Nimekuwa nafuatilia jinsi desturi ya kuchangia na kufanya sherehe kubwa inavyozidi kushika kasi, ikipelekea ule wigo wa kuomba michango kupanuka kiasi kwamba sasa hata mtu ambaye jina lako halijui vizuri anaweza kukuomba mchango.

Aidha michango na sherehe hizi zimekuwa mzigo mkubwa sana kwa baadhi ya watu, ikiwa ni pamoja na wale wenye kipato kidogo wanaochangiwa na kulazimika kulipa michango hiyo kwa miaka mingi. Je, wajua kuwa kuna familia ambazo zimefikia kulazimisha ndugu wauze mashamba au mifugo mtaji ili kupata fedha za kuchangia sherehe?.

Je, wajua kuwa kuna watu ambao zaidi ya nusu ya kipato chao wanatumia kuchangia sherehe na huku wakishindwa kulipia huduma muhimu kama shule, matibabu, lishe, nk. Na kuwa wakati mwingine wewe au mimi (au wengine kama mimi na wewe) ndio wenyeviti na makatibu wa sherehe hiyo?. Na ni sisi tunaoona fahari ya kutumia milioni 30 au zaidi kwenye sherehe usiku mmoja?

Kuna kijana mmoja jamaa yetu juzi juzi alipata shule Australia akawa anatafuta mchango wa dola 5,000 aende. Alipata 2,000 na amwekwama kwenda. Mwaka kesho akisema anaoa tutamchangia milioni 15-20!!!.

Hii si hadithi, ni ukweli, na ni kielelezo cha ulimbukeni tuliofikia.
Siku za karibuni nimetambua kuwa kuna kundi kubwa tu linasikitishwa na huu mwenendo, na hata kutambua kuwa tunaweza kuwa tunaandikiwa dhambi kubwa (na hukumu yatusubiri) kwa jinsi wengi wetu tunashindwa kusaidia mambo ya msingi lakini tunakuwa wepesi kutoa kwenye sherehe.

Wengi wanaamini kuwa tumeshatumbukia kwenye lindi la mazoea ambapo hatuwezi kujitoa mpaka upepo uje ubadilike wenyewe!.

Mimi nafikiri wasomi tuna jukumu muhimu la kuwa chachu ya mabadiliko pale ambapo mazoea yenye madhara yanavuka mipaka na kuweza hata kuwa chanzo cha ufukara na kuviza maendeleo.

Ili kubadilisha hili jambo, lazima tuanzie mahali. Mimi napendeleza na kuanza kutekeleza. Kuanzia Januari 2011, nitapunguza michango ninayotoa. Nitatoa tu kwa mtu wa karibu sana, na nitachanga kidogo.

Usishangae nikakuchangia 20,000/= kama ulitegemea 50,000/= kwa mfano. Kuanzia July 2011, nitaacha kabisa kuchangia sherehe. Badala yake nitakuwa nachangia elimu pale ambapo mzazi hayupo au mhusika kweli hana uwezo na pia nitachangia miradi mingine ya jamii na maendeleo.

Je waniunga mkono?

By Mdau wa Tegeta

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 38 mpaka sasa

  1. ulichosema ni kitu cha maana sana na muhimu kuokoa jamii yetu ambayo imefika pabaya. Ahsante sana kwa hoja muhimu. Nakuunga mkono

    ReplyDelete
  2. Nakuunga mkono mdau wa Tegeta, 100%! In fact mimi utaratibu huu mimi nimeanza huu utaratibu muda kidogo na maisha yanaenda. kweli ni kuchochea tu ufukara mifukoni maana kwa watu tulioko maofisini unawezza kukuta at least kila baada ya miezi miwili kuna mtu anaoa ama kuolewa basi ni mchango! mbaya zaidi maofisini tunajuana mishahara yetu ina range wapi basi unajitutumua angalau mchango uendane na mshahara wako! isitoshe tuna ndugu, majirani, marafiki nk ambao na wao wanahitaji michango ya harusi, kitchen party, send off, kipaimara nk! kwa haraka unaweza kukuta unaspend kiasi cha 40% of ur salary! huo si umaskini ni nini jamani????? FUNGUKENI WADAU!

