Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 4 Mei, 2012 alitangaza mabadiliko katika safu ya Baraza la Mawaziri.  Katika uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri, Mheshimiwa Rais aliwateua Mawaziri wapya kutoka miongoni mwa Wabunge aliokuwa amewateua na kuwatangaza.  Baada ya uteuzi huo, kumetolewa maoni kwamba hatua ya Mheshimiwa Rais kuwateua Wabunge Wapya ambao hawajaapishwa Bungeni kuwa Mawaziri ni kitendo cha uvunjaji wa Katiba.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayachukulia maoni haya kama ni jambo lenye maslahi ya jamii na linalohitaji kufafanuliwa; kwa upande mmoja lakini pia, kutolewa kwa elimu ya Umma; kuhusu Mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge. 

Msingi wa Katiba tunaoanza nao ni maelekezo ya masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 55(4) kwamba:
“Mawaziri na Naibu Mawaziri wote watateuliwa kutoka     miongoni mwa Wabunge”
Pili, ni mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wabunge aliyopewa na masharti ya Ibara ya 66(1)(e) yenye aina ya Wabunge wasiozidi kumi watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizotajwa katika aya za (a) na (c) za ibara ya 67 na angalau Wabunge watano kati yao wakiwa Wanawake.  Wabunge aliowateuwa Mheshimiwa Rais wanatokana na Ibara hii.

Tatu, baada ya hatua zote hizi ikumbukwe kwamba aliyeteuliwa au kuchaguliwa kuwa Mbunge anakuwa Mbunge ama baada ya kutangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi; au baada ya kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kwa wale Wabunge wa viti maalum au anapochaguliwa na Baraza la Wawakilishi au anapoteuliwa na Rais akitumia Mamlaka yake ya uteuzi yanayotokana na Ibara ya 66(1)(e). Hivyo Wabunge wanaohusika hawahitaji kuapishwa kwanza Bungeni ili wawe Wabunge.  Kiapo cha Mbunge Bungeni kinamwezesha tu kushiriki katika shughuli za Bunge. 

Katiba ya nchi haiweki kwa Rais masharti kwamba kabla ya kumteua Mbunge wa aina hiyo kuwa Waziri au Naibu Waziri Mbunge huyo awe ameapishwa Bungeni kwanza.  Masharti mawili muhimu na ya kuzingatia ni kwamba mteule wa nafasi ya uwaziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka kwa mujibu wa Ibara ya 56 ya Katiba, awe ameapa kwanza mbele ya Rais kiapo cha uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kitakachowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge.  Sharti la pili, litahusu kiapo cha Uaminifu katika Bunge kabla Mbunge hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge kwa masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba.  Viapo hivyo havitegemeani na vinaweza kufanyika kwa nyakati tofauti.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inasisitiza kwamba Wabunge ambao hawajaapishwa ndani ya Bunge ni Wabunge na wanapoteuliwa kushika nafasi ya Uwaziri au Naibu Waziri ni halali kwa kuwa uteuzi huo haukiuki masharti yoyote ya Kikatiba au Sheria.  Aidha, katika kutekeleza madaraka ya kazi ya Uwaziri au Naibu Waziri Mbunge atahitaji kiapo mbele ya Rais hata kama hajaapishwa Bungeni.  Busara ya uandishi wa Katiba na Sheria imetambua kwamba kunaweza kukatokea uteuzi wa aina hiyo wakati Bunge limeahirishwa kama ilivyo sasa.  Masharti ya Ibara ya 68 ya Katiba yatazingatiwa katika kikao cha Bunge kijacho.

Bila shaka ufafanuzi huu utaleta uelewa katika jambo hili na kuepusha mikangayiko isiyokuwa ya lazima.

Imetolewa na Jaji Frederick M. Werema (Mb)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
06 Mei, 2012
_______________________

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 15 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 06, 2012

    Kaazi kweli kweli, malalamiko yote hayo yametokana na kutokusoma na kuielewa katiba inasema nini.

