Rais Jakaya Mrisho Kikwete jana ameanza mikutano yake ya kufuatilia utendaji wa Serikali yake kwa kufanya mkutano wa kwanza na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na mashirika yake muhimu.

Mkutano huo wa kwanza uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam, umezungumzia utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam na umehudhuriwa na viongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wale wa Bandari yenyewe ya Dar es Salaam pamoja na maofisa waandamizi wa Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA).

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein; Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Waziri mwenyewe wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa.

Katika mkutano wake wa pili, Rais Kikwete anatarajiwa kukutana baadaye leo jioni na uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), na ule wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Mikutano hiyo ya kwanza ni mwanzo wa mfululizo wa mikutano ambayo Rais Kikwete atafanya na viongozi wa wizara mbali mbali za Serikali yake kutaka kujua utendaji wa wizara hizo, kutathmini utelekezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2005 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa wakati alipotembelea wizara zake mwanzoni mwa uongozi wake mwaka 2006.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na kukubaliwa katika mkutano wa kwanza ni kama ifuatavyo:

(a) Kuitaka Kampuni ya Kupakia na Kupakua Makontena (TICTS) katika Bandari ya Dar es Salaam kutekeleza wajibu wake ipasavyo kwa mujibu wa mkataba wake kwa kuongeza ufanisi na kuboresha kiwango chake cha utendaji kwa lengo la kupunguza mlundikano wa meli katika Bandari ya Dar es Salaam.

(b) Kuchukua hatua nyingine za kupunguza mlundikano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuchukua mfululizo wa hatua ikiwa ni pamoja na:


(i) Kuhakikisha kuwa mizigo inaondolewa haraka kwa kadri inavyowezekana katika Bandari, kwa kutumia taratibu muhimu zilizopo, ikiwa ni pamoja na kontena kupigwa mnada baada ya kuwa zimekaa bandarini kwa siku 21 kwa mujibu wa sheria.

(ii) Ili kutekeleza jambo hilo la kuhakikisha kuwa mizigo inaondolewa Bandari haraka, TPA na TRA zimeagizwa kuhakikisha kuwa zinapiga mnada kiasi cha asilimia 30 ya makontena yaliyokaa zaidi ya siku 21 katika bandari hiyo, kama njia ya haraka ya kupunguza mlundikano wa mizigo katika Bandari hiyo.

(iii) Kuhakikisha kuwa kuanzia sasa kontena zote zinazopakuliwa kwenye meli, zinapelekwa moja kwa moja kwenye Vituo vya Kuhifadhi Kontena Nje ya Bandari (ICD’s) na gharama za zoezi hilo zinakuwa sehemu ya kutoa mizigo katika Bandari hiyo.

(iv) Kuchukua hatua za kupunguza muda wa meli kusubiri pwani ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kuhakikisha kuwa upakiaji na upakuaji mizigo unaharakishwa kwa TICTS kununua vifaa zaidi na pia kuhakikisha kuwa vifaa vya TPA vinatumika.

(v) Kuhakikisha kuwa maarifa yanatafutwa kuondoa magari yaliyoko Bandarini kwa sasa yakisubiri kuchukuliwa na wenyewe, ili kupatikane nafasi zaidi ndani ya eneo la Bandari hiyo kwa shughuli na mizigo mingine. Hili lifanyike kwa kutafuta eneo jingine nje ya Bandari kuhifadhi magari hayo.

(vi) Kuharakisha zoezi zima la kuondoa mizigo Bandarini kwa nyaraka muhimu za kufanikisha jambo hilo kujazwa na kupitishwa haraka iwezekanavyo na TRA.

(vii) Ili kufanikisha uharaka huo, TRA imeagizwa kuhakikisha kuwa sehemu ya kushughulikia nyaraka ya long-room inafanywa kuwa short-room kwa maofisa wa Mamlaka hayo kufanya kazi kwa saa 24, ikiwa ni pamoja na siku za Jumapili.

(viii) Kuongeza ushirikiano wa utendaji miongoni mwa taasisi mbalimbali zinazohusika na kuondoa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, ili kuongeza ufanisi wa Bandari hiyo na kuiwezesha kupambana ipasavyo na ushindani kutoka kwa bandari nyingine katika eneo la Mashariki na Kusini mwa Afrika.

(ix) Kuchukua hatua za kuboresha ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kwa miaka ijayo, hasa baada ya ongezeko kubwa la mizigo litakalokuwa linapitia katika bandari hiyo baada ya Reli ya Kati kufanyiwa matengenezo makubwa ya kupanua geji yake.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Hivi, does it have to be that the president notices these things and acts on them? Wale wanaorun hizo taasisi, mawaziri, makatibu wakuu na wizara zao, etc, wapo wapi jamani?

    Sintashangaa kusikia walioambiwa waongeze "graveyard shifts" na weekend shifts wataanza kugoma wakidai huyu raisi kachanganyikiwa eti kwa vile amesema wafanye kazi 24/7 - listen and watch!

    Tutafika kweli?

    ReplyDelete
  2. Bwana Michuzi maamuzi mengine JK naona kama kachemusha vile!

    Kwa mfano anaposema kuanzia sasa LONG RUUM wafanye kazi masaa 24 na Jumapili, hiyo itamaanisha kuajiri wafanyakazi wapya na/au kuwepo kwa hela ya kuwalipa Ovataim wale watakaokuwa wanafanya kazi kwa masaa ya ziada.

    Mchemsho ni kwamba sasa hivi hiyo Taasisi ndo iko katikati ya utekelezaji wa Bajeti yake iliyopitishwa mwezi Juni 2008, na siku hizi wenyewe wanasema ni AKTIVITI BEZID BAJET, sasa hiyo pesa za hizi activity za ziada zilizoongezeka watazipata wapi wakati kahikuwepo katika PANI.

    All the Best.

    ReplyDelete
  3. Mbona JK hajazungumzia WIZI wa bidhaa, magari na vipuri BANDARINI???? Kwani ule WIZI uliisha????

    Na hilo zoezi la kuhamisha magari kuyapeleka sehemu nyingine, upo uwezekano mkubwa wa magiri mazima-mazima kutoweka.

    Hajazungumzia RUSHWA bandarini kwani zile rushwa ziliisha??? Nakumbuka kuna wakati niliwahi kuombwa rushwa ya Shs. 100,000/= miaka ya 1995-96, hapo Long-room. Wakati nashughulikia kukomboa Toyota Carina, ambayo alitakiwa itoke kwa Exemption.

    Mama mmoja alifanya kuwa rushwa ni kama sehemu ya pato lake halali kabisa. Maana alikuwa anaseme "Toa tu, uweke hapa mezani." bila woga hata aibu.

    JE, HALI HII ILIISHA???? Na kama bado ipo, ni hatua gani zimechukuliwa???

    Mdau,
    Ughaibuni

    ReplyDelete
  4. Hivi kweli Jamani hawa wataalamu wetu wajayaona haya muda wote huo, mpaka waje kukaa na Raisi ndio waazimie kuyatekeleza. Duh kazi kweli, kweli ! Haya masuala kama ucheleweshwaji wa utoaji mizigo bandarini, mizigo kulundikana wamekuwa wimbo wa siku nyiiingi! mpaka hata watoto wadogo wanaweza kuuimba bila hata ya kuelewa una maana gani. Mimi nilidhani hatua kama kutafuta sehemu kubwa zaidi ya kuhifadhia mizigo /magari labda ilishafanyiwa kazi na iko katika hatua fulani karibu na kukamilika, lakini kwa jinsi ilivyoandikwa hapa ina maana ndio wanafikiria sasa kutafuta sehemu kwa ajili ya kazi hiyo. Mambo mengi yaliyoainishwa kwenye taarifa hii sidhani kama yalihitaji kusubiri mkutano na Raisi ili kuyaazimia au kuyatekeleza. Yangetekelezwa mwaka mmoja au miwili nyuma mbona tungekuwa mbali..?!Watendaji wanafanya kazi gani kila siku kuanzia asubuhi mpaka jioni kwa mwaka mzima bila ya kutatua mambo ya msingi kama haya mpaka tumsubiri Raisi ?! Tutafika kweli ??!

    ReplyDelete
  5. Kweli Rais wetu ana kazi. Tanzania ni bora uwe mkulima kuliko kuwa kiongozi. Yaani mpaka Rais apite idara hadi idara! Haya ni mambo ambayo viongozi wa idara, wizara nk inabidi wayaone wao wenyewe na kuyarekebisha. Usinambie bandari, TRA, wizara ya fedha nk walikuwa hawajui kwamba utaratibu wa long room ni karaha tupu? Watu wameupigia kelele lakini wapi......... Mwishowe Rais atawajibika kupita majumbani kwa watu kuwaambia akina mama waweke kiasi gani cha chumvi kwenye mboga! Haya sasa tunasubiri apite kwenye mabenki awambie kutoweka wateja kwenye foleni kwa muda mrefu!

    ReplyDelete
  6. JK pole na kazi. Mimi ushauri wangu ambao anyway hautatiliwa maanani yeyote but wacha niseme tuu ni kwamba Hiyo Mikutano bwana bora uwafuate wewe sio wao kuja Ikulu. Unajua mtu akikufuata wewe anakuja amejikamilisha kwa lolote so Ukiwafuata huko kwenye Makampuni na Mawizarani kwanza ile kitendo tuu cha kusikia wana appointment na Raisi angalau hata hizo Ofisi zitapigwa msasa mana kama ni chafu ama zilikuwa hazirizishi na wana tabia ya kula hela za ukarabati basi wakisikia bosi wao Mkubwa nakuja watatafuta pesa wasafishe mbio sana hiyo tuu itakuwa ahueni kwa watu wa kawaida wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu ya kukosa services muhimu za kiofisi. JK WAIBUKIE MAOFISINI HAO MMOJA BAADA YA MWINGINE........trust me !

    ReplyDelete
  7. Mfumo wetu wa utawala wa "Silos" kwa maana taasisi ya wizara ya miundo mbinu (mfano TPA, RTL) ikiona kuna tatizo la kutatua lakini ili utatue inabidi kuongea na taasisi iliyopo kwenye wizara ya fedha (mfano TRA)... Kawaida jamaa wanaishia hapo... maana kuipata hiyo taasisi ya fedha muongee nayo... lazima upitie kwa waziri na kama mawaziri hawaelewani lazima ipitie kwa Mkuu wa nchi na kama yuko safarini ni mpaka arudi.

    Mbili: Tatizo la kutunza kumbukumbu za maazimio na utekelezaji wake... Mh. Edward Lowassa alishawakalisha hao TRA na TPA... swali mangapi yametekelezwa tangu kipindi hicho? Issue ya Kufanya kazi masaa 24 ilishaongelewa wakati huo...sina hakika kama bado...

    Tatu: Kuhusu TRA nadhani wao wameshafanya angalau machache kuhuru hiyo long rumu... ninavyojua mimi tayari wamesha-link makampuni makubwa na huenda na ma-ajenti kupitia kwenye mtandao wa wa Asycuda++ kwa ajili ya ku-log documents bila kufika kwenye hata hiyo short rumu..

    Nne: Kwa mtizamo wangu... alichofanya mkuu wa nchi ni kazi ya Waziri Mkuu... au angalau yaliyoamuliwa inabidi Waziri Mkuu ayafuatitilie kila siku hadi kuona yanafanyika.

    Tano: Taifa letu lina matatizo makubwa sana, mfumo wa utawala inabidi uangaliwe ili uendane na Science na Technology iliyopo sasa.

    ReplyDelete
  8. Rais fukuza hao wanaokufanya wewe kuwa Waziri wa Miundombinu, katibu Mkuu wake, na mkuu wa bandari, ikiwa ni pamoja na wewe kuwa mkuu wa ukuli bandarini!

    Wengine watajitayarisha kabla ya kunyolewa kukavu!

