
Serikali imeombwa kupunguza gharama za usajili wa vyombo vya habari mtandaoni (Online Media) ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kujiajiri.
Ombi hilo limetolewa na Jumamosi Januari 24, 2026 na Mkurugenzi wa BMG Media, George Binagi wakati wa hafla fupi ya kupokea tuzo maalum kutoka YouTube baada ya chombo hicho cha mtandaoni kufikisha wafuasi (Subscribers) laki moja.
Binagi amesema licha ya Serikali kupunguza gharama za usajili wa online media kutoka shilingi milioni moja hadi laki tano, bado watengeneza maudhui mtandaoni wanaomba gharama hizo kupungua hadi laki moja hatua itakayosaidia vijana wengi wakiwemo wahitimu wa vyuo vya uandishi wa habari kujiajiri na kuajiri wenzao.
Pia Binagi amebainisha kuwa kuanzia mwaka huu 2026 watengeneza maudhui mtandaoni wameanza kukatwa asilimia tano ya mapatano wanayopata mtandaoni na kuwasilishwa serikalini wakati huo huo wakilipa kodi jambo ambalo limewaongezea mzigo wa kulipa kodi mara mbili na hivyo kuomba changamoto hiyo kutatuliwa.
Katika hatua nyingine, Binagi amewashukuru wadau, wasomaji na wafuasi (subscribers) wa BMG Media kwa mchango wao uliofanikisha kupata tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kutengeneza maudhui yenye weledi unaokidhi mahitaji yao
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwenyekiti wa MISATAN na MPC, Edwin Soko amesema mitandao ya kijamii kwa sasa ni fursa kwa vijana kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, hivyo amehimiza matumizi sahihi ya mitandao hiyo.
Kuhusu gharama za usajili na kodi mbalimbali, Soko ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, amesema atafikisha suala hilo kwa mamlaka husika kupitia vikao mbalimbali vya wadau wa habari ambavyo vimekuwa vikifanyika kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.





























.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)



.jpeg)
.jpeg)


.jpeg)













