AMRI YA KUMKAMATA KIONGOZI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI YAINGILIA UHURU
WA BUNGE, YAHATARISHA DEMOKRASIA!!!

Dar es Salaam, Juni 3, 2011:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepokea kwa mshtuko, masikitiko na mshangao mkubwa taarifa za Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha kutoa amri ya kumkamata Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe. 

Mheshimiwa Mbowe pamoja na Wabunge, viongozi na wanachama kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanakabiliwa na mashtaka kadhaa yanayotokana na maandamano tarehe 5 Januari 2011 katika Jiji la Arusha yaliyopelekea Jeshi la Polisi kuua wananchi watatu na kujeruhi wengine wengi. Taarifa zinaonyesha kwamba amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Charles Magessa, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Mei 2011 na kurudiwa tena jana, yaani tarehe 2 Juni 2011.

Mheshimiwa Mbowe hakuhudhuria mahakamani katika tarehe zote mbili kwa vile amekuwa akihudhuria vikao vya Kamati mbali mbali za Bunge vilivyoanza tarehe 23 Mei 2011 na ambavyo vinaendelea hadi hivi sasa kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotazamiwa kuanza tarehe 7 Juni hadi tarehe 7 Septemba 2011. Kama Mbunge na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Mbowe ni mjumbe wa Kamati mbali mbali za Bunge
kama vile Kamati ya Uongozi, Kamati ya Kanuni za Bunge na Kamati ya Fedha na Uchumi. Aidha, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge na ndiye msemaji mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na amri ya kumkamata Mheshimiwa Mbowe kwa vile inakiuka moja kwa moja sheria, mila nadesturi za miaka mingi zinazohusu kinga, haki na mamlaka ya Bunge na ambazo ndio msingi mkuu wa demokrasia yetu ya kibunge. Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda “uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.”Uhuru huu wa kikatiba umetiliwa mkazo katika vifungu vya 5, 6 na 11 vya Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988 vinavyokataza Mbunge kukamatwa au kupewa amri ya kuhudhuria mahakamani wakati akiwa ndani ya eneo la Bunge au wakati Bunge limekutana bila kuwepo kwa kibali cha Spika.

Maneno ‘eneo la Bunge’ limetafsiriwa na kifungu cha 2 cha Sheria hiyo kumaanisha “ukumbi ambao hutumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, vibambaza (lobbies), maeneo ya wageni (galleries), courtyards, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya matumizi au malazi ya wajumbe, maafisa au wageni wa Bunge pamoja na njia zinazounganisha maeneo hayo na maeneo mengine yanayoweza kutangazwa na Spika kuwa ndani ya maeneo ya Bunge.” Kwa maana hiyo, Mbunge anapokuwa anahudhuria vikao vya Bunge au Kamati zake au anapokuwa mahali pengine popote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria vikao hivyo vya Bunge hawezi akakamatwa ili kutekeleza amri ya Mahakama au ya chombo kingine chochote nje ya Bunge.

Kufuatana na mila na desturi za kibunge za Jumuia ya Madola ambazo nchi yetu imezikubali na inatakiwa kuzifuata, kinga ya Wabunge dhidi ya kukamatwa inakuwa na nguvu wakati wa mkutano wa Bunge pamoja na muda muafaka na wa kutosha’ kabla na baada ya mkutano wa Bunge. Kwa mujibu wa Erskine May, mwandishi maarufu wa mila na desturi za mabunge ya Jumuia ya Madola, “muda muafaka na wa kutosha umechukuliwa kwa ujumla kuwa ni siku arobaini kabla na baada ya mkutano wa Bunge.” 

Kwa mantiki hiyo, wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha inatoa amri dhidi yake, Mheshimiwa Mbowe alikuwa analindwa na kinga ya Bunge.Aidha, Mheshimiwa Mbowe ataendelea kulindwa na kinga hiyo kwa kipindi chote cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na ‘muda muafaka na wa kutosha’ - kama unavyotambuliwa katika mila na desturi za Mabunge ya Jumuia ya Madola - utakapokwisha baada ya Mkutano huo!