    ReplyDelete
  3. ehh bwana eehh, I real support you on that, hiki kitu tulikuwa tunakijadili muda si mrefu na marafiki zangu na tumeona ni bora jamii ibadilike sasa na tutokomeze hizi mambo za michango ya sherehe unless realy demanded

    ReplyDelete
  4. NI KWELI KABISA HII MICHANGO YA HARUSI INAUMIZA SANA, UNAKUTA MTU UNACHANGIA WATU KAMA WATATU KWA MWEZI NA NI SH. 50,000/- WAKATI HUO NDUGU YAKO AKIJA KUKUOMBA MSAADA UNAMWAMBIA HUNA KITU, KWENYE HARUSI KINAKUWAPO. HATA MIMI NAKUUNGA MKONO NA MGUU KABISA NAMI NILISHAJIUNGA KWENYE GROUP LA KUTOCHANGIA KABISA. INGAWA NINA WATOTO WA KIKE WANNE. NA NILISHAWAAMBIA WATAKAPOOLEWA NIWAAGA NYUMBANI SIO UKUMBINI. NDOA NZURI NI HOME SIO UKUMBINI. HIVYO NAJUA HATA MIMI MWENYEWE NAWEZA NIKAANDA CHAKULA NA VINYWAJI. MAANA MIE SENDOFF YANGU NILIFANYIA NYUMBANI NA ILIKUWA BOMBA ILE MBAYA.

    ReplyDelete
  5. Hiyo ni kweli kabisa uliyoyasema, watu wamekuwa wazito sana kuchangia mambo ya msingi hasa pale linapokuja suala la elimu mfano mtu anaomba msaada wa ada labda ya elimu ya juu kutoka kwa famila na ndugu bila mafanikio na hii ni kutokana na kwamba watu washaona umefikia level ya juu ya elimu na wanaona kwanini wewe usome kiasi hicho so wanakataa kukusaidia kwa ajili ya chuki ya mafanikio yako na si kwakuwa hawana. hata kama labda ni ndugu alikuchukua tokea mdogo akakulea na kukulipia ada anapoona unaendelea vizuri labda hata unakaribia kuingia chuo utaona anaanza kubadilika na hata kufikia kukataa kukusaidia tena, hii naona ni chuki na wivu wa kuona kwanini fulani aendelee au afaidike ni bora ni changie harusi ambapo naenda nakula na kunywa nakufarahi kuliko kumsaidia mtu mwenye shida mfano mzuri ni huyo kijana alikuwa akiomba msaada na kushindwa kusaididiwask. Jamani ndugu zangu watanzania tubadilike na kuwa ni watu wenye upendo kwa wenye shida kwani unapomsaidia mwenye shida Mwenyezi Mungu anakuzidishia zaidi na zaidi.

    Mdau Sweden

    ReplyDelete
  6. Mi nakuunga mkono,harusi zimekuwa za gharama kubwa sana unajikuta kwa mwezi una card 5 @ mchango ni shilingi 50,000/= wakati kuna watoto yatima hawana uwezo pia kuna familia nyingi wanalala na njaa,mi siku hizi nachagua watu wa karibu ndo nachangia

    ReplyDelete
  7. Binafsi, hakuna ndugu yangu hata mmoja au rafiki atayeniomba mchango kwa ajili ya kufanikisha sherehe yake binafsi. Nina msimamo wangu, mimi nilivyoa sikutaka mtu yeyote anichangie kwani nilioa for myself na sikuoa kwa ajili ya jamii au ndugu. So in short, when I got engaged na mke wangu we sat down na planned when to get married. We worked hard and saved every penny we had ili tufanikishe ndoa yetu and we did. Na nilifanya hivi ili kuonyesha watu kuwa naoa for me si kwa ajili ya mtu mwingine. Kwa mtazamo wangu; yeyote aombaye msaada ili aoe basi huyo hayuko tayari kuishi na kutunza mke. Jamani huu upuuzi wa kuombana michango tuache.

    ReplyDelete
  8. Profesa Mbele amekuwa akisema jambo hili kwa muda mrefu tunambeza lakini ni tatizo ambalo inabidi tuliangalie na kidogo tubadilike. Tumeweka priorities zetu mahali ndipo-sipo.

