NA RAYA HAMAD - MAELEZO ZANZIBAR

Imeelezwa kuwa moja kati ya neema alizopewa mwanaadamu ni umri mrefu hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuutumia vyema uhai wake kwa kutenda mema na kushukuru kila siku kwani hapaswi mwanaadamu kuwa aasi bali anachotakiwa ni kumuabudu Mola wake aliyemuumba .

Kadhi mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji Khamis ameyasema hayo katika dua ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kutimiza miaka 93 ya kuzaliwa kwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Alhajj Aboud Jumbe Mwinyi iliyofanyika Kiembe Samaki .

Sheikh Khamis Haji ametowa ukumbusho kwa kusema kuwa “ Ifanye dunia kama kwamba utaishi milele kwa maana ya kutenda mazuri na kumuabudu Allah kama tulivyoamrishwa katika dini pia ifanye akhera yako kama utakufa sasa kwa maana ya kujiandaa kwa kutenda amali njema na kuomba msamaha kila siku .

Katika khutba yake iliyosomwa na Ustadh Moh’d Yoyota kwa niaba yake Rais Mstaafu Awamu ya Pili Alhajj Aboud Jumbe amesema kuwa anamshukuru Mola wake kwa umri aliyomjaalia kwani ameshuhudia neema nyingi ambazo hazina kiima kisicho kifani,kina wala mizani katika maisha yake na kupitia nyanja tofauti za maisha hadi M/Mungu atakapomjaalia mwisho wa maisha yake.

Alhajj Aboud Jumbe ameongeza kusema kuwa anamshukuru Mola wake kwa kumpa rehema zake huruma na hisani pale alipokabidhiwa dhamana ya kuongoza baadae kumnusuru na kumfariji na hatimae kumuongoza pale alipoteleza mnamo asiyoyaridhia kwani majibu sahihi ya mithani yetu wanaadamu yanasubiri siku ya malipo ambayo yatupasa tutambue kuwa kila mmoja wetu atakutana nayo.

“Namuomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu azidi kuitakasa amali yangu na kunipa khusni l khatima mimi pamoja na waislamu wenzangu “

Akitowa shukurani kwa waalikwa waliohudhuria katika dua hiyo kwa niaba ya familia ndugu Mustafa Aboud Jumbe ambae ni mtoto wake amesema kuwa lengo la kusoma dua hii ni kukumbushana namna gani tunatumia neema na kila mmoja vipi atautumia uhai wake na kusisitiza kuwa dua hio ni mwenyewe baba yao aliyetowa utaratibu juu ya namna gani isomwe dua hio “Tumekuwa tukipata masuala mengi kuhusu hali ya mzee wetu jibu ni kwamba hajambo ila uzee tu ndio unaomsumbua, nuru ya macho imepotea ,kusikia kumekuwa shida kidogo lakini anasikia na anazungumza na hii shughuli yake ya leo amepanga mwenyewe”alisisitiza Mustafa Jumbe.

Nae Sheikh Moh’d Iddi ametowa wito kwa jamii kufanya matendo mema kwani kuwepo kwetu ipo historia ambayo M/ Mungu amewashushia waja wake na aliyebahatika kuishi kwa kumuabudu huyo atakuwa amefaulu.

Miongoni mwa waliohudhuria katika dua hio ni pamoja na Kadhi Mkuu Mstaafu Sheikh Habib Ali Kombo baadhi ya Masheikh, Familia yake, baadhi ya wanafunzi aliwahi kuwasomesha na kuwafundisha kazi .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Rehema JettaJune 17, 2013

    Allahuma Ameen

    ReplyDelete
  2. Nami kuombea Mola, kujalia siha njema,
    Ule kunywa na kulala, ushuwarike mutima,
    Akwepushe na madhila, akupe njema kalima
    TISINATATU SI HABA, AKUJALIYE MINGINE.

    Akujaliye mingine, 'TISINATATU' si haba.
    Yanojiri uyaone, ya leo hii nasaba,
    Kwa pamoja tuungane, penye kheri na misiba,
    INSHA ALLAH FIKA KARINE, PASI YEYOTE ADHABA.

    Baidi umetokea,' TISA TATU' losimama,
    Mengi umeshuhudia, dahari zote za nyuma,
    Nyadhifa ulipitia, hukudiriki dhuluma,
    RABI MOLA KUJALIA, KUPA 'KHUSNI-L-KHATIMA'

    Nne beti zinatosha, kuombea kwa KARIMA,
    Umrio urefusha, kikuongoza kwa mema,
    Yafata loamrisha, yaepuka alosema,
    HAPA SI PETU MAISHA, KUPA MWISHO ULO MWEMA.


    Nimelazimika kuikumbuka nyimbo hii".....TUNAMUOMBEA DUA RAIS BABA JUMBE AKALIE KITI CHAKE KWA SALAMA NA AMANI..." yalikuwa ni baadhi ya maneno katika wimbo huo enzi hizooo!!!!


    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 18, 2013

    HK, Hilal wa family mirror!? Uko Wapi?


    sesophy@yahoo.com

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...