Na.Mwandishi Wetu-ADDIS ABABA, ETHIOPIA

Wadau wa maendeleo ya sekta ya afya wameonesha utayari wa kuunga mkono ajenda ya sifuri tatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Mama na Mtoto Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana barani Afrika,

Utayari huo umetangazwa na Viongozi na wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Maendeleo kwenye Mkutano wa Ngazi ya Juu uliolenga kujadili kuhusu utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Watoto na Vijana (RMNCAH) 2026–2030, uliofanyika Novemba 24, 2026, jijini Addis Ababa, Ethiopia, siku moja baada ya Rais Dkt. Samia kuzindua rasmi Mpango Elekezi huo katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Afrika (CPHIA 2026).

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema hatua inayofuata ni kuhakikisha dhamira ya kisiasa iliyowekwa kupitia mpango elekezi huo inatafsiriwa kuwa uwekezaji, maamuzi na utekelezaji wenye matokeo katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.

“Sekretarieti itaendeleza ushawishi kwa viongozi wa Afrika, kuratibu mikutano ya kitaalamu, kuhamasisha rasilimali za kifedha na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ili kuhakikisha nchi zinatimiza ahadi zilizowekwa,” amesema Mhe. Ummy Mwalimu.

Wakizungumza mara baada ya wasilisho la kitaalamu kuhusu Mpango Elekezi huo, wawakilishi wa taasisi na mashirika mbalimbali ya maendeleo, akiwemo Dkt. Shamma Khalifa Al Mazrouei, Mkurugenzi Mkuu wa Mohammed Bin Zayed Foundation for Humanity, Bw, Samwel Mulyanga Afisa Programu Mwandamizi wa Gates Foundation, Dkt. Sennen Hounton – Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Kanda ya Afrika Magharibi na Kati; Bi. Patricia Wamala, Afisa Programu kutoka Begginings Fund, Dkt. Tabinda Sarosh Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Pathfinder; Bi. Karoline Myklebust Mkurugenzi Mtendaji wa Laerdal Global Health; Dkt. Ntuli Kapologwe Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC); Serikali ya Norway, wameonesha utayari wa kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika pamoja na Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto katika kuunga mkono na kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya sifuri tatu ya Rais Samia.


Awali akizungumzia hali ya afya ya mama na mtoto barani Afrika, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), Profesa Diana Nambatya Nsubuga, amesema bara hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya vifo vya mama na watoto, ambapo asilimia 70 ya vifo vya wajawazito duniani hutokea Afrika, huku asilimia 58 ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano pia vikitokea katika bara hilo.

“Takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa afua za afya zenye matokeo makubwa ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma muhimu za chanjo” amesema Prof. Nsubuga.

Mshauri wa Kiufundi wa Sekretarieti ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Dkt. Sunday Dominico, amesema kufikia lengo la Sifuri ya uzazi wa nyumbani tunahitaji vituo vya afya kuwa na watumishi wenye ujuzi, vifaa tiba na uwezo wa kutoa huduma bora, ikiwemo huduma za dharura na rufaa kwa wajawazito na watoto wachanga.

Ameeleza kuwa Sifuri ya vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga tutahitaji uchunguzi wa kina wa vifo vinavyotokea pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya kitaalamu, huku lengo Sifuri ya mtoto anayekosa chanjo likihitaji Serikali na wadau kushirikiana kuimarisha huduma za chanjo na kuwafikia watoto wote.likihitaji Serikali na wadau kushirikiana kuimarisha huduma za chanjo na kuwafikia watoto wote.



Akiwakilisha Tanzania katika mkutano huo, Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Nassoro Mazrui, amesema uzoefu wa Tanzania unaonesha kuwa uongozi madhubuti na uwekezaji endelevu katika sekta ya afya vinaweza kuleta matokeo katika kupunguza vifo vya mama na kuboresha huduma za afya.

Amesema takwimu za tafiti za afya na demografia zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito nchini vilipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2022, huku asilimia 80 ya wanawake wakijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya mwaka 2022.