Kwa upande mwingine, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa na unafiki na ubaguzi wa wazi unaoonyeshwa na Jeshi la Polisi juu ya Wabunge wa vyama vya upinzani. Hii ni kwa sababu wakati Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata Wabunge wa Upinzani bila kuomba kibali chochote cha Spika kama inavyotakiwa na Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge - kama ilivyotokea kwa Wabunge wa CHADEMA Waheshimiwa Mbowe, Godbless Lema (Arusha Mjini), Phillemon Ndesamburo (Moshi
Mjini), Joseph Selasini (Rombo), Meshack Opulukwa (Meatu), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalum, CHADEMA) na Magdalena Sakaya (Viti Maalum, CUF), wabunge wa CCM – na ambao wanakabiliwa na tuhuma za makosa makubwa zaidi – wamekuwa wanaombewa kibali cha Spika kabla ya kukamatwa. 

Kwa hili, tuna ushahidi wa barua ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza SP B.M. Wakulyamba kwa Katibu wa Bunge ya kumwomba Mheshimiwa Titus Mlengeya Kamani (Busega, CCM) ili akahojiwe na Jeshi la Polisi kuhusu kuhusika kwake na njama za kutaka kumwuua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Busega Dk. Raphael Masunga Chegeni.
 
Barua hiyo ya tarehe 31 Mei 2011 ilinakiliwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Makao Makuu ya Polisi DCI Robert Manumba. Hakuna Mbunge hata mmoja wa CHADEMA au chama kingine cha upinzani ambaye – kwa taarifa zetu – amewahi kuombewa kibali cha kukamatwa na Polisi kama inavyoonekana kwa Wabunge wa CCM. Hii inadhirihisha upendeleo wa wazi wa Jeshi la Polisi kwa Wabunge wa CCM

Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitarajii, naitapinga kwa nguvu zake zote, kitendo chochote cha kumtishia au kumkamata Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa 
Freeman Aikaeli Mbowe kwa kipindi chote ambacho ana kinga ya Bunge kama inavyotambuliwa na Katiba na sheria zetu pamoja na mila na desturi za kibunge ambazo tumechagua kuzifuata kwa hiari yetu wenyewe.


Aidha, tunatarajia Mahakama pamoja na vyombo vingine vyote vilivyoanzishwa na vinavyofanya kazi zake kwa mujibu wa sheria za nchi yetu vitatumia busara ili kuiepusha nchi yetu na fedheha ya kuonekana inakamata Wabunge wake wakati wakiwa wanatekeleza wajibu wao wa kibunge!

------------------------------
------
Tundu A.M. Lissu (MB.)
Mnadhimu Mkuu
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 04, 2011

    Bado hamjatambua tu kwamba watanzania wnengi wakiwemo mapolisi na mahakimu bado wanaiona CCM kama ndio serikali. Hayo ni madhara ya mfumo uliopita wa CHAMA KUSHIKA HATAMU.

    Jambo jingine wapinzani hasa Chadema mmeonesha nia ya kupambana na ufisadi, mnafikiri mtapendwa na hao mliowaita wanafiki wakati wanategemea ufisadi kuishi?

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 04, 2011

    Yaleyalee ya Kigamboni. Mimi ni mheshimiwa, kwa hiyo lazima nipite mlango maalumu, Sheria za nchi hazinihusu!

    Tulitegemea Nyie muonyeshe mfano wa kufuata taratibu za mahakama na sheria za nchi! sio Kiburi kwa sababu tu wewe ni mkubwa huko Bungeni!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 04, 2011

    Huo ni uonevu. jeshi la polisi someni sheria, kanuni na taratibu.msifanye mambo kama wehu na wendawazimu. nchi hii sio yenu. Usawa na haki udumishwe, sisi watanzania hatupendi vurugu kabisa..na mkae mkijua sasa hivi ndio tunasoma sheria kuliko hapo zamani,,haburuzwi mtu kishenzi hapa. acheni upuuzi.
    Umeniumiza sana ujinga huo.
    mdau
    ROK

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 04, 2011

    watanzania lazima muelewe mbunge yoyote hayupo juu ya mahakama hata kidogo lazima afuate sheria za mahakama tusiwe watu wa kutoelewa tusifate ushabiki tu wa kisiasa je wewe kama raia wa tanzania upo juu ya mahakama?mboe ni raia tu kama mwingine raia wa tanzania afate sheria za mahakama hayupo juu ya mahakama tuelewe ndugu zangu