    Nilishawahi pia kuligusia hapa kwa ufupi:

    http://matondo.blogspot.com/2010/12/fikra-ya-ijumaa-kama-tungemsikiliza-na.html

    ReplyDelete
  9. Nakuhunga mkono kabisa mtoa mada. Kwani nakumbuka hata mimi imetokea kwetu kwan mama wakati naenda shule advance haliomba michango kwan wakati baba yupo hai walikuwa wanachangia harusi lakini wapo walio mchangia na wapo walio mtupia kadi zake tukapia moyo konde akatuwezesha hadi hapa tuna mshukuru sana mungu na mama yetu pia katusaidia sana. Hivyo mimi pia ninawaambia vijana wenzangu hasa wanaotaka kuoa, kwan usipotuchangisha sisi ukafunga ndoa wewe na mwenza wako bila sherehe ya matarumbeta hamta ishi? Hivyo nami napendelea kuchangia michango yakumpeleka kijana shule kama kweli hana sapoti lakini michango ya harusi naipinga kwanguvu zote, nasina aibu nawaambia kabisa hata mkikasilika hayo ni maisha yako na mkeo tufikilieni maendelea tz tupo nyuma sana tusijidanganye na hizi phd za kutunukuwa viongozi wetu na sifa kibao kutoka mataifa ya nje jamani tutafute elimu. MAONI YANGU NI BORA NIKAPATA ELIMU BORA, NANIKAKOZA KAZI KWAN NITAISHI KWA AMANI SANA, ELIMU SIO SIFA KAMA MWALIMU NYERERE ALIVYO SEMA BARI INATUSAIDIA KUPAMBANA NA MAZINGIRA YANAYO TUZUNGUKA.

    Naipenda nchi yangu Tanzania.

    ReplyDelete
  10. mdau wa tegeta kwanza wewe binanfsi unahitaji kujiponya ili uwe na uwezo wa kutekeleza maamuzi binafsi badala ya kutaka kutumia kigezo cha 'wengi siku hizi hawachangii harusi'.
    kwanza nikuulize, umefunga ndoa kwa sherehe na shamrashamra za kuchangiwa? kama ndio, jibu ni rahisi tu kwamba lipa michango ya watu.
    kinyume cha hapo ni hiari ya moyo wala sijaona mtu akipelekwa mahakamani kwa kushindwa kulipa mchango wa harusi.

    ReplyDelete
  11. mdau wa Tegeta NyaishoziDecember 29, 2010

    Nakuunga mkono sana mdau,haya ndo mwazao ya kisomi,kuchanga sio tatizo lakini inapofikia mpaka inaleta madhara ktk jamiii ni tatizo kubwa,wabeba maboksi nao huwa wana fujo ili tujue wametoka nje ,nonsense!!!!!!

    ReplyDelete
  12. Meku-K'njaroDecember 29, 2010

    Mdau wa Tegeta,Mimi naungana nawe kwa asilimia mia moja.Tena naona kama kuanza Julai 2011 kuacha kuchangia sherehe utakuwa umechelewa sana.Hii ni tabia inayoashiria ulemavu na uzembe wa akili.Wenzetu wazungu hawana sherehe za kifahari(licha ya kuwa wana uwezo),maa nyingi wanafanya matembezi ya hisani,maonesho mbalimbali na pesa zinazopatikana zinazopatikana wanazituma Afrika kusaidia watu ambao hata mlo mmoja kwa siku ni tabu.Hapa kwetu Tanzania utakuta mtu yupo Jijini Dar,ana kazi nzuri na kipato kizuri,nyumba nzuri na anafuja pesa na nyingine nyingi anachangia sherehe(wengine kila mwisho wa wiki wana kadi ya mchango)na wanachangia kiasi kikubwa sana tu cha pesa,lakini mtu huyohuyo ana ndugu yake(mfano-mtoto wa kaka yake) amepata nafasi ya masomo hata pale chuo kikuu huria cha Tanzania na anahitaji laki tatu kwa mhula lakini atajibia-HAKUNA PESA..wiki hiyohiyo inakuja kadi ya mchango wa harusi tena wala sio ndugu na anachangia hadi laki 4..Yaani ni upuuzi mtupu,Hawa watu wapo wengi sana hapa Tanzania..Naomba yeyote atakayesoma mada hii awe chachu ya mabadiliko na awabadilishe na wenzake.Maendeleo ni sisi wenyewe,tuache kujitafutia'sifa za kijinga".tufane mambo ya maana.

