofanyiwa utafiti. Kwa mfano, FIA imefanya vizuri, lakini pia Taribani 1-14, jamii ya Matoke kwa Tanzania na Uganda, nazo zimeleta matokeo chanya,” alisema Shimwela.

Alisema kupitia tafiti zinazofanywa na taasisi za utafiti wa kilimo barani Afrika, ikiwemo TARI, jitihada zinaendelea za kupata na kusambaza aina za migomba zinazoweza kutoa uzalishaji unaoendana na mazingira ya mkulima pamoja na changamoto zinazoukabili uzalishaji wa zao hilo.

Aliongeza kuwa nchi zinazoshiriki katika mtandao huo zimeahidi kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko ya uzalishaji wa migomba, hususan matumizi ya aina mpya zilizofanyiwa utafiti.

Mbali na vikao vya wataalamu, timu hiyo imetembelea mashamba ya wakulima katika maeneo mbalimbali na kuzungumza nao kuhusu uzoefu wao baada ya kuanza kutumia aina za migomba iliyofanyiwa utafiti.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, hatua hiyo ni muhimu katika kupata mrejesho kutoka kwa wakulima ambao ndio watumiaji wakuu wa teknolojia na aina mpya za migomba zinazozalishwa kupitia tafiti.

Miongoni mwa wakulima hao ni Nasoro Mpendekaki, mkulima kutoka Kemondo, Halmashauri ya Bukoba, ambaye alieleza namna alivyopokea mbegu mpya aina ya FIA na changamoto alizokutana nazo katika kuachana na migomba ya asili ambayo ilikuwa imeanza kupungua uzalishaji na kushambuliwa na ugonjwa wa Mnyauko.

Mpendekaki alisema haikuwa rahisi mwanzoni, hasa kutokana na mtazamo wa jamii iliyomzunguka, lakini kwa sasa amepata matokeo mazuri kutokana na matumizi ya migomba iliyofanyiwa utafiti.

Alisema kwa sasa huuza kati ya mikungu 100 hadi 120 kwa mwezi, huku bei ya mkungu mmoja ikiwa kati ya Sh15,000 na Sh20,000.

Amesema mapato hayo yamemsaidia kupata mahitaji ya chakula na kuboresha maisha yake, huku pia akirithisha uzoefu huo kwa watoto wake ambao, kwa sasa, wameanza kuwa na mashamba ya migomba.

Mpendekaki aliongeza kuwa ameweza kufungua tawi la mauzo katika Mkoa wa Tabora, hatua ambayo amesema imeongeza kwa kiasi kikubwa kipato chake kutokana na biashara ya ndizi.

Kwa upande wao, wajumbe kutoka nchi nyingine, akiwemo Dorcas Ibitoye kutoka Nigeria, Jean Prosper kutoka Comoro na Michael Batee kutoka Uganda, wamesema ziara hiyo imewakutanisha watafiti kutoka nchi tisa zinazozalisha ndizi barani Afrika.

Wamesema jambo kubwa lililokubaliwa ni namna ya kuhakikisha matokeo ya tafiti yanaondoka maabara na kuwafikia wakulima moja kwa moja.

Wamesema watafiti hao kwa pamoja wanataka kuona aina za migomba zinazofanyiwa utafiti zikifanya kazi katika mazingira halisi ya wakulima, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji na kipato kwa wazalishaji wa ndizi barani Afrika.











Na Mwandishi Wetu, Masasi

Msimu wa Korosho 2026/2027 umezinduliwa rasmi wilayani Masasi, huku viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wakitakiwa kuwa waadilifu na kutohujumu zao hilo, kwa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya hivyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Emmanuel Shilatu, amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayehujumu zao la korosho au kufanya vitendo vinavyoweza kuwarudisha nyuma wakulima.

Shilatu ameyasema hayo katika kikao cha uzinduzi wa msimu wa Korosho 2026/2027 kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa zao hilo.

Amesema wakulima wa korosho wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuhakikisha zao hilo linapewa heshima na kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.


“Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayefanya mzaha au kujaribu kuhujumu kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia kwa kutaka kulihujumu zao la korosho kwa namna yoyote ile. Hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, ikiwemo adhabu ya kifungo,” amesema Shilatu.

Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza, amewataka makarani wanaohusika katika shughuli za ununuzi wa korosho kuhakikisha wanatumia mizani ya kidijitali, kuzingatia ubora wa zao na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Naye Kiongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Biadia Matipa, amesema chama hicho kimejipanga kikamilifu kuhakikisha msimu wa Korosho 2026/2027 unakwenda vizuri.

Matipa amesema maandalizi yote yamekamilika na ameahidi kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha malipo yanafanyika ndani ya siku saba tangu kufanyika kwa mnada.

Kwa upande wao, viongozi wa AMCOS wameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi ili msimu wa Korosho 2026/2027 uwe na tija kwa wakulima na wadau wote wa zao hilo.




 

WAZIRI wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amefanya mkutano na Wadau wa Tasnia ya Tumbaku mkoani Tabora tarehe 3 Oktoba 2026 kutatuai changamoto za tasnia hiyo kuanzia ya bei ya pembejeo, masoko, teknolojia duni ya ukaushaji pamoja na madeni ya AMCOS na halmashauri ambayo hayajalipwa kwa wakati.

Kikao hicho kimewahusisha wakulima; Vyama vya Msingi (AMCOS); wanunuzi pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania; ambapo Mhe. Chongolo amezitaka kampuni zinazodaiwa fedha za wakulima kuhakikisha malipo yote yamekamilika ifikapo tarehe 30 Oktoba 2026, akisisitiza  kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha malipo baada ya wakulima kuuza Tumbaku.

Kuhusu bei ya pembejeo, Mhe. Chongolo amesema Serikali imechelewesha kutangaza bei kwa makusudi ili kutafuta unafuu kwa wakulima.  Ameelekeza kufanyika mazungumzo ya wadau ndani ya siku kumi (10) ili kupata bei nafuu zaidi, huku akisisitiza kuwa mbolea lazima isambazwe kwa wakulima ndani ya wiki mbili.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Dkt. Gerald Mongella, amesema kuwa uchumi wa mkoa huo unategemea zao la Tumbaku huku akisisiriza Serikali kuongeza kiwango cha ruzuku kwa wakulima wa Tumbaku na kuharakisha mchakato wa kuanzishwa kwa kiwanda cha mbolea mkoani Tabora unafanikishwa ili kukabiliana na changamoto hiyo. 

Nae Meneja wa Bodi ya Tumbaku Kanda ya Tabora, Bw. Albert Charles amesema kuwa licha ya changamoto zilizopo, idadi ya wanunuzi imeongezeka kutoka kampuni tatu msimu wa 2020/2021 hadi kufikia kampuni 18 kwa sasa, hatua inayotoa matumaini kwa wakulima.








WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amewataka watumishi wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kufanya kazi yenye tija inayoonekana, maarifa na ubunifu ili kuleta matokeo kwa wananchi.

Amesema akiwa katika ziara ya kikazi kukagua shughuli za uzalishaji wa mbegu katika Shamba la Mbegu la Kilimi linalosimamiwa na Wakala wa Mbegu za Kilimi (ASA) tarehe 2 Oktoba 2026, mkoani Tabora.

“Niwaombe tujielekeze kwenye matokeo, tutafute matokeo kwa kutengeneza jambo kwa tija. Kila mmoja ataliona na watu watasema jambo hili limefanyika,” amesema, akisisitiza kuwa mafanikio ya uzalishaji wa tani mbalimbali katika shamba hilo si jambo dogo bali ni matokeo ya kazi iliyofanyika.

Shamba la Mbegu la Kilimi ni miongoni mwa mashamba yanayomilikiwa na ASA yenye jukumu la kuweka msukumo wa uzalishaji wa mbegu nchini ili kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.

Aidha, Mhe. Chongolo ameielekeza ASA kuongeza uwekezaji wa miundombinu ya umwagiliaji, ili kuhakikisha msimu ujao uzalishaji unaongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa ASA, Mhandisi Innocent Masaka, amesema shughuli za uzalishaji katika Shamba la Mbegu la Kilimi kwa sasa zinafanyika kwa misimu miwili kwa mwaka kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika miundombinu ya umwagiliaji, ambapo eneo lenye ukubwa wa ekari 1,000 limewekewa miundombinu hiyo.

