Na Luppy Kung’alo wa Jeshi la Polisi Dodoma.

Mwanafunzi wa Darasa la Saba shule ya msingi Hogolo, aliyefahamika kwa jina la Matha Mazoea Mwenye umri wa Miaka (14) ameuawa kwa kunyongwa na kufukiwa kwenye shimo nyuma ya nyumba yao karibu na choo baada ya kubakwa.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Zelothe Sephen alisema tukio hilo limetokea mnamo tarehe 11/08/2012 majira ya saa 08:00 asubuhi katika mtaa wa Ikulu Kijiji cha Hogolo Kata ya Hogolo tarafa ya Zoisa Wilaya ya Kongwa.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi kwani marehemu alikuwa amevunja uhusiano na mpenzi wake wa muda mrefu aliyejulikana kwa jina la Heri Aboubakar na kuanzisha uhusiano na mpenzi wake mpya aliyefahamika kwa jina la Wilfredy Muhaha @ Kabo mwenye miaka (17) “ Alielezea Kamanda Zelothe

Katika tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji hayo ambao ni Asha Jafari Mohamed mwenye umri wa miaka 16, mkulima, mkazi wa Mtaa wa Nyerere Hogolo ambaye ni rafiki wa marehemu na Rino Mazoea mwenye umri wa miaka 21, Mkulima, Mkazi wa Ikulu Hogolo Wilayani Kongwa ambaye ni kaka wa marehemu.

Bw. Zelothe alieleza kwamba ili kufanikisha uchunguzi wa awali Jeshi la Polisi pia Wilayani humo linamshikilia mpenzi mpya wa marehemu Bw. Wilfredy s/o Muhaha pamoja na kumtafuta mpenzi wa zamani wa marehemu Bw. Heri s/o Aboubakar ambaye amekimbia kijijini hapo na hajulikani alipo mpaka sasa.

Aidha kamanda Zelothe alisema Katika tukio hilo Kaka wa marehemu ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi, katika maelezo yake ya awali alidai kusikia purukushani zikitokea usiku wa tukio hilo la mauaji lakini hakuweza kutoka usiku huo ili kushuhudia nini kinaendelea.

Kamanda Zelothe alisema Marehemu alikuwa akiishi na babu na bibi yake hapo Kijijini na kwamba siku ya tukio walikuwa wameondoka kwenda katika Vijiji vya jirani, ambapo bibi yake na marehemu alikuwa amekwenda Kongwa kwa ajili ya kujengea makaburi na babu yake alikwenda kijiji cha Banyi banyi kwa Shughuli za kutemebelea wagonjwa.

Wakati huo huo Gari lenye namba za usajili T. 750 AEU aina ya TOYOTA CHASER likiendeshwa na Kenedy James mwenye umri wa miaka 48, Mkazi wa Mpwapwa liliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha Salum Kaduma mwenye umri wa miaka (13) Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Katika shule ye sekondari ya Mpwapwa, na kusababisha kifo chake.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma alisema ajali hiyo ilitokea mnamo tarehe 12/08/2012 majira ya saa 09:00 asubuhi katika eneo la Kisima Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa magurudumu mawili ya upande wa kulia kitu kilichopelekea gari hilo kuacha njia na kupinduka.” Aliongeza Bw. Zelothe

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Jamani tunaenda wapi...? 14 yrs kufa kwa wivu wa mapenzi..! Am very sad

    ReplyDelete
  2. Mmh, hao waliovunja mahusiano na kuhamishia kwingine ukiangalia umri wao, unabaki kuguna mwenyewe tu. Eeh Mola nusuru wanetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...