    Hivi mimi huwa nashangaa watu wengine wanavyojifanyaga wanajua kila kitu, yaani huyo Rais na wasaidizi wote hao including Makamu wa rais, Mwanasheria Mkuu hawajui kitu isipokuwa mtu mmoja tu? Nendeni shuleee eeh! Na mkienda shulee someni acheni kudesa na kukariri itawasaidia kwenye thinking zenu

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 06, 2012

    Jaji Werema ni mbunge wa wapi? Mbona ameandika "Mb"? Tafadhali atufafanulie na hili kikatiba.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 06, 2012

    Bravo, watoa dukuduku

    bila ya malalamiko elimu ya uma ingetolewa lini?.


    Mnyagatwa USA

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 06, 2012

    Na JE, SUALA LA MNZANZIBARI KUWA WAZIRI KWENYE WIZARA ISYO YA MUUNGANO HILO SIO LA LIKATIBA NA WALA HALIJAVUNGA SHERIA NA HATI ZA MUUNGANO?

    ReplyDelete
  5. AnonymousMay 06, 2012

    Mimi naanza kufurahishwa sana na serikali yetu ya sasa maanaimeanza kuota masikio. Enzi hizoooo hata mpige kelele mgalegale chini, ufafanuzi kama huu hautolewi ili watanzania wote wakaelewa na kujifunza mwenendo mzima wa jambo linaloendelea. Sasa malalamiko yakitokea tu serikali inajibu na kutoa ufafanuzi ili kudumisha mahusiano mazuri kati ya serikali na wananchi wake. Juzi moto umewaka Bungeni, serikali imeonyesha mrejeo nyuma, Jana tu upinzani umeibua suala la ukiukwaji wa katiba ya nchi katika uteuzi alioufanya Rais, na leo tena sio siku ya kazi mrejeo nyuma umesikika. Tunashukuru upinzani kwa kupandikiza vijisikio kwenye kichwa cha serikali sasa inaanza kusikia.

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 07, 2012

    We mdau wa kwanza sheria haina bingwa wake hata kama ulienda shule ya sheria ukawa bingwa inawezekana ukakosea kuitafsiri sheria ndo maana hata mahakamani mhukumiwa ana haki ya kukata rufaa na rufaa ikasikilizwa na akashinda japo mwanzo alishindwa. Binafsi nlisikia pia ningependa kupata ufafanuzi wa uteuzi mwingine wa Rais. Hizi wanaziita siku hizi changamoto za Muungano. Ni kuhusu uteuzi wa Dr. Mwinyi kua waziri wa Afya

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 07, 2012

    Katiba haimzui Rais wa Jamhuri ya Muungano kumteua mwananchi wa Jamhuri ya Muungano kutoka sehemu yoyote ile ya Jamhuri ya Muungano kuwa waziri wa wizara yoyote ya serikali ya Jamhuri ya Muungano.Labda kama mnataka kuwe na makatazo na vizuizi aina hiyo basi mpelekeeni jaji Warioba sasa na Tume yake kama kero yenu ya muungano ili hilo liingizwe kwenye katiba mpya.
    Mjadala huu mzuri, nimeupenda; tusiishie hapa kama liko linalotukera kikatiba, tukashtaki kwa Warioba sasa!

    ReplyDelete
  8. AnonymousMay 07, 2012

    Anoni wa pili. Mwanansheria Mkuu kwa nafasi yake ni Mbunge ndani ya Bunge la Jamhuri. Na anashiriki katika vikao. Vilevile anashiriki kikao cha Baraza la Mawaziri kwa nafasi yake. Soma katiba yako.

    ReplyDelete
  9. AnonymousMay 07, 2012

    Hii ni Live bila chenga:

    Jaji Werema maefafanua vizuri sana, tatizo ni kuwa wengi huwa wanakurupuka tu kutoa malalamiko na kuwa na sintofahamu nyingi tu.

    Nasikia pana Mwana mama mmoja Mbunge wa Kuteuliwa Viti Maalum alipoona Mhe. Raisi amewapa Uteuzi wa Ubunge wengine watatu (3) na halafu akawapa Unaibu Waziri wanamama hao (2) na Mwanaume Uwaziri Kamili, huyo Mwanamama aliyekuwa Viti Maalum ikamkera!