    ReplyDelete
  13. Da!!!...umenikuna sana hili jambo limekuwa likinisikitisha sana na kweli mpaka leo nimeamua kumchangia mtu wa karibu sana tena sana,pili kinacho nisaidia sina marafiki wengi,2011 nafuta kabsa huu mzigo

    ReplyDelete
  14. Salaam,

    Yaani mdau una DUKU DUKU kama langu! mimi hii tabia inaniudhi sana! na siipendi kabisa, na kwa kifupi HUWA SICHANGII MTU! na ofisini kwangu wananijua kisawa sawa! mtu akileta kadi yake namwambia KWETU HATUCHANGISHI! tunaamini kuwa sherehe ni ujumuike wewe na ndugu zako na marafiki walio karibu na wewe unatakiwa uwakaribishe kwa kufanya kijisherehe kidogo ambacho unaweza kumudu! na zaidi ya hiyo kama unaweza mumpe bwana na bibi arrusi pesa yote mnayochangisha wakaanze maisha! utakuta mtu anafanyiwa sherehe ya million 30 lakini hana hata kibanda cha kumpeleka mkewe baada ya hapo! hata pesa ya chumvi hana jamani ULIMBUKENI HUU WATANZANIA TUNATAKIWA TUUACHE KABISA! ni ujinga uliokithiri utadhani tumerogwa! naandika kwa uchungu sana ! kama alivosema mdau mtoa mada kuwa utakuta mtu anaumwa anatikwa matibabu ya laki 5 tu watu wanashindwa kumchangia lakini subiri uje mchango wa arusi mtu atatoa hizo laki 5 yeye peke yake kjamani MUNGU ATUSAMEHE! sasa kama itawezekana inabidi hivi vitu watu tuelimishane ! mimi na ndugu zangu tumefanya sherehe za arusi na tumekula wali tu sherehe ambayo haipiti 1.5m na tunashukuru kwa MWenye Ez Mungu tuna uwezo wa kufanya sherehe hizo za mil 30. lakini badala yake ni bora kusaidia wasio na uwezo, kusomesha ndugu na jamaa ambao wantoto wao wana akili lakini hawana uwezo wa kusomesha watoto hao! jamani TUBADILIKE! tuwe kama wenzetu wakenya! mtoto akiwa anataka kwenda university hukaa pamoja na kufanya vikao kama hivi na kuraise funds KUPELEKA WATOTO VYUO!

    ReplyDelete
  15. Mi nakuunga sio mkono tu hata na mwili mzima. This thing has got to stop. Kama watu hawako tayari kufanya harusi then why bothering other people's money.
    kwakweli inabidi kuchangia wale ndugu wa karibu tu na marafiki ambao nao huwa wanakuchangia au kukusaidia ktk matatizo mengine
    kama mtu hana muda na wewe ktk shida na wewe kaa nae mbali ktk michango yake

    ReplyDelete
  16. mdau mimi sishangau hata kidogo kwa hili.nimekuwa nikifanya utafiti wa jambo hili nikagundua hayo ulioyasema. haya yote sio bure ile ni ugonjwa mkubwa wa life obsession jamii umepata. Lakini kama ninavyo amini upepo hubadilika mwelekeo.

    na naamini kuna watu watakuja na matusi kumponda mdau wa mada lakini sitoshangaa kwa hilo.

    ReplyDelete
  17. mimi nakuunga mkono kwa hatua uliyochukua,lakini bado hujaamua kikweli kweli.mimi naona michango isiwepo badala yake mialiko,ili anayefanya shughuli ajiandae mwenyewe kuliko kutegemea watu wamsaidie.kama huna uwezo sherehe za nini?kila kabila Tanzania lina tamaduni zake za kufanya sherehe nadhani zikifuatwa siyo mbaya kuliko kukimbilia utamaduni mimi nauita ulimbuko,ni kama vile watu wanashindana nani zaidi.

