Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene akizungumza  na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam  kuhusu  mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ulioituhumu   Serikali ya Tanzania.Picha na Hassan  Silayo – MAELEZO.
--
Na Fatma Salum- MAELEZO
SERIKALI  ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma mbalimbali dhidi yake zilizotolewa na mtandao wa kijamii wa nchini Kenya ujulikanao kama   www.standardmedia.co.ke  unaosadikika kuendeshwa na kampuni ya gazeti la The Standard la nchini humo.
Akizungumza  na waandishi wa habari leo  jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari- (MAELEZO) Assah Mwambene , alisema mtandao huo umeripoti kuwa  Serikali ya Tanzania imekataa kuiuzia Kenya gesi asili ya Songosongo jambo ambalo halina ukweli  kwa kuwa  gesi inayozalishwa hivi sasa bado haijafikia kiasi cha kuweza kuuzwa nje ya nchi.
Mtandao huo pia umeripoti kuwa Serikali ya Tanzania ilikataa viwanja vyake vya ndege vya kimataifa kutumiwa na ndege zilizopaswa kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata wakati wa ajali ya moto iliyotokea kwenye uwanja huo hivi karibuni.
Mwambene alifafanua kuwa tuhuma hizo ni za uongo kwani mara baada ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyata kuwaka moto, ndege zilizotakiwa kutua uwanjani hapo ziliruhusiwa kutua kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania vya Julius Nyerere   International   Airport (JNIA) na Kilimanjaro International Airport (KIA).
“Sio kweli hata kidogo kwamba Tanzania ilikataa ndege za Kenya zisitue kwenye viwanja vyake kwa sababu uwanja wa Jomo Kenyata ulipoungua ndege nyingi zilizopaswa kutua katika uwanja ule zilitua kwenye viwanja vyetu na hii pia ilitokana na ukweli kwamba Tanzania na Kenya zinachangia ndege nyingi za nje ya nchi,” alisema Mwambene.
 Aidha Mwambene alikanusha tuhuma nyingine iliyodai kuwa mwaka 2010 Tanzania ilikataa kuiuzia Kenya chakula badala yake ikaiuzia nchi ya Uganda taarifa ambazo si za kweli kwa kuwa mwaka huo nchi nyingi za Afrika zilikumbwa na baa la njaa ikiwemo Tanzania yenyewe. 
Hivyo  Tanzania  ililazimika kusitisha utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara kuuza chakula nje ya nchi na hakukuwa na taarifa yoyote ya kuuzwa chakula nchini Uganda.Kutokana na upotoshaji huo Mwambene alisema Serikali ya Tanzania imeutaka mtandao huo kuomba radhi na isipofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Katika hatua nyingine Mwambene alifafanua kuwa zoezi linaloendelea nchini  la kuwataka wahamiaji haramu wanaoishi hapa kinyume cha utaratibu kuondoka kwa hiari haliwahusu wakimbizi waliopo nchini kisheria. 
Pia zoezi hilo linawalenga wahamiaji haramu wote kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Congo DRC, Zambia na Uganda na hakuna serikali ya nchi yoyote kati ya hizo iliyolalamika kuhusu hatua hiyo.
“Mpaka sasa zoezi linaenda vizuri hakuna taarifa yoyote ya malalamiko kutoka Zambia, DRC, Burundi, Rwanda wala Uganda na tayari Rwanda imetuma taarifa rasmi kuishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendesha vema zoezi hilo. Kinachoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari ni upotoshaji unaolenga maslahi binafsi ,” alisisitiza.
Akizungumzia usalama wa Watanzania nchini Rwanda, Mwambene alisema hakuna taarifa ya  Mtanzania yeyote kunyanyaswa nchini  humo  na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Tanzania haujakatika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. kaka mwambene nakupongeza kwa hatua uliyochukua hasa kwa kuzingatia hali iliyopo sasa

    ReplyDelete
  2. tujitoe tu umoja wa Afrika Mashariki kwa majungu yamekuwa mengi na hakuna tunachofaidika na umoja huu. kikubwa wanataka ardhi na raslimali zetu.

    ReplyDelete
  3. Wakati mwingine msiwajibu hao watu wanataka kutufanya kama sisi mbumbu,sasa kuuza gesi imekuwa lazima jamani?inabidi tuwe waangalifu sana na hawa watu hasa Kenya kwa kuwa hata katika hali ya kawaida wanatudharau sana na kujiona wapo juu kwa kila kitu.Nia yao kubwa kwenye jumuia ni kutaka kutumia opportunies kwa faida ya nchi yao na si kingine hasa ardhi,wakenya na wanigeria hawana tofauti. Serikali ikae kuangalia matatizo ya ndani ya uchumi ajira na kupambana na madawa na rushwa badala ya kutumia muda mwingi kujibu tuhuma zisizo na msingi na zinazolenga kupoteza muda wetu wakati wao wanafanya mambo ya maana.