    Angalieni watu hawa wenye tamaa ya Madaraka ni watu hatari sana ktk jamii yetu, alitaka labda Unaibu Waziri apewe yeye Viti Maalum!

    Hivi jamani unapokuwa Mwanasiasa (tena Mbunge wa upendeleo wa Viti Maalum) ni lazima wakati wote watu wakufikirie kukupa Madaraka zaidi kama Uwaziri?

    ReplyDelete
  10. AnonymousMay 07, 2012

    Jamani, Mzanzibari yeyeote ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwahiyo kama sifa anazo anaruhusiwa kuwa Waziri kwenye serikali ya Muungano, lakini kwa upande mwingine Mtanzania Bara haruhusiwi kuwa waziri katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Dr. Mwinyi anaruhusiwa kabisa kuwa waziri katika wizara ya Afya. Tanzania Bara hatuna serikali kama ilivyo kwa Zanzibar. Mheshimiwa Rais hajakosea kabisa kumteua Mzanzibari kwenye serikali ya muungano. Tatizo Wabara wengi wanachanganya Serikali ya Muungano na Tanzania Bara (isiyo na serikali).

    ReplyDelete
  11. AnonymousMay 07, 2012

    Mimi nafikiri Katiba imekiukwa. Hata Tume ya Uchaguzi inapomtangaza mshindi wa kiti cha Rais, mshindi huwa ni Rais mteule hadi atakapoapishwa na kula kiapo cha Urais. hali kadhalika mbunge anapotangazwa anakuwa mbunge mteule hadi atakapokula kiapo cha ubunge.....hii iko wazi, vinginevyo, mwanasheria mkuu anataka kutuambia kuwa hivi viapo havina maana na umuhimu kihivyo....

    ReplyDelete
  12. Walter, Godluck.May 07, 2012

    Mr.Michuzi,
    Tunaomba kwenye hizi pages za taarifa zako, toa option ambayo itamruhusu mtu kama ameipenda au ameiona ni ya muhimu anaweza ku"LIKE" au aweze kui-post/ ku-share kwenye Facebook maana yawezekana sio wote wameiona, lakini akahitaji kuwafikishia jamaa zake hasa mambo muhimu kama haya yenye Elimu ya Uraia ndani yeke.

    Regards,

    ReplyDelete
  13. AnonymousMay 07, 2012

    Raisi amekiuka katiba. Jaji Werema anapiga siasa badala ya kusimamia katiba. Naomba tuonyeshwe mahala popote huko nyuma ambapo Raisi (yeyote, Nyerere, Mwinyi na Mkapa) aliwahi kuteua mawaziri ambao hawajaapishwa kuwa wabunge bado? Naomba tuletewe mifano na sio kukanusha tu.
    Halafu Wizara ya Afya vilevile Raisi amevunja katiba. Hii sio wizara ya Muungano. Mbona Jaji werema anachagua lipi la kujibu? Hii imelalamikiwa mbona hajasema kuwa ni sawa kwa Raisi kumchagua mtu toka upande wa pili wa Muungano kwenye wizara isiyo na Mambo ya Muungano? Tunaomba utolee ufafanuzi la hilo Jaji Werema.
    Nawasilisha.
    Mdau#1

    ReplyDelete
  14. AnonymousMay 07, 2012

    HIVI MBARA ANAWEZA KUWA WAZIRI KATIKA SERIKARI YA MAPINDUZI ZANZIBAR ?

    ReplyDelete
  15. AnonymousMay 08, 2012

    Katiba yetu bado ina mapungufu sana. Ningeshauri katika mchakato wa kuandika katiba mpya, "madaraka ya Rais" yapunguze, ili asiwe anafanya maamuzi bila kukiuka sheria (katiba) ya nchi. Maana ukisema tu, hakuna umuhimu wa mbunge kula kiapo, basi mi sioni umuhimu wa wabunge kuapa pale bungeni..

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...