    ReplyDelete
  18. Nakuunga mkono mdau!

    Mimi huwa sichangii harusi na ndugu zangu huwa nawaambia hakuna kuchangisha na huwa sherehe tunafanyia majumbani mwetu. Anayetaka kuleta zawadi alete. Hela yangu nasomesha watoto wa ndugu zangu basi!

    ReplyDelete
  19. Nimeona hii mada nikaona na mimi niwe mmoja wa wakuchangia.

    Miaka ya nyuma-kama 13 hivi iliyopita nilikuwa na rafiki yangu aliyepata nafasi ya kuja kusoma hapa USA.
    Huyu jamaa akaomba mchango kwa ndugu zake, pamoja nakwamba walikuwa wamesoma-walimnyima kabisa-tena alikuwa anaomba hela ya nauri ya ndege tu. Vile alishapata ufadhili nje.

    Mbaya zaidi walidiriki kumsemea mbaya kwamba haendi kusoma anawazuga tu.
    Huyu jamaa aliwaambia wazi kuwa nyie mnapenda kuchangia arusi...( manapenda kuchangia pilau)
    kwavile mmenikatalia nitatafuta njia nyingine na Mungu atanisaidia LAKINI hata kwenye arusi yangu baadae msije mkanichangia.
    Huyu jamaa akahangaika kivyake na Mungu akamwezesha kwenye safari yake ya masomo nje ya nchi.
    Yale maneno huyu rafiki yangu aliyoyasema wakati ule..inaonyesha jinsi gani alikuwa na upeo wa juu wa kufikiria kuliko hata lile kundi zima la wale ndugu zake.
    Kweli watu bado wanachangia minuso(arusi) wanaacha kuchangia elimu?
    Hii ni laana kabisa...badilikeni jamani Watanzania.Elimu ni bora kuliko hayo mapilau mnayochangia!

    Mdau,
    Canada

    ReplyDelete
  20. HAKI YA MUNGU NAUNGA MKONO. NALINGANISHA NA WAKENYA KWA JINSI WALIVYO,HUCHANGIA HARAMBEE YA SHULE SANA KULIKO HARUSI ZA VODA FASTA HIZI.2 DAYS DIVORCE NA UCHAFU WA KISALITI WA KILA AINA.

    ReplyDelete
  21. Hili swala nilidhani ni mimi peke yangu naliona ni tatizo.. Watu wanaonyesheana ufahari kwa kuwa na budget kubwa ya harusi, na wengi wao hawajawahi tena kushika tena nusu ya hela alizotumia katika sherehe especially harusi.. Naona ni ufahari usiokua na maana hata kidogo.

    Mdau.
    www.greatdesign.co.tz

    ReplyDelete
  22. namuunga mkono mdau, kwa kweli michango hii inaumiza sana, mfano unaweza kutoa laki1 au 2 halafu hata huthaminiwi kabisa unaenda kwenye harusi wala hawajui kama ni wewe ndie ulietoa huo mchango mkubwa, mfano unapoenda kuchukua chakula unapewa kandizi kamoja na kipaja kimoja yaani hata hakilingani na pesa unayotoa utakaa pale kwenye foleni ya chakula kujichelewesha labda utaongezewa kinyama kingine lakini wapi!! na jamaa wanajifanya kama hawakuoni inabidi usalimu amri uondoke kisailensa sawa unalipia na ukumbi, mapambo lakini angalau vilingane na mchango ulichotoa kwa kweli michango noma sana na sasa nimejifunza sichangii mtu labda wa karibu saaana hata nae pia ntachanga kwa tabu sana!