Ameongeza kuwa matokeo ya awali ya utafiti mpya wa kitaifa yanaonesha kupungua zaidi kwa vifo vya wajawazito nchini, hatua inayokaribia lengo la Malengo ya Maendeleo Endelevu la kufikia chini ya vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.

Kupitia ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Africa CDC, Serikali na wadau wa maendeleo, ajenda ya sifuri tatu inalenga kuunganisha nguvu, uwekezaji na uwajibikaji ili kuhakikisha kila mama anajifungua salama na kila mtoto anapata fursa ya kuishi, kukua na kufikia afya bora.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF), wamesainiana Mkataba wa Haki za Matangazo kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, yatakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

Mkataba huo umesainiwa jijini Dar es Salaam leo Novemba 25, 2026 na Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi. Thereza Mugobi, kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Katibu Mkuu wa CAF Samson Adamu aliyewakilisha shirikisho hilo.

Akizungumza kabla ya utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema hatua hiyo ina manufaa makubwa kwa Sekta ya Utalii na mnyororo mzima wa thamani katika sekta hiyo kwani itachochea ukuaji na maendeleo yake.

“Utiaji saini wa mkataba huu ni faida kwa Sekta ya Utalii na mnyororo wote wa thamani katika sekta hiyo,” amesema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kuhakikisha Tanzania inanufaika na ujio wa michuano hiyo, akieleza kuwa AFCON 2027 ni fursa ya kipekee ya kuitangaza nchi pamoja na vivutio vyake vya utalii ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, amesema hatua hiyo inaweka historia na kuendelea kudhihirisha uzalendo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akitambua na kuendeleza sekta mbalimbali nchini, zikiwemo Sekta ya Utalii na Michezo.

Amesisitiza kuwa uongozi imara wa Rais Samia Suluhu Hassan umechangia kuifungua Tanzania kwa fursa mbalimbali za kimataifa, hivyo anastahili pongezi kwa juhudi hizo.Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda (Mb), amesema kuwa ujio wa michuano ya AFCON 2027 nchini ni fursa muhimu ya kiuchumi, kwani utaleta wageni wengi, kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuongeza kipato kwa wananchi.















NAIBU Waziri wa Fedha, Mhe.  Laurent Deagratius Luswetula (Mb), ameitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), kuendelea kuimarisha hatua za kinidhamu dhidi ya wahasibu na wakaguzi wanaokiuka maadili ya taaluma hiyo ili kudhibiti upotevu wa mapato na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mhe. Luswetula (Mb), alitoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa 39 wa Mwaka wa Wahasibu katika Hoteli ya APC, Bunju, jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Alisema NBAA inapaswa kuchunguza kwa kina tuhuma za ukiukwaji wa maadili na kuchukua hatua zinazolingana na uzito wa makosa yaliyothibitishwa, kwa kuzingatia haki na ushahidi.

Aliwataka wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kufuata sheria na taratibu za taaluma yao ili kuendelea kulinda mali za umma.

‘’Nawahimiza wahasibu kukataa shinikizo la kuficha madeni, kubadilisha tarehe za nyaraka au kuthibitisha kazi ambazo hazijafanyiwa uhakiki, saini ya mkaguzi kwenye taarifa za fedha inapaswa kuungwa mkono na ushahidi wa kutosha’’ alisema Mhe. Luswetula.

Pia aliwataka waajiri na viongozi wa kampuni za ukaguzi kuwapa watumishi wao muda na mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao kwa usahihi, kusikiliza hoja zao na kuhakikisha changamoto za kitaaluma zinapatiwa majibu yanayotegemea ushahidi.

Katika hatua nyingine, aliipongeza NBAA kwa kuanzisha mfumo wa NBAA Verification Number (NBAAVN), unaowezesha uhakiki wa taarifa za fedha zilizokaguliwa. Alihimiza kampuni za ukaguzi kuwasilisha taarifa hizo kwa wakati na kuzitaka benki, taasisi za fedha na mamlaka za umma kutumia mfumo huo kuthibitisha uhalali wa taarifa hizo kabla ya kufanya maamuzi.

