Marehemu Steven Kanumba enzi za Uhai wake
Na Freddy Macha
Nilianza kumsikia- Stephen Charles Kanumba- wakati wa kazimoto la - Big Brother South Afrika 2009- aliposababisha mjadala mkali wa uzungumzaji wa Kiingereza.
Steve Kanumba alikuwa mwigizaji wa kwanza wa Kitanzania kujitokeza nje ya Bongo na mjadala ukawa moja ya matokeo yaliyochomoza kutokana na juhudi zake kisanaa. Wapo waliomcharura kuwa hakuongea Kiingereza sawasawa na waliotetea kwamba uzungumzaji Kiingereza fasaha haukuwa muhimu kuliko kipaji na jasho la mtu. Ila la msingi ni namna alivyojitokeza haraka na kutikisa bendera ya Bongo na waigiza sinema wa Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, nk.
Awali vijana walioitangaza nchi walipitia michezo - Filbert Bayi (1973) na bondia Titus Simba (1970). Tanzania haina majina maarufu ya kimataifa. Ukiacha Mwalimu Nyerere, mwandishi Shaaban Robert (aliyetwishwa tuzo la Malkia Elisabeth- akafariki 1962), wanamuziki Hukwe Zawose (aliyefariki 2003) na Remmy Ongala (ambaye alihamisha uraia wake toka Kongo, akafariki 2010)- hatuna jina linalowasha mwenge, kimataifa.
Steve Kanumba katutoka angali mbichi (miaka 28 si mingi)- jogoo aliyeanza kupeperusha mbawa, manyoya na kitundu. Ingawa tunaambiwa katoa sinema 100- bado hajulikani duniani-taifa letu changa-alichofanya ni kuonyesha dira na njia...kwa hilo ni nyota na mbalamwezi – shujaa wetu.
Fani aliyobarikiwa na kuchaguliwa kuililia marehem Kanumba ina nguvu sana leo ulimwenguni. Kwa miaka mia moja - fani hii imetawaliwa na Wazungu na Wahindi. Bado Waafrika hatujaikalia sawasawa. Ingawa ukipita mitaani na madukani utazikuta sinema nyingi za Tanzania- bado nchi yetu haina sinema inayotamkwa na midomo ya kimataifa- kiheshima na kiuchumi.
Hata hivyo kwa kipindi tulicho nacho sasa hivi-soko la kimataifa lina kiu na hamu ya filamu toka Afrika.
Mazingira na visa vyetu vinavutia. Tuna mengi ya kueleza na kustarehesha. Kimandhari- milima ya Lushoto, Meru, Usambara, Kilombero, mito na maziwa ya Tanganyika, Victoria, mbuga za Serengeti, Manyara, Kilimanjaro, Mikumi- bahari na visiwa vya Mafia, Unguja na bonde la ufa- mandhari tamu ya wanyama na wanadamu kisinema.
Si ajabu kwa miaka zaidi ya 60 sasa- Wazungu wameonyesha wanyama pori na mbuga na taswira za Waafrika kijuu juu- wakizingatia uchi na mainzi, tukifa njaa, tukiuana, tukiharibu, tukifanya upumbavu kuliko kuonyesha mazuri pia tuliyo nayo. Uzuri kisinema uko wapi na Mungu katukirimu mazingira ya kupendeza macho kushinda yote duniani?
Kombe la Soka la Dunia 2010 -Afrika Kusini lilirejesha hadhi. Rangi rangi, muziki, vicheko na tabasamu vilifuatana na tamasha. Sinema ya mpira na kuchekesha kuhusu vijana na watoto -Africa United- iliyotolewa na dada wa Kiingereza -Deborah Gardner Paterson-mwaka huo huo ilihusisha waigizaji na mazingira ya Rwanda, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Hivyo basi jitihada za Mtanzania yeyote kutengeneza sinema lazima zipigiwe makofi. Ila jitihada hizi lazima ziende na utaalamu, ufundi, mpangilio na busara- si kulipua na kubabaisha.
Harakati zake marehemu Steve Kanumba ni mwanzo wa baragumu na mchakamchaka. Mwanzo. Sinema zetu zina mustakbali mkubwa. Kifo chake si mwisho bali dirisha la hewa burudani kuendeleza filamu Tanzania.
kifo cha kanumba nakifananisha na kifo cha dandu na kifo cha amina chifupa
ReplyDeleteni vijana wadogo tuliowategemea sana kutuletea mengi kwa faida ya nchi yetu
mungu amewachukua wakiwa ndio kwanza taa imewaka kuashiria mwanzo wa sherehe
daima tutawakumbuka mchango na jitihada zao katika kuleta maendeleo ya nchi ya tanzania
kazi ya mungu haina makosa na tukumbuke ule usemi usemao KIZURI HAKIDUMU.
m,mungu ilaze roho ya marehemu pema peponi ameen.
ukiwa duniani,mema yako hayaonekani mpaka ufe.RIP kanumba
ReplyDeleteAsante sana kaka Macha kwa makala hii, Kuhusu marehem Steven kanumba (RIP),pamoja na kipindi hiki kigumu kwa sisi watanzania wote cha kuondekewa na msanii huyu,
ReplyDeleteKinacho sikitisha kuwa sifa hizi kwa nini ?ziandikwe mtu napokua marehemu!
Hivi kungekua na ubaya gani kama zingeandikwa wakati wa uhai wake? na mwenyewe akazisikia na kujua kuwa kazi yake ina thaminiwa na wengi, mpaka unapoandika makala hii unasema hakuna msanii au mwanamichezo aliyewasha mwenge kimataifa,kesho akifa mwingine utaandika haya haya! TUJARIBU KUISHI KATIKA UKWELI,MTU ANAPOFANYA JEMA BASI HAKI YAKE APEWE WAKATI YUPO HAI, SIO MPAKA UMAUTI UMFIKE NDIE ASIFIWE,
SHUJAA WA SINEMA STEVE KANUMBA (RIP)
Mzee Macha kaandika mambo mazuri sana...RIP Mr. Kanumba
ReplyDeleteRIP Kanumba.. Watanzania tutakukumbuka kwa mchango wako mkubwa!
ReplyDelete