    ReplyDelete
  23. Eheee.. Leo mmeleta mada iliokua ikinigusa sana. Hii naona ni ulimbukeni na ufahari usiokua na msingi wowote.. Inatupasa tubadilike sana.. Tuwe halisi, inakua ni sawa na kuigiza Movie kwani maisha ktk harusi ni ya kifahari sana tofauti na maisha halisia ya wahusika baada ya harusi (kiuchumi)
    Mdau
    greatdesign.co.tz

    ReplyDelete
  24. Toka ilipodhihirika kwamba siasa za Azimio la Arusha zimeshindwa, na toka Mzee Mkali Nyerere atoke madarakani, ulimbukeni uliokithiri umeikumba nchi yetu.
    Tazama ambavyo viongozi wanatumia pesa za umma kuingiza magari ya kifahari na kudai yanagharimu zaidi ya $200,000 wakati bei yake ya halali pamoja na vikolokolo vyote ni $80,000. Tazama wanavyoiba bila aibu kwa mirija isiyofichika kama Richmond na Dowans. Na wakisha kukwiba hivyo wanajenga (bila aibu kabisa) mahekalu ya kujisujudia na kuonyesha kwamba wanaweza kutumia.
    Nasi walala hoi tunajitia makundini ili nasi tuonekane japo siku moja katika arusi.Kwa hivyo tunachangishana au tunakamuana.
    This has got to stop. I love to party, I love having good time with friends and relatives. But I'd rather not try kunya kwa tembo, hasa wakati kuna mambo mengine mengi muhimu zaidi kwa mustakabali wa watoto wetu. Tunawafunza watoto tabia mbaya kabisa.

    ReplyDelete
  25. Hii ni ulimbukeni na hivi sasa ndugu zangu hawaongei na mimi vizuri ati kwa sababu niliwaambia msinichangishe mahela ya sherehe zenu. Hivyo sikuchanga hela ya X-mas mwaka huu basi kila mtu ananiona noma. Nikawauliza mimi nikibatiza watoto wangu huku niliko au kufanya sherehe ya x-mas nafanya sherehe kwa uwezo wangu. Sherehe ambayo nitaaford kulipa mwenyewe. Sichangishi mtu yeyote. Nyie kwanini mnafanya sherehe ambazo hamuwezi kuafford halafu mnaniambia mimi toa $500. Halafu wanasema sisi huku kila moja katoa laki 5 (as if I am stupid sijui exchange rates)

    Niliwaambia nyie mnapiga simu mnataka kiasi fulani kwa ajili ya sherehe.(wamenipangia nitoe sio mimi nachagua) Mnajuaje nina hiyo hela? Wakasema ati kama sina nikope mahali halafu niwape kwa vile wao ndio wanafanya hivyo. Nikawaambia mimi nitakopa na kutuma hela ya misiba lakini sio hela ya sherehe.

    Halafu niliambiwa ati usipofanya sherehe kubwa watu wanasema. Nikiwauliza ni watu gani hao wanasema? Hata hawana jibu ni ili inferior mind tu imejaa kwa waboongo hawana la kufanya ila ni kuchunguza nani ana kula nini, nani anavaa nini, anaendesha gari gani etc etc. Nikawaambia basi na nyie mnasema watu wengine?

    Mimi naona hii ni ujinga na ndio maana hatuendelei watu wanaishi maisha ya shida lakini ukiwauliza kwa nini mnafanya party za kukufuru wanasema kila siku watu wanakufa. Wacha tuenjoy.

    ReplyDelete
  26. Mdau wa TEGETA na wadau wengine wote kweli hakuna laana kubwa kama:
    Kuchangia arusi na kuacha kuchangia elimu..
    Hili jambo linanikera sana..Kwanini pasiwe na harambe za kusaidia vijana waende shule? Kuna maharambe ya mapilau kama mdau wa Canada alivyosema?
    Ni aibu sana, tubadilikeni jamani!

    Mdau ,
    South Africa

    ReplyDelete
  27. ...Wadau nawaunga mkono...kwanini tunapenda kulakula tu na kuacha kuchangia mambo ya maana kama elimu, ujenzi wa vituo vya afya na maendeleo mengine ya maana?

    Mnachangia arusi karne hii...alafu mnashindwa kumchangia mtu tena ndugu yenu aende chuo? Alafu mbaya zaidi kesho akifanikiwa mnamkasirikia eti anaringa yule...
    aibu kabisa.