Amesema katika msimu wa masika, shamba lilizalisha mbegu za Mahindi katika hekta 142 na Alizeti katika hekta 119, ambapo tani 231.900 za Mahindi na tani 40.300 za Alizeti tayari zimesafirishwa kwenda Makao Makuu ya ASA Morogoro kwa ajili ya uchakataji, huku kilo 8,800 za mbegu za Alizeti zikiwa bado shambani zikisubiri kusafirishwa.

Kwa msimu wa kiangazi, shamba limezalisha mbegu za Maharage aina ya Uyole Njano katika eneo la hekta 40, ambapo zao hilo liko katika hatua ya kukomaa na linatarajiwa kutoa tani 40 za mbegu.

Mhandisi Masaka amesema kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027, Shamba la Kilimi linatarajia kupanda hekta 145 za Mahindi na hekta 155 za Alizeti, kwa matarajio ya kuvuna tani 363 za Mahindi na tani 155 za Alizeti.











ONGEZEKO la mradi wa umwagiliaji Idudumo III  uliopo Nzega, mkoani Tabora kutoka hekta 173 hadi kufikia hekta 1,500 umepongezwa kwa kulenga kuchochea kasi ya uzalishaji wa mazao na kuleta tija ya kiuchumi kwa wakulima. 

Hayo yamesemwa tarehe 2 Oktoba 3026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika (Mb) wakati wa ziara ya kikazi mkoani humo.  Ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NiRC) chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa kwa kuhakikisha mradi huo unasimamiwa kwa  thamani halisi ya fedha  ambapo wanufaika ni wananchi wa Nzega, mkoani Tabora.

“Miradi hii inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi na kutoa fursa kubwa za kiuchumi. Ni muhimu wananchi watambue kuwa miundombinu hii ni ya kwao na wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuitunza na kuchangia huduma kwa mujibu wa sheria ili iweze kudumu na kuleta tija iliyokusudiwa,” amesema Mhe. Mwanyika.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema kuwa kilimo cha umwagiliaji ni azma ya Serikali ya kuimarisha usalama wa chakula kwa kuleta mapinduzi katika Sekta ya Kilimo kupitia umwagiliaji, akibainisha kuwa uwekezaji huo unalenga kumkomboa mkulima mdogo na kukuza uzalishaji wenye tija.








Wanachama waliohitimu pamoja na familia zao kwenye mahafali ya Awamu ya Pili, Mapigano, Ulyankulu, tarehe 21 Agosti 2026.

Mradi wa DREAMS Tanzania ulianza ukiwa na lengo la kuthibitisha kwamba kaya maskini zaidi zinaweza kujenga biashara zinazodumu. Ndani ya siku nne za mwezi Agosti, kaya 1,356 zilizohitimu zilitoa ushahidi.


ULYANKULU, MKOA WA TABORA, TANZANIA · AGOSTI 2026.

Mwezi Februari 2025, maafisa wa mradi walipita nyumba kwa nyumba katika vijiji vinne vya eneo hili la mkoa wa Tabora. Walikuta kwamba asilimia 14 tu ya kaya maskini zaidi zilikuwa zinaishi kwa zaidi ya dola tatu kwa siku. Baada ya miezi 12 ya utelekelezaji wa mradi, idadi hiyo ilikuwa imefika asilimia 82.75.

Mahafali mawili yaliyotenganishwa na siku tatu yalionesha mabadiliko hayo. Chini ya hema pale Mapigano siku ya Ijumaa tarehe 21 Agosti, kaya 762 kutoka Mbeta, Mapigano na Taba zilipokea vyeti vyao kutoka kwa Jumanne Singani, mkuu wa makazi ya Ulyankulu. Pale Sasu siku ya Jumatatu tarehe 24 Agosti, kaya nyingine 594 zilipokea vyao, huku Mkuu wa Wilaya ya Kaliua akiwa mgeni rasmi. Viongozi wa vikundi walipanda mmoja mmoja kupeana mikono mezani kuu, kuchukua cheti na kusimama kwa ajili ya picha. Kwaya ziliimba, vikundi vya biashara vilitandika mazao, kuku na mchele uliokobolewa, na kila mradi ulipotajwa umati ulijibu jambo lilelile: ongeza kipato cha familia.

