Kwa sisi ambao tunafanya kazi na kutekeleza wajibu wetu wa kila siku pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam, kwenda Posta ni kati ya maswala magumu na mtu unafanya hivyo tu unapolazimika sana. Hivyo ni jambo la kawaida kabisa kwenda Posta na kukuta mabadiliko makubwa kama vile barabara au jengo jipya kwa sababu tu hujafika muda mrefu.
Leo nilikwenda Posta na baada ya kumaliza yaliyonipeleka Posta nilikua na safari ya kwenda kununua nyanya, vitunguu, dagaa, bamia na ngogwe sokoni Kariakoo. Hivyo nilitokea barabara ya Ohio na kuingia Bibi Titi Muhamed. Mahesabu yangu ilikua niingie Barabara ya Morogoro na kisha nielekee Kariakoo kwa kupitia pale Fire. Kwa kua hapakua na foleni, nilikuja kwa kasi ya kawaida na nikaonesha kiashiria cha kuingia Barabara ya Morogoro. Bila kujua kuwa hakuna tena uwezekano wa kutoka Barabara ya Bibi Titi na kuingia ya Morogoro, nilishangaa kuona wa nyuma yangu ananipigia honi kuwa napoteza muda. Nilipojaribu kukata kuingia Morogoro nikashtuka kuwa hakuna njia na nilipopita sio mahali halali pa kuingia. Wakati nashtuka na kurudi nyuma, ili ninyooke na Bibi Titi, ghafla nikaona askari wa usalama barabarani ananiita mbele yangu kua nisimame. Akaingia ndani ya gari na kunieleza makosa yangu. Kwa maelezo yake pale nilikua nimefanya makosa matatu kwa wakati mmoja: Kutumia barabara vibaya, kutokufuata sheria za barabarani, na kutaka kusababisha ajali kwa kupita kusikoruhusiwa. Nilitakiwa kulipa 90,000/= (30,000/= kwa kila kosa). Ilibidi nivute pumzi jinsi ya kujieleza hadi nikajikuta naanza kwa kujitambulisha jina, ninakotoka na ninapofanya kazi kama vile najitambulisha kwenye mkutano kabla ya kuanza kutoa mhadhara au kuchangia mada...usicheze na kulipa faini ambazo hujazitegemea.
Kusema ukweli nilichoka na kwa uungwana na ukweli wa moyo nilimweleza yule askari kuwa sikukusudia kuvunja sheria ila ukweli ni kuwa sikua na taarifa kuwa barabara zile kubwa mbili haziingiliani tena. Nilimwambia kuwa sijapita hiