TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

13 / 09 / 2011

YAH: KUOMBA RADHI KWA NDUGU ZETU WALIOPATWA NA MAAFA YA AJALI YA MELI HUKO ZANZIBAR .

Usiku wa kuamkia jumamosi ya tarehe 10 / 09 2011 tukio kubwa na la huzuni lilitokea huko Zanzibar ambapo wananchi wengi walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa wakati walipopatwa na ajali ya kuzama kwa MELI iliyokuwa ikitoka Unguja kuelekea Pemba .

Kwa bahati mbaya siku hiyo ya Jumamosi taaasisi yetu ilikuwa inahitimisha Fainali za Taifa za Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania 2011.

Kama waandaaji wa Mashindano haya na wenye Mamlaka kamili ya maamuzi juu ya ama kuendelea au la kuahirisha jambo hili, tulipatwa na mshituko mkubwa sana juu ya tukio hilo .

kamati yetu ilikaa na kutakafari katika tukio hilo kwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

• Taarifa kamili ya maafa haya tuliipata rasmi saa tisa na nusu mchana ( 9:30 ) siku ya jumamosi ambayo ilikuwa ni masaa machache kabla ya Fainali za Miss Tanzania kuanza katika ukumbi wa Mlimani City .

• Wenzetu wa TFF waliendelea na mechi za ligi kuu ikiwemo ya Yanga na Ruvu Shooting.
• Katika kumbi za starehe ikiwemo mabaa na burudani za muziki wa bendi na kumbi za disco ziliendelea kama kawaida.

• Muda uliokuwa umebaki kuwakilisha jina la mshiriki wetu kwenye fainali za Miss World zilikuwa zimekwisha hivyo kulikuwa na hatari ya kupoteza nafasi hiyo

• Pia tamko rasmi la kusimamisha shughuli zote za burudani lilianza tarehe 11 septemba 2011 kuomboleza Kitaifa maafa hayo.

Hata hivyo kama waandaaji tulifanya shindano tukiwa katika maombolezo kwani kabla ya kuanza shindano Watu wote waliokuwepo ukumbini walisimama kimya kwa dakika moja na hata washiriki walipoingia kwenye jukwaa kwa mara ya kwanza walikuwa wamevaa vitambaa vyeusi katika mikono yao ikiashilia maombolezo.

Hali hii imetupa mkanganyiko na kujikuta tukiendelea na mashindano kitu ambacho tunaona tumewakosea Watanzania wenzetu.

Kama Waandaaji tunapenda kusistiza kwamba tunawajibika kwa hayo yaliyotokea na si Taasisi yeyote au Kampuni yeyote na tunaomba ichukuliwe kama ni makosa ya kibinaadamu hasa ukizingatia mazingira magumu tuliyokuwa nayo kwa wakati huo na mkanganyiko wa matukio na taarifa za tatizo hilo.

KUOMBA RADHI

Hata hivyo shughuli hiyo inawezekana imewakwaza watu wengi na kwa sababu hiyo na pia hali halisi ya janga hilo na kwa niaba ya viongozi wenzangu na wadau wa shughuli zetu tunatoa tamko la dhati kwa Familia za ndugu wote walikumbwa na maafa haya, wale wote walionusurika katika ajali hii na Watanzania wote kwa ujumla, kwamba TUNAWAOMBA RADHI KWA MKANGANYIKO ULIOTUTOKEA HADI KUFIKIA HALI HII. Hatuna neno zaidi ya kusema na kusisitiza “TUNAOMBA RADHI”

Mwenyezi MUNGU aziweke roho za marehemu mahali pema peponi,

Amina,

Hashim Lundenga
Mkurugenzi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Asante Boss umeeleweka kabisa na kupa big up kwa uamuzi wenu. biblia ilisema wacha wafu wawazike wafu wao. maisha yaendelee. huzuni bado ipo lakini pasipo wezekana hakuna jinsi.

    ReplyDelete
  2. MUUNGWANA NI KITENDO...KWA KITENDO HIKI CHA KUOMBA RADHI, KAKA TUMEWASAMEHE.