Jumanne Singani, mkuu wa makazi ya Ulyankulu na mgeni rasmi, akizungumza na wahitimu kutoka meza kuu pale Mapigano.

Kwa pamoja kaya hizo 1,356 ndio Awamu ya Pili, na zote ziliingia kwenye mradi zikiwa miongoni mwa kaya maskini zaidi ndani ya makazi. Mradi huu unaitwa DREAMS Tanzania, na upo ili kujibu swali ambalo mashirika ya maendeleo yameshughilika nalo kwa miongo mingi: je, familia zilizo kwenye umaskini uliokithiri zinaweza kuingizwa kwenye uchumi wa kudumu, au msaada huishia kupotea tu mara mradi unapoondoka?

DREAMS, au Delivering Resilient Enterprises and Market Systems, unaongozwa na Mercy Corps kwa kushirikiana na Village Enterprise, Caritas Tabora na shirika la msaada wa kisheria la Dignity Kwanza. Utaendelea hadi Desemba 2027, unalenga kujenga uwezo wa kujitegemea kwa watu 150,000 katika makazi ya Ulyankulu, Mishamo na Katumba pamoja na vijiji vinavyozunguka hayo makazi, ambako Watanzania waliopewa uraia na vijiji vinavyowazunguka wanaishi bega kwa bega. Hadi sasa umewafikia watu 140,414.

JINSI MRADI UNAVYOFANYA KAZI

Mbinu yenyewe ni ya polepole kwa makusudi. Hakuna anayekabidhiwa pesa siku ya kwanza. Maafisa hupita kwanza kila kaya katika kijiji kilichochaguliwa wakiwa na dodoso la kupima hali ya umaskini, Poverty Probability Index (PPI), na majibu ndiyo yanayoamua nani anastahili. "Hatukai chini ya mti na mwenyekiti tukamuuliza nani maskini hapa," anasema January Julius Nyanda, anayesimamia timu za uwandani kwa upande wa Caritas Tabora. "Angetutajia majina ya ndugu zake wote."

Katika Awamu ya Pili, kaya 1,670 zilikidhi vigezo na kaya 1,356 zikajiunga. Zilipitia mada tisa za mafunzo kuhusu uendeshaji wa vikundi, elimu ya fedha na ujasiriamali, kisha zikaunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana vya wanachama thelathini hadi arobaini na tano, pamoja na vikundi vya biashara vya kaya tatu tatu. Ndipo pesa ilipofika: shilingi 533,820 kwa kila kikundi, na mgao wa pili wa shilingi 228,720 baada ya miezi sita, jumla ya shilingi milioni 344.4 katika biashara 452.

Kikundi cha biashara kikionesha bidhaa zake kwenye mahafali: miche ya sabuni, sahani zilizopangwa, nyanya na kabichi.

Fredrick Kumbule Modestus, aliyewashauri takribani washiriki 150, anakumbuka waziwazi walipoanzia. "Mtu alikuwa anapata shilingi elfu kumi bila kuwa na wazo kwamba angeweza kutumia elfu saba na kubakiza elfu tatu," anasema. "Wazo la biashara halikuwepo kabisa."

Si kila mtu alijiunga mwanzoni. Zilienea tetesi kwamba mtaji ungerudishwa baadaye, kwa ardhi au kwa mifugo, na baadhi walikaa pembeni mpaka walipoona vikundi vya kwanza vikinufaika.

MWAKA MMOJA UMEZAA NINI

Utafiti wa mwisho, uliofanywa na Caritas Tabora awamu ilipomalizika, ulionesha wastani wa mali za kaya umepanda kutoka dola 260 hadi dola 955, na matumizi kwa kila mtu kutoka dola 164 hadi dola 453. Kaya zinazoweka akiba mara kwa mara zilipanda kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 99.7, na asilimia 91.8 ya biashara zilipimwa kuwa zenye afya wakati wa kuhitimu.

John Brighton Mwangolela ni mkulima wa kitongoji cha Itagwa, kilichoko Sasu. Kwenye mahafali ya Jumatatu alizungumzia mafanikio waliyopata katika kikundi chao;

"Tulianza na mbuzi wanne. Mwisho wa mwaka tukawa na mbuzi kumi na sita. Tukagawana mbuzi mmoja mwenye mimba kila mmoja, na wale kumi na watatu waliobaki tukawauza tukanunua ng'ombe jike mwenye mimba. Hivi ninavyosimama hapa, ana wiki tangu amezaa, na sasa tunakunywa maziwa yake."
John Brighton Mwangolela
Mhitimu, kitongoji cha Itagwa, Sasu

Antonet Yohana ni mwenyekiti wa kikundi cha kuweka akiba cha Muungano kilichoko Taba, ambacho hununua mpunga, hukikoboa na kuuza mchele kwa kupima. Mwezi aliouchagua ni Januari, wakati ada za shule zinapofika na wazazi walipokuwa wanakopa kwa wenye pesa kwa riba aliyoiita nusu kwa nusu. Sasa kikundi chake kinawakopesha wanachama wake wenyewe kwa riba nafuu.

SHERIA ILIBADILISHA NINI

Pesa huleta matatizo yake yenyewe, na ndiyo maana shirika la msaada wa kisheria lipo ndani ya muungano huu wa mashirika. Ulyankulu ni ardhi tengefu na haiwezi kununuliwa wala kuuzwa ndani ya makazi, hivyo kipato kinapopanda ni lazima kiambatane na uelewa wa mahali ambapo ardhi inaweza kununuliwa kihalali. Masala Johnson, afisa wa masuala ya kisheria wa mradi, pia amewasaidia wanachama kupata vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wanaojiunga na kidato cha tano, na namba za utambulisho wa taifa, ambazo bila hivyo hakuna akaunti ya benki inaweza kufunguliwa.

Timu yake ilifanya kazi kwenye mazingira magumu. "Awali tulipoingia kwenye mradi huu, kulikuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yakiripotiwa ndani ya nyumba, ikiwemo wanaume kutowaruhusu wake zao kuhudhuria mafunzo ya biashara," anasema. "Sasa wapo wanaume wanaotoa ushuhuda kwamba wamewaruhusu wake zao kufanya biashara."

Kwa Mwangolela, masomo ya sheria yalibadilisha namna kijiji chake kinavyozungumzia mabinti.

"Akizaliwa mtoto wa kiume tulisema tumepata mchungaji wa mifugo, na akizaliwa wa kike tulisema tumepata mahari kubwa. DREAMS walitufundisha sheria na wakatufundisha madhara yake. Nenda Itagwa sasa. Shule yetu imejaa watoto kwa sababu ya DREAMS."
John Brighton Mwangolela

MASOKO YENYE SABABU ZAKE ZA KUBAKI

Kinachotofautisha DREAMS na mradi wa kugawa ruzuku ni kinachotokea pale biashara zinapokuwa zimeshaanza. CRDB Bank Foundation ilihamisha pesa kutoka kwenye masanduku na kuiingiza kwenye akaunti takribani 708 katika eneo la Ulyankulu pekee, KickStart International inasambaza pampu za umwagiliaji, SimuSolar inatoa mashine za kusaga na za umwagiliaji zinazotumia nishati ya jua kwa mkopo usio na riba, na AKM Glitters inatoa vifaranga vya siku moja. Mgarang'ombe Traders, wanaokoboa mpunga, walijiunga ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mpunga, nao wakapata kitu.

"Mimi ni mfanyabiashara wa muda mrefu, lakini nilikuwa sina elimu ya biashara. DREAMS walitufundisha, na wakatuomba tuwafikishie wakulima tunaowanunulia mazao. Sasa wanazalisha mchele bora kabisa wa grade A na grade B."
Peter Maganga Mapembe
Wakala, Mgarang'ombe Traders, kata ya Makingi

Kwa mradi mzima, kila dola moja ambayo DREAMS inawekeza imeambatana na dola 4.83 za mtaji wa sekta binafsi.

Kikundi bora cha kuweka akiba katika kila kijiji kilipewa viti hamsini vya plastiki badala ya pesa taslimu, kwa sababu katika vijiji, kila harusi na kila msiba unahitaji viti, viti vinaweza kukodishwa.

KINACHODUMU

Hata zawadi zilibeba mantiki ya mradi. Ili kikundi kistahili kupata viti, kila mwanachama alipaswa kuwa ameweka akiba isiyopungua shilingi 250,000 katika mzunguko wa wiki 52. Pale Sasu zawadi ilikwenda kwa kikundi cha Maboresho, kilichokuwa kimeweka shilingi 12,882,000.

Vyeti vina uzito zaidi. DREAMS hufanya kazi kupitia viongozi wa wilaya badala ya kuwazunguka, na pale Sasu Mkuu wa Wilaya ya Kaliua aliwaambia wahitimu kwamba halmashauri hutenga asilimia kumi ya mapato yake kwa ajili ya mikopo ya vikundi, akiwaagiza watumishi wake kuvipa kipaumbele vikundi vyenye vyeti vya DREAMS. "Cheti hicho kimesajiliwa na halmashauri na kinatambulika nayo," Martin Mgallah, meneja msaidizi wa mradi, aliwaambia. "Wenyeviti, kitunzeni. Ndiyo uhai wa kikundi chenu."

Martin Mgallah, meneja msaidizi wa mradi wa DREAMS Tanzania.

Sehemu nyingine za mpangilio wa mradi zinaelekea upande huohuo. Vikundi vya kuweka akiba vinamilikiwa na wanachama wenyewe na havihitaji pesa kutoka nje ili viendelee kufanya kazi, kila biashara ni mali ya kaya tatu badala ya kaya moja, na maafisa wa wilaya wanashikilia kumbukumbu za kila kikundi.

Awamu ya Kwanza ndiyo mtihani halisi wa kwanza. "Tuliwaaga mwaka mmoja uliopita," alisema Mgallah. "Tumetembelea biashara zao jana. Bado wanafanya biashara na wanaendelea kufanikiwa." Mmoja wao ni Abraham Mgaywa wa Makingi, aliyekuwa na familia kubwa na hakuwa na kipato cha kukidhi mahitaji yake wakati dodoso lilipomfikia. Sasa anajiita Mabala the Farmer, na mwezi huu amesafirisha maroli mawili ya matikiti kwenda Dodoma wakati bei ilipokuwa juu kabisa.

Awamu nyingine nne zinaendelea na mafunzo nyuma ya Awamu ya Pili, jumla ya kaya 5,245, na mwakani maafisa watakuwa milangoni Mkindo, Makonge, Kaswa, Usigara, Keza na Ikonongo. Obed Method Bujoro, mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mapigano, anataka warudi kijijini kwake. Ameona jambo ambalo hakuna utafiti ungeliweza kuligundua: watoto wa kaya zenye shida walikuwa wakitokea milangoni kwa majirani wakati wa chakula, na hilo limekoma.

Wahitimu na watumishi wa DREAMS wakicheza mwishoni mwa mahafali.

Anastazia Paulo Makula alisoma risala ya wahitimu pale Sasu. Alijiunga bila mtaji wowote, akajiwekea lengo la kuweka akiba kwa muda wa miezi mitatu, na kwa pesa iliyopatikana akafungua duka la nguo za watoto. Muhtasari wake ndio uliokuwa mfupi kuliko yote siku hiyo.

"Tulikuwa na maisha ya chini sana. Leo nina imani sisi wana Sasu tuko vizuri."
Anastazia Paulo Makula
Kikundi cha kuweka akiba cha Maboresho, Sasu Centre

Mradi wa DREAMS Tanzania unatekelezwa na Mercy Corps kwa kushirikiana na Village Enterprise, Caritas Tabora na Dignity Kwanza, pamoja na wadau wa sekta binafsi wakiwemo CRDB Bank Foundation, Mgarang'ombe Traders, AKM Glitters, SimuSolar na KickStart International.