Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (aliyevaa kilemba) akikata utepe kuzindua matanki ya kuvunia na kuhifadhia maji ya mvua yaliyojengwa Mkoani Dodoma kwa gharama ya shilingi milioni 627 kwa msaada wa WFP. kushoto kwake ni Mbunge wa Bahi Mhe. Omary Badueli
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi akikinga maji kwenye kikombe kama ishara ya uzinduzi wa matanki ya kuvunia na kuhifadhia maji ya mvua yaliyojengwa kwenye shule za msingi Mkoani Dodoma kwa msaada wa WFP.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (aliyevaa skafu) akipiga ngoma na kuserebuka pamoja na kikundi cha ngoma za asili ya kigogo wakati wa hafla ya kuzindua na kukabidhi matanki ya kuvunia na kuhifadhia maji ya mvua kwa shule za msingi Mkoani Dodoma, wanaomfuatia kushoto kwake ni Mwakilishi wa WFP Mkoani Dodoma Nima Sita, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Betty Mkwasa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Godfrey Jeremia.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (aliyevaa skafu) akipiga ngoma na kuserebuka pamoja na wanakikundi cha ngoma za asili ya kigogo wakati wa hafla ya kuzindua na kukabidhi matanki ya kuvunia na kuhifadhia maji ya mvua, anaemfuatia kushoto kwake ni Mwakilishi wa WFP Dodoma Nima Sita.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mpalanga Wilayani Bahi wakisoma kibao cha jiwe la uzinduzi wa matanki ya kuvunia na kuhifadhia maji ya mvua yaliyojengwa Mkoani Dodoma kwa gharama ya shilingi milioni 627 kwa msaada wa WFP.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dr. Rehema Nchimbi amesema atawachukulia hatua viongozi wa kisiasa wanaohamasisha na kushawishi wanachi wasichangie shughuli na miradi ya kijamii na ya maendeleo Mkoani Dodoma.

Hayo aliyasema leo katika shule ya Msingi Mpalanga Wilayani Bahi wakati wa hafla ya kuzindua na kukabidhi matanki 66 ya kuvunia na kutunzia maji ya mvua kwa shule mbalimbali za msingi za Wilaya za Mkoa wa Dodoma, matanki hayo yamejengwa na shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP chini ya mpango wa maji safi mashuleni na mpango wa lishe mashuleni na yamegharimu jumla ya shilingi za kitanzania milioni 627.

Dr. Nchimbi amesema kuwa viongozi hao wa kisiasa wanaohamasisha wananchi wasichangie shughuli hizo za Kijamii na Maendeleo sio viongozi makini wa kisiasa na wanasababisha viongozi wa serikali na watendaji wake kuonekana hawafanyi kazi yao ipasavyo.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Betty Mkwasa alisema kuwa kuna wanasiasa wanaoingiza siasa kwenye masuala ya jamii na maendeleo kwa kuwahamasisha wananchi wasichangie shughuli za kijamii na maendeleo.

Akitolea mfano wa mpango wa chakula/lishe mashuleni unaofadhiliwa na WFP kwa kuzipa chakula shule zote za msingi Wilayani Bahi na shule nyingine katika Wilaya za Mkoa wa Dodoma ambapo jukumu la wazazi ni kuchangia kiasi kidogo cha shilingi mia tano (500) kwa ajili ya kumlipa mpishi, kununulia kuni na kumlipa mlinzi amesema kuwa wanasiasa hao wanahamasisha wananchi wasichangie kiasi hiko.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa mpango wa kuwapa chakula wanafunzi wakiwa shuleni umepunguza sana utoro kutoka asilimia 70 mpaka kufikia 98 hivi sasa, pia umeongeza kiwango cha ufaulu kwa darasa la saba ambapo mwaka 2004 kilikuwa asilimia 24 wakati mwaka 2011 kilifikia zaidi ya asilimia 50. Vilevile kimeboresha afya za wanafunzi na kupunguza gharama za chakula cha mchana majumbani kwa wazaza kwa kuwa watoto wao wanapata chakula shuleni.

Kufuatia hatua hiyo Mkuu wa Mkoa ameagiza mikakati ya makusudi iwekwe kuongeza zaidi viwango vya ufaulu na kuondoa kabisa utoro, vilevile amewaasa wananchi kuchangamkia fursa za kuwekewa miradi kama hiyo kwa kuchangia pale inapohitajika. Aidha ameziagiza Hamashauri zote za Wilaya Mkoani Dodoma kuwa na mkakati wa kuvuna maji ya mvua kwa msimu wote wa mvua kwa kuanza kuweka miundombinu ya kuvunia na kutunzia maji ya mvua kwenye majengo ya Halmashauri na shule zote.

Aidha katika hatua nyingine Dr. Nchimbi amewaagiza wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Maafisa Ardhi kuweka mikakati ya kuwapatia walimu na watumishi wote wa Halmashauri viwanja vya ujenzi wa makazi na kuagiza wammpe taarifa za utekelezaji wa mkakati huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. huo ni muda wa kazi wajibikeni sio kucheza ngoma

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...