    ReplyDelete
  9. Hapa sasa mkuu wa nchi amewapatia ulaji wa hali ya juu watu wa TRA na Bandari kwa ujumla. Unaposema macontena yapigwe mnada kwa mujibu wa sheria baada ya siku 21, wakati watu wengi wenye mizigo malengo yao ni kwamba mzigo usilale hata siku moja bandarini, Ila hawa jamaa wa TICTS wanakula dili na TRA kudelay ili wapate storage charges. Inatakiwa storage charges zipigwe marufuku na badala yake ziwe ni gharama za kutolea mizigo, hapo utaona jinsi hawa jamaa watakavyofanya kazi kutoa mizigo kwa muda.

    Pili kazi ya ku assess kodi ifanyike mapema na watu walipe provisional assessed tax refundable in failure of delivery and adjustable after ukaguzi.

    Tabia ya kusubili manifest ndiyo wanaanza ku assess kodi ndiyo chanzo cha uzembe na ucheleweshaji wa mizigo bandarini, Ila nafikiri sasa umefika wakati kubadili mfumo wa ukusanyaji kodi mtu aki submit documents kuwa meli imeondoka basi akaunti yake ya kodi inafanyiwa assessment na kuambiwa kiasi cha kulipa kama provisional tax, meli ikifika mzigo unakaguliwa kama kuna additional anaambiwa na kulipa ziada akishatoa toa mzigo kodi inakuwa confirm kwamba earned. Hii itakuwa na ufanisi wa kasi sana.

    tatizo lililopo sasa wanasubiri mpaka meli iingie na kuona manifest ndiyo wanaanza ku assess, matokeo yako mzigo unakaa bandarini long time mpaka uwape rushwa ndiyo wanafanya fasta ili uepuke storage charges.

    System nzima inatakiwa ifumuliwe. Kama mtu akishindwa kuwakilisha docs on time basi ucheleweshaji wowote utokane na uzembe wake.

    Kwa kila mteja atakaye peleka documents zake apewe certificate of dicuments presentation ambazo zitaonesha tarehe aliyopeleka Documents zake na akiisha pewa provisional tax assessment apewe kielelezo cha lini alipewa ili akishindwa kulipia on time ndiyo Container ilipigwe mnada. Ila the current system inachochea rushwa zaidi kuliko utendaji kwani watendaji watatumia mwanya huo kuomba rushwa ili wateja waepukane na adhabu ya kupigwa mnada ma kontena yao.

    Naomba kama Mkuu wa nchi anapitia blog hii aongeze haya kwenye dondoo, vinginevyo ataua biashara na mapato ya nchi kwani mchawi si kuchelewesha mizigo mchawi ni system ya sasa iliyojaa rushwa na kutegea kupata storage kwa TICTS.

    Niliagiza gari 2008 nilijuta, mbali gharama za utoaji niliingia gharama za ziada(aka rushwa) kama Shs 900,000 na haikuchukua hata zaidi ya siku tatu nikatoa gari.

    ReplyDelete
  10. Kawa kifupi hapa JMK anachemsha tu sababu hii si kazi yake. Na haya maagizo yasiyokuwa na muda maalum na jisnsi ya kupata feedback yanaelekezwa tu kwa waandishi na wananchi hayana maana yeyote.
    Kazi hazifanyiki hivi na ukiona Rais anaanza kuingilia kazi ujue mambo yanamshinda..
    Mfano unaagiza mzigo CIF Dar es laam halafu wanakuambia ulipie kuupeleka UBungo sasa hiyo si kukulazimisha kubeba matatizo ya Bandari?? Kisheria inakuja?? Maana mimi sijaagiza wapeleke huko..
    Mimi namshauri JMK afanye kazi yake ambayo ni kuweka sera bora, kuteua viongozi safi, weleji na makini na kuhakikisha mfumo wa serikali unafanya kazi kikamilifu kuanzia waziri hadi mwenyekiti wa kijiji, n wawajibike.
    Hii anayofanya ni kwa ajili ya picha tu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...