Kuhusu matumizi ya teknolojia, alisema uchanganuzi wa takwimu, mifumo ya kidijitali na akili unde vinaweza kuboresha ukaguzi na kubaini miamala isiyo ya kawaida, lakini wahasibu na wakaguzi wanapaswa kuendelea kuwajibika katika kuhakiki ushahidi, kulinda taarifa za siri na kutumia uamuzi wa kitaaluma.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na NBAA kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, ubora wa taarifa za kifedha na maendeleo ya kitaaluma ili kuunga mkono utekelezaji wa Dira 2050.

Alisisitiza kuwa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ni muhimu kutathmini si kiasi cha fedha kilichotumika pekee, bali pia kama mradi umekamilika, mali iliyojengwa inaweza kutunzwa na wananchi wanapata huduma zilizokusudiwa.

Aidha, aliipongeza NBAA kwa kuendesha CPA Sustainability Day Novemba 24, 2026, katika Hospitali ya CCBRT na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, akisema hatua hiyo inaonesha mchango wa taaluma hiyo katika ustawi wa jamii.

Awali akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema imani ya umma ndiyo msingi wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi na inajengwa kupitia ubora wa kazi za wahasibu na wakaguzi.

Kuhusu usimamizi wa fedha za umma CPA Prof. Mzenzi alisema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hauwezi kufanikiwa bila usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma.

‘’Natoa wito kwa maafisa masuuli na wahasibu wa sekta za umma na binafsi kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani, kuandaa taarifa sahihi za fedha kwa wakati na kuchukua hatua zinazostahili kutekeleza mapendekezo ya wakaguzi’’ alisema Prof. Mzenzi.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Shayo Temu, alitoa wito kwa wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini kubadili namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa kutumia maarifa, teknolojia na ubunifu kuleta matokeo yanayopimika katika maendeleo ya uchumi na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

‘’Taaluma ya uhasibu inapaswa kwenda zaidi ya kuandaa taarifa za fedha na badala yake kuwa mshirika muhimu katika mageuzi ya uchumi, kuimarisha utawala bora na kuongeza uwajibikaji katika taasisi’’ alisema Prof. Temu.

Mkutano huo wa siku tatu, unaofanyika Novemba 25 hadi 27, 2026, umebeba kaulimbiu “From Insights to Impacts: Driving Innovation and Sustainability in the Accountancy Profession for Dira 2050” na unajadili ubunifu, teknolojia, uendelevu, ubora wa ukaguzi na usimamizi wa fedha za umma.

Mkutano huo umewakutanisha wahasibu, wakaguzi wa hesabu, wawakilishi wa taasisi za Serikali, sekta binafsi, kampuni za ukaguzi na taasisi za kitaaluma kutoka Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akikabidhiwa tuzo  na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akikabidhi tuzo kwa Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ​NBAA, CPA Pius A. Maneno kwa utendaji wake katika Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu.
Mkurugenzi Mtendaji wa ​NBAA Mtaafu, CPA Pius A. Maneno  akipongezwa mara baada ya kupokea Tuzo ya heshima 
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akikabidhi tuzo kwa CPA Eustace Osler Katagira kwa kutunukiwa Uanachama wa Heshima kama Heshima Maalumu ya Kutambua Mchango wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi. Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu.
Naibu NaibuWaziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ulioandaliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kufanyika katika hoteli ya APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu akizungumza kuhusu mikakati mbalimbali ya kusimamia Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka 2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi akisoma hotuba kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi uliofanyika katika hoteli ya APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa ​NBAA Mtaafu, CPA Pius A. Maneno akitoa salamu katika mkutano mkuu wa 39 wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi.
Baadhi ya wa wahasibu na wakaguzi wa Hesabu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi NaibuWaziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka 2026 wa Wahasibu na Wakaguzi
Picha za pamoja