Na Mwandishi Maalum,
Mikumi, Morogoro
Rais Jakaya Mrisho Kikwete ametaka viongozi nchini kutumia utaratibu za kuuza hisa kwa wananchi moja kwa moja kama njia rahisi ya kupata mitaji ya kuanzisha mabenki ya jamii na wananchi.
Lakini pia amehadharisha kuwa mabenki hayo ya wananchi lazima wasimamiwe na kuendeshwa vizuri, ili wasije kuwa kama miradi ya upatu.
Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo kwa viongozi wakati anapokea taarifa ya Mkoa wa Morogoro alipoanza ziara ya kihistoria kwenye mkoa huo katika Nyumba ya Kufikia Wageni ya Mikumi, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani humo. Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Meja Jenerali (Mstaafu), Saidi Kalembo.
Ziara hiyo ya Mkoa wa Morogoro inakuwa ya kihistoria kwa sababu ni mkoa wa mwisho kati ya mikoa 21 ya Tanzania Bara kutembelewa na kiongozi huyo mkuu nchini katika jitihada zake za kukagua jitihada za maendeleo; kusikiliza matatizo, karaha na kero za wananchi; na kujua furaha na mafanikio yao. Rais bado kutembelea mikoa mitano ya Tanzania Visiwani.
Ziara hiyo pia ni ya kihistoria kwa sababu inamfanya Rais Kikwete kuwa rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea mikoa yote, na wilaya zote 133, na majimbo yote ya uchaguzi, kabla ya kufikisha miaka mitatu ya kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano cha urais. Hakuna Rais amepata kuweka rekodi hiyo. Anabakiza kiporo cha Wilaya ya Namtumbo tu katika Mkoa wa Ruvuma.
Mbali ya ziara hizo za kihistoria, Rais Kikwete pia alifanya ziara katika makao makuu ya mikoa yote ya Tanzania kuwashukuru wananchi kwa kumchangua kuwa Rais baada ya ushindi wake wa kishindo wa asilimia karibu 82, Desemba, 2005.
Hakuna Rais yoyote katika waliomtangulia kwenye madaraka ya kuongoza Tanzania alipata kufanya jambo hilo. Alitanguliwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere; Rais Ali Hassan Mwinyi na Rais Benjamin William Mkapa.
Baada ya kuambiwa kuwa Mkoa wa Morogoro mpaka sasa umekusanya kiasi cha sh milioni 70.7 kati ya sh milioni 500 zinazohitajika kuanzisha Benki ya Wananchi wa Morogoro, Rais amewaelekeza viongozi wa mkoa huo kutafuta nguvu za wananchi katika kuchangia na kununua hisa katika benki hiyo.
“Uzeni hisa kwa wananchi. Wananchi wetu wanazo pesa. Tengenezeni utaratibu mzuri kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar Es Salaam ambalo linaweza kuwasaidieni katika kuandaa nyaraka nzuri za kuweza kuuza hisa kwa wananchi wenu. Kwanza ni kuwawezesha wananchi, lakini pia ni njia rahisi ya kupata mitaji ya kuanzisha mabenki hayo,” amesema Rais Kikwete.
Amesema Rais Kikwete: “Msisikilize maneno ya watu wapuuzi. Haya yanasemwa mengi na yatasemwa mengi, lakini ukweli ni kwamba watu wetu wanazo pesa nyingi za kununua hisa. Angalia taasisi ambako Serikali imeuza hisa ambavyo hisa hizo zimekimbiliwa na wananchi na wakatoa fedha kuliko hata hisa zilizokuwa zinauzwa.”
Ameongeza: “Lakini mabenki haya yasimamiwe vizuri. Kwa sababu kama mnavyosikia duniani, mabenki yasiposimamiwa vizuri yanaweza kuingia katika matatizo kama tunavyosikia katika nchi za wakubwa. Sasa wakubwa hao wanalazimika kuyaokoa mabenki yao kila siku. Kwa sababu wasipofanya hivyo, uchumi mzima utasambaratika.” Amesema kuwa usimamizi wa mabenki ya wananchi ni jukumu ya viongozi na wanahisa. “Tusiyafanye mabenki haya kama miradi ya upatu.”
Rais pia ameutaka uongozi wa Mkoa wa Morogoro kuchukua hatua za kufufua vyama vya ushirika katika mkoa huo, na hasa kile cha Kilimo cha Pamba cha Kilosa (Kicu).
Baada ya kuwa ameuliza kama chama hicho kiko hai ama hoi kwa maana ya uhai, Rais amesema kuwa Serikali inaweza kusaidia kukifufua chama hicho kama wanachama wake watakubaliana na masharti ya Serikali katika kukiokoa chama hicho.
“Kwanza tutataka kujua kama chama chenu kiko hai ama hoi, na baadaye tutataka kujua kama kiko ICU (Chumba cha Wagonjwa Mahututi) ama tayari kimezikwa. Kwa sababu kama kimekufa na arobaini tayari, hatuna la kufanya,” amesema Rais.
Ameongeza: “Kama bado kinaweza kuokolewa, tutasaidia. Lakini masharti yetu magumu. Sijua kama mtayaweza kwa sababu tutawanyang’anya madaraka. Hatuwezi kukifufua chama hicho kwa kushirikiana na wezi ambao wamekifilisi. Tutakifufua na kuwanyang’anya madaraka.”
POLITICALLY CORRECT.
ReplyDeleteTHIS IS NOT NEWS. Hii ni ratiba ya safari zake, tupe BREAKING NEWS - JK leo yumo ofisini mwake IKULU.
ReplyDelete