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 04, 2011

    MHESHIMIWA LISSU, NAOMBA UWE KIONGOZI VILEVILE WA KUWASHAURI WATU WAFUATE SHERIA ZA NCHI. MH. MBOWE ANA KESI MAHAKAMANI, HATA KAMA ANAONEWA NI KWAMBA ANATAKIWA AENDE KESI IENDESHWE THEN UKWELI UTAJULIKANA. SASA KILA MTU AKIJIFANYA KUWA YUKO JUU YA SHERIA KWA SABABU YUKO JUU YA SHERIA, HATUTAFIKA JAMANI. TANZANIA INA WATU ZAIDI YA MILIONI 43, HAMNA ALIYEBORA KULIKO MWINGINE. WOTE TUNA HAKI SAWA NA KILA MTU AKIFANYA KAMA ANAVYOFIKIRIA NCHI HAITAENDA MAHALI. LAZIMA TUFUATE SHERIA ZA NCHI ILI KILA KITU KIENDE SAWA. KATIKA NCHI YETU KUMEKUWA NA TABIA YA WATU KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI KAMA WANAVYOAMUA WENYEWE. LAKINI HIYO SIO SAWA LAZIMA SHERIA IFUATWE. KWA HIVYO MH. HAINA HAJA YA KUANDIKA ESSAY NDEFU HAPA. WEWE NENDA MAHAKAMANI HUKO ARUSHA THEN KILA KITU KITAAMULIWA HUKO. I WISH U ALL THE BEST KATIKA KESI YAKO INAYOWAKABILI WAHESHIMIWA.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 04, 2011

    Sasa ina maana eti kwa kuwa huyu jamaa ni mbunge imekuwa ni halali kwake kuvunja taratibu za utawala bora na anapofanya huo uvunjifu wa amani ya nchi yeye kushitakiwa iwe ni mwiko? Ubunge wake utamudu kwa angalau miaka mitano, sasa ina maana asubiriwe hadi muda huo umalizike, yaani ni haramu kwake kuhudhuria mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili? Hii ndio aina ya utawala bora unaohubiriwa na CHADEMA na watu wenye uelewa wa sheria? Tuwe wakweli na waadilifu na tuachane na masihara.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 04, 2011

    We Tundu Lissu na Chadema wacheni unafiki wenu: (1) Mnatambua kabisa sheria inataka mtu anayeitwa mahakamani lazima ahudhurie na kama ana udhuru unaomfanya asiweze kufika mahakamani aiarifu mahakama. Mbowe alifanya jeuri tu. Angeliweza kumtuma wakili wake aipe taarifa ya kotoweza yeye kufika kortini. Hakufanya hivyo. He is not above the law!!!! (2) Sisi wenyeji na wazawa wa Arusha tumeona kuwa kuna wabunge watatu wa mkoa wa jirani wa kabila fulani ambao kazi yao kuja hapa Arusha (tarehe 5/1/2011 walidhamini mabasi 32 ya vijana wa kabila lao kuja kufanya fujo Arusha). Je sisi tukenda Moshi kufanya fujo watasemaje? (3) Komeni kuiita Arusha yetu "Moshi B". Mollel7.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 04, 2011

    Kyadema wanajua lugha moja tu: nguvu. Kyadema ni waongo wanaposema eti wanafuata utawala wa sheria. Kama wangelikuwa wanafuata sheria "mh" mbowe angelituma notisi ya kuwa hataweza kutekeleza summons ya mahakama.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 04, 2011

    kuna siku mboye alisema wakati wa kampeni ya uchaguzi kwamba wao wanachadema wako ktk hatari kubwa ya kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kukomboa nchi hii ya tz inayoshikiliwa na hawa mafisi akasema wanakazi kubwa ya kumtoa simba nyama ktk ya mdomo nanikweli kabisa mboye piga kiume usitishwe na mtu najua sheria unaelewa sasa hawa mafisi wasijekukutisha ukashindwa kutetea wananchi ambao wamekukubali Mungu atakupigania na utashinda hatakama ukiwekwa ndani utatoka tu wewe ni dume la mbegu laiti kama tz tungekuwa na wakina mboye kumi hii nchi ingekomboleka mboye songo mbele mtetezi wako yu hai usijali wananchi tuko nyuma yako iko siku ushindi itapatikana vita hivi nivikali kama ulivyowahi kusema kumtoa simba nyama ktkt ya mdoma sio mchezo good luck