    ReplyDelete
  4. Lecturer Benson Bana wa Chuo Kikuu Dar Es Salaam wa Idara ya Sayansi ya Siasa alisema ktk suala la Afrika ya Mashariki mambo makubwa mawili yanayotakiwa ni:

    1.Maamuzi na mahitaji papendekezwe na watu na sio Wanasiasa:

    (Citizens should propose and not Politicians)

    2.Inahitajika MANTIKI YA NGUVU na sio NGUVU YA MANTIKI:

    (Needs Force of Logic and not Logid of force).

    Hivyo kama yalivyo Mashirikihso mengine Duniani kama lile la Umoja wa Ulaya na Marekani ya Kaskazini,,,KUWEPO KATIKA JUMIYA YA AFRIKA YA MASHARIKI KUSIWE KIGEZO CHA NCHI ZINGINE KULAZIMISHA NCHI WENZAO KUKUBALI MAAZIMIO AMBAYO MENGI YANAKUWA NA MASLAHI NA INCHI INAYOSHINIKIZA,,,

    HIVYO TANZANIA KAMA WANACHAMA WA EAC HARUWEZI KULAZIMISHA KIUNGIA MAAZIMIO YOOOTE HATA YALE TUNAYO JUA YATATUKOSESHA TIJA.

    HIVYO NDIVYO ILIVYO HATA KTK UMOJA WA ULAYA SIO KWAMBA KUWA MWANACHAMA NDIO KILA KITU UKUBALI KWA KUWA MAAMUZI YANATOLEWA NA WAU WOTE NA SIO WACHACHE KAMA KENYA NA RWANDA WANAVYOTAKA KILA KITU WANATAKA TUKUBALI,,,HIYO HAPANA HATA UMOJA WA ULAYA HAWAKUBALI KILA MAAZIMIO KTK UMOJA WAO.

    NDIO MAANA BAADHI YAMAMBO NCHI ZA ULAYA NCHI ZINGINE NCHI ZINGINE HAKUNA NA UMOJA UPO NA WANCHAMA WANAO.

    HIVYO HATA HII AFRIKA YA MASHARIKI PANA HITAJI RWANDA NA KENYA WAELEIMISHWE YA KUWA WACHUKUE MFANO UMOJA WA ULAYA SIO WATUSHINIKIZE KWA KILA KITU.

    HII NDIO TANZANIA BANA KILA MTU MJANJA HAPA BONGO RWANDA NA KENYA MSIFIKIRI MTANZANIA KUTOJUA KIINGEREZA VIZURI NDIO ATAKUWA HAELEWI MAMBO!!!

    ReplyDelete
  5. Habari ingenoga zaidi kama tungeambiwa ni flight za ndege gani zilitua katika viwanja vya Kilimanjaro na Julius Nyerere kutokana na moto uliofanya ndege hizo kutua Tanzania.

    Mara nyingi taarifa bila data huishia kudhaniwa ni propaganda wakati ni kweli.

    Hivyo wasemaji wa serikali yetu tukufu ya Tanzania wafuate mtindo wa 'John Pombe Magufuli'' kwa kutoa taarifa kwa umma zikiwa na data husika kutoka mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania kukidhi kiu ya wasomaji na kutengua majungu kama haya ya mtandao wa www.standardmedia.co.uk.

    Mdau
    Taarifa + Data

    ReplyDelete
  6. kumekucha, wameanza hao wasisahau kwamba walikuwa chimbuko la kuvunjika kwa afrika ya mashariki, wanatamani sana raslimali zetu, wametafuta kila njia ya kutaka kuchukua ardhi yetu kwa kisingizio cha ushirikiano wa afrika mashariki, watanzania tumekaza buti sasa wanatafuta kila sababu ya kutuchafua kwa visingizio kibao, watanzania tuwe macho na hila na jicho la husuda la majirani zetu wasiotutakia mema. ni wakati muafaka tushikamane bila ya kujali itikadi za kisiasa kuilinda na kuitetea nchi yetu. Mungu ibariki Tanzania na watu wake

    ReplyDelete
  7. wakenya wenyewe wabinafsi kama hizi rasilimali zingekuwa kwau tusingewajua kabisa wachoyo wana roho za kibinafsi

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...