    ReplyDelete
  3. MR Lundenga hauta kosa lolote la kuomba msamaha hapa kwani ajali ni ajali na mbona shughuli nyingine nyingi hata za kisiasa ziliendelea kama zilivyopangwa! You have nothing whatsoever to apologize about kwani hajali haikupangwa na mwanadamu yoyote na taarifa zilichelewa kuufikia umma vilevile. Cha msingi sasa hivi ni kuendelea na kuumalizia msiba na kuwapumzisha waliotakulia katika haki katika nyumba zao za milele na kuwasaidia wajeruhiwa na familia zao. Sioni sababu ya ku feel guilt kwa kuendelea na tamasha kwani hata mngesimamisha msingebadilisha chochote. Anayekwazika analo lake jambo na sio uungwana. Kwahiyo uwe huru na hakuna kosa mlilolitenda la kuwafanya kuomba msamaha hapa.
    Asante.
    Mdau USA

    ReplyDelete
  4. Duu! 'uncle' tunapokea tu msamaha wenu kwa vile limeshatokea,lakini ukweli hamkututendea haki!..Yaani issue inatokea 'mtaa wa pili' tuu hapo, nyinyi huku mnaendelea na maraha?..uko wapi mshikamano wetu wa kitaifa?

    ReplyDelete
  5. Tumewasamehe kwani hamjui mlitendalo....

    ReplyDelete
  6. HONGERA LUNDEGA KWA KUONYESHA UUNGWANA KWA KUOMBA RADHI WATANZANIA UMEONYESHA KUWA NA BUSARA SANA KWA HILO NA NDIVYO TUNATAKIWA KUWA HIVYO KIBINADAMU BIG UP SANA -mdau ughaibuni

    ReplyDelete
  7. Lundenga bwana? Yaan hizo sababu ulizotoa wala hazina maana, eti kwasababu TFF iliendelea na mechio zake, hapo hapo unasema kumbi za starehe ziliendelea na shughuli zake, unaendelea kusema tangazo la kusitisha shughuli zote za starehe lilitoka tarehe 11. Kwahiyo tufuate lipi? We sema unaomba radhi kwakuwa watu walilipa hela zao na piga ula shindano lilikuwa lazima lifanyike. Huna sababu nyingine, acha kutuhadaa.

    ReplyDelete
  8. Unawachongelea TFF na wenye mabaa,lol! umekumbusha enzi za utoto,ili na wao waadhibiwe au waombe radhi pia, Sasa unahalalisha ulivyofanya kosa kwa vile uliona mwingine anafanya?

    Nimefurahi sana!!!

    ReplyDelete
  9. Bwana hashim Lundenga,huo uwongo,hata mtoto mdogo huwezi kumdanganya
    wewe sema kuwa hamukujali na suala hilo kwani nyinyi lilikuwa haliwahusu,lakini mfano huo ungelikuwa wa kwako naamini usingelifanya hivyo
    Kuhusu Taarifa ya ajali umesema umepata tisa na nusu si kweli habari zilikuwa kila kona ya dunia sema wewe na baadhi ya wzembe wengine hamukuta hizo habari

    ReplyDelete
  10. Kwanza kabisa I dont believe kuwa taarifa rasmi mmeipata saa 9.30 za mchana wakati dunia nzima ina taarifa hiyo by saa nne za asubuhi? Pili unashindana na mabaa kwa kuwa wamewekaburudani! Mabaa ni mambo yao binafsi, shindano la Miss Tz ni la kitaifa!

    Mdau hapo juu wa 11.56 PM, ulioongea kuhusu mambo ya kitoto kuchongeana, umenifurahisha, hahahahaha.

    ReplyDelete
  11. Lundenga shindano lako kubwa, tafuta mtaalam wa mahusiano / mawasiliano ya jamii yaani PR.
    Na hii si Lundenga peke yake bali taasisi nyingi hazijuwi kuongea na wateja, jamii na wengineo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...