    ReplyDelete
  10. AnonymousJune 04, 2011

    Nilivyosoma hii taarifa na ukweli wa kifubgu 100 cha katiba ya JMT, naona havina mahusiano. hii ni kwa sababu kifungu hicho kinaeleza pale mbumge tekeleza majukumu yake ya Kibunge bungeni, hawezi kushitakiwa. Hivyo ambacho sijakielewa, Huko Arusha ambapo Mbowe anashitakiwa, je anashitakiwa kama mbunge au Mbowe (mwenyekiti wa Chama)? Binafsi, naona ni vitu viwili tofauti hapa, hivyo kuunganisha taasisi mbili tofauti na matukio tofauti ni sahihi. Kwa hali hiyo Mbowe bado anawajibika kisheria kufika mahakamani.
    Pili, Mkuu wa Kambi rasmi bungeni ni ofisi wala si mtu. Hivyo anaweza kukaimisha au kumtuma mtu kwa niaba kwenye kikao husika. Inakuaje hii inakuwa ndio sababu? Bado narudi kusisita, katika kesi hii, Mbowe anawajika mahakama kwa mujibu wa sheria an katiba ya nchi.

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 05, 2011

    Ila jamani nani aliona siku ile Mbunge wetu Lema alipokuwa anatolewa nje kwenye kikao kimojawapo? hata kama alikosea niliona kama kuna madharau fulani vile.Hivi serikali inaangalia nchi za jirani wanavyofanya na yanayotokea? na imejipangeje, right there is some problem for our Government and wananchi, wananchi wengi hawajuisheria maana serikali iliifanya siri haikuweka sheria zote wazi zaidi zile ndogondogo tu kama usizini, usiue, usiibe even thou haikuwekwa wazi kuwa ukiiba sheria inasema hivi. Mi binafsi i was born in Tanzania but i wonder i dont know anything about sheria. Ingekuwa vema sana kuwafundisha wanafunzi mashuleni from primary school maana itaipunguzia serikali na mahakama kuwa na kesi ambazo hazina maana. But ukamlaumu mtoto wako kuwa kafanya kosa while hakujua kuwa ni kosa we kama mzazi majirani watakucheka. Ni kweli CCM ni waonevu na wanatumiaga vyombo vya sheria kama ni vya chama ni si vya serikali ila enyi ccm msishangae yatakayo wapata wananchi wenu coz now teenager are tired, maisha ni magumu wakiuza nyanya mgambo unawasumbua then wafanye nini kama si kupata hasira kuvuta bangi na kufanya maovu? Angalizo kwa viongozi"fikirini kabla hayajatokea" Kiongozi mzuri kwa kizazi hiki ni yule anayeona dunia kwa miaka mingi mbeleni than anayefikiri ya leo tu

    ReplyDelete
  12. AnonymousJune 05, 2011

    tatizo kuu la nchi yetu ni kutofuata sheria..hata barabarani ajali haziishi kwa sababu ya uzembe huu wa kutofuata sheria..hawa CHADEMA sasa wanataka kutuharibia amani kwa tamaa zao za madaraka...mimi nawaambia watanzania wenzangu msihadaike na mbwembwe za chadema wako pale kwa manufaa yao binafsi.....na hii ni tamaa ya madaraka...hakuna mbunge wala mtu yeyote aliye juu ya sheria ...sheria za nchi lazima zifuatwe...tumechoka kusikia mara maandamano mara wameenda kugombea maiti hospitali mara fungeni milango tupigane bungeni huko....kama kweli wana ucnhungu na chi na wanataka usawa basi wapiganie kupunguzwa posho na malipo ya wabunge na wakatae yae maVX wanayopewa kwa mikopo nafuu....fanyeni kazi watanzania wenzangu acheni ushabiki wa siasa..hakuna mtu atakaekuletea hela nyumbani kwako awe chadema wala ccm...basi hapo mbiwe kakamatwa wataitisha tena maandamano haramu bila kibali na watachezea kichapo tena...tufuate sheria kama nchi za wenzetu zilizoendelea..sio kutafuta umaarufu wa kijinga kwa vurugu zisizo na msingi

    mdau anayeona mbali ..MTWARA VIJIJINI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...