220px-Coat of arms of Tanzania.svg f1f71


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefuatilia taarifa kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini, kuhusu kushiriki kwa Mheshimiwa Lu Younqing Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika huko Shinyanga, mwishoni mwa juma lililopita.
Taarifa hizo zimeambatana na picha zinazomuonyesha Mheshimiwa Lu akiwa amevaa kofia yenye nembo ya CCM. Habari zinaeleza kuwa Balozi alikwenda Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vita kuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani.

Wizara inatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Jamhuri ya watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vilevile inatambua kazi nzuri ambayo Balozi Lu Younqing amekuwa akifanya toka alipowasili nchini Tanzania. Kutokana na tukio hili, Wizara inapenda kuelekeza  kwamba kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa sio sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia.  Mkataba huo wa Vienna unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi. Aidha, Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986 ambayo ni zao la Mkataba wa Vienna pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi.

Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012 Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki.  Na kwa tukio hili pia Wizara  imechukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena.

IMETOLEWA NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
18 Septemba, 2013
Dar Es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Japokuwa hamjasema ni hatua gani stahiki mmechukua lakini kwa kauli hii tu ni kuonyesha ukomavu. Naomba na Nape na yeye aonyeshe ukomavu na ustaarabu kama huu.

    ReplyDelete
  2. Ama kweli ukubwa sio hoja, unaweza ukawa mkubwa halafu ukafanya mambo ya kitoto.

    Jamhuri ya China pia ina Vilaza?

    Hivi kama Mwana Diplomasia anaokea kwao akichaguliwa kwa kazi je, bado hajui Kanuni za kazi yeke aje afundishiwe Tanzania?

    ReplyDelete
  3. Je kwa nini Balozi wa China asiwajibishwe kutokea kwenye Serikali yao huko China?

    ReplyDelete
  4. Ahhhh,

    Mwacheni Balozi ni vile alinogewa na Sebene la ngoma ya Jadi ya Kisukuma akajikuta amevaa Kofia na labda zaidi ya kuvaa Kofia akajikuta amevaa na ''mawani'' yaani 'alikunywa kidogo' na akajisahau!

    Sherehe niliona zilikuwa na mapipa kadhaa ya Chimpumu Matingazzz ya Kisukuma.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...