    Mdau
    UK

    ReplyDelete
  28. Mdau umeleta mada ya maana sana na inayogusa jamii yetu sana tu. Mi naungana na wewe kuwa michango ya harusi haina maana hata kidogo naamini kama kila mtu ataamua kufanya sherehe ya harusi kutokana na kipato chake adha ya kugombana na watu kwa kuwa hajakutolea mchango itaisha. Mi ni mmojawapo ninayechukia michango ya harusi na siku ya harusi yangu nilihakikisha hamna cha vikao vya harusi (navyo ni upotevu wa muda) wala michango na sherehe ilifanyika vizuri tu.

    Ifike wakati wabongo tuachane na kuchangia harusi tuanze kuchangia mambo ya maana kama ada kwa ajili ya ndugu na marafiki tungekuwa na tabia hiyo naamini huyo aliyetaka kwenda kusoma nje angepata ada na yeye angeweza kuwasaidia wengine baadaye. Jamani tuache kuchangia harusi za kifahari wakati kuna ndugu wanahitaji ada za kwenda shule au fedha kwa ajili ya matibabu

    ReplyDelete
  29. Aisee naunga mkono!! Suala hili limekuwa ni kero laiti kasi ya vikao vya kukusanya michango ya harusi iliyopo miongoni mwa watu ingehamishiwa kwenye masuala ya maendeleo kama kuwakwamua ndugu zetu mbalimbali waliotaabani kimaisha na wagojwa tungekuwa mbali.Haingii akilini kwa mtu anayetegemea kuishi kwenye chumba cha kupanga kimoja choo cha passport size harusi yake inagharimu 10milioni, Binafsi sijaoa lakini sitarajii kufanya huu ujinga, nafikiri suala la muhimu ni kufanya kile unachokiweza usitake makuu ndoa si pombe nyingi,ukumbi wa kifahari etc.

    ReplyDelete
  30. Kweli maisha magumu....watu wamechoka kuchanga......

    ReplyDelete
  31. Afadhali wanaume asilimia fulani huwa hawajali maarusi makubwa lakini sisi wanawake tunapenda sana kufanya maharusi makubwa kuliko hata uwezo wa family na mume mtalajiwa. Tunataka kujionyesha kwa wasichana wengine kuwa harusi yangu imefanya kuliko yake! Jamani wakina dada tuache usumbufu huu. Ni afadhali tuoane wawili na wasindikizaji tu halafu niwe na nyumba nzuri kuliko harusi nzuri. Nyumba memory yake inaonekana kila siku lakini harusi baada ya miaka miwili watu hawakumbuki maana kutakuwa na zingine nzuri zaidi. Watu mkianza kugombana ndani bila hela ya kulipa rent hapo ndio watu wanajua upesi kuliko hata harusi ya mamilion! Wakina dada tusishindane tafadhali. Kama ni rafiki wa kweli utampata bila kushindana nae.

    ReplyDelete
  32. YAANI MDAU ULIYELETA MADA HII UMEFANYA JAMBO LA MAANA SANA,HII MICHANGO YA HARUSI IKOME KABISA MAANA IMEKUWA IKIWAWEKA WATU KWENYE WAKATI MGUMU WA MAISHA NA HOFU,TUNALAZIMISHA SHEREHE ZA KIFAHARI WAKATI FAMILIA NYINGI HAZIWEZI HATA KUJITOSHELEZA KIMAISHA,TABIA HII IMEZIDI SANA MIAKA HII YA KARIBUNI,MIAKA YA NYUMA WATU WALIKUWA WANAFUNGA NDOA SIMPLE TU NA ZINAFANA PIA WATU WANARIDHIKA,KWA SASA IMEKUWA KAMA MASHINDANO !!!!KAMA IKIBIDI TUCHANGIE SANA ELIMU,MATIBABU NK.TUWAIGE NDUGU ZETU WAKENYA KWA KUENDESHA "HARAMBEE"ZA KUCHANGIA WATU KWENDA KUPATA ELIMU YA JUU NJE YA NCHI NA SIYO HARUSI ZA KIFAHARI.IMEKUWA KAMA KASUMBA SIKU HIZI,TUJUE KUWA
    HII NI KERO KUBWA KWA WATU,MAISHA YENYEWE NI MAGUMU !!MISHAHARA HAITOSHI KABISA KUWEZA HATA KUKIDHI MAHITAJI YA FAMILIA MOJA NA HAPO HAPO KILA MWEZI MICHANGO YA HARUSI !!NADHANI UMEFIKA WAKATI WA KUBADILISHA SYSTEM HII,MBONA MIAKA YA NYUMA HAKUKUWA NA UPUUZI HUU???NA WATU WALIKUWA WAKIOANA KAMA KAWAIDA ??
    MTOA MAONI,USA.

    ReplyDelete
  33. Angalizo: Hii michango ya harusi haiishii Bongo tu, hata tulio ulaya, Wabongo wanaooana huku pia wanaendeleza tabia hizo hizo. Hata mimi binafsi kama siwafahamu maharusi sitoi kitu, na sijisikii vibaya kufanya hivyo.

    Kinachosikitisha ni hizo harusi za gharama kubwa kutoongeza thamani yoyote kwenye uhusiano. Mimi nilimvisha Ex wangu pete ya $1000 na chenji, ilikuwa gharama kwangu hiyo miaka michache iliyopita (na sasa bado naona hiyo ni pesa nyingi), lakini haikumzuia binti kufanya uhuni ndani ya ndoa. Tuwekeze kwenye ndoa zetu na mahusiano yetu mambo yatakayoboresha mapenzi na sio upuuzi wa harusi kubwa saaaana n.k

    ReplyDelete
  34. Kwanza nakupongeza sana ulieleta mada hii, kiukweli watanzania inabidi tubadilike tuanze kuwa tunatoa kipaumbele kwa michango ya mambo ya maana kama elimu na ugonjwa.
    Mimi nilishasitisha michango ya harusi, sichangii mtu yoyote unless ni ndugu tena wa karibu au very very close friend. There was a time in 2007, yaani katika kipindi cha miezi 3 nilikuwa na kadi 11 za kuchangia............ hivi mimi nina kipato gani cha kuchangia watu wote hao? na je sina mambo mengine ya muhimu ya maisha zaidi ya michango ya sherehe? Watu wengi wanaogopa kutochanga sababu wanaona kama watachukiwa na kuwekewa uhasama but no bwana, unajikuna unapofikia.

    ReplyDelete
  35. Dah Mdau ni kama umeniwahi, Yaani hiyo ni moja ya maazimio yangu 10 ya Mwaka 2011. Ila tofauti ni kuwa mie sipunguzi, nafuta kabisa michango yote inayohusu sherehe, kuanzia, harusi, kipaimara, bethdei, jubilee, mahafali n.k Michango yote ambayo haitohusisha kula na kunywa na viburudisho kama ngoma na muziki ntashirki kwa asilmia mia moja.

    ReplyDelete
  36. Yaani ndugu umenikuna vibaya sana. Kama ni kukuunga sio mkono bali ni akili na roho pia. Zaidi ni pale uliposema tunaweza tukapata dhambi kwa baadhi ya michango. Na wale wanaoomba michango bila hata kukujua jina ndio ombaomba kitu ambacho sio kizuri. watu jikuneni mnakojifikia.

    ReplyDelete
  37. Kwa kweli hii michango ya harusi inakera sana. Unajua watanzania tumekuwa watu wa ajabu sana - watu wanafanya harusi kwa bajeti za mamilioni ya fedha wakati maharusi wenyewe hawana kitu cha kuanzia maisha. Tunafanya ushindani - mara ooh kijana wa fulani alikuwa na bajeti ya milioni 15 sisi yakwetu tunataka ifike milioni 20; wakati huo kuna watoto kibao wanaotuzunguka hawana ada za shule au vijana wanaokosa mitaji ya shughuli ndogo ndogo za biashara mitaani kwetu. Ni pale tu tutakapoachana na hizi tabia za ufahari wa kijinga ndo mwanzo wa kuondokana na umaskini...

    ReplyDelete
  38. nilichanga elfu ishirini 20,000 nikaambiwa sitopata kadi ya mwaliko kwani kiwango ilikuwa ni 50,000 na kuendelea cha ajabu harusi sikualikwa na 20,000 yangu walichukua kaaaaaazi kweeeeli jamani mingine miradi na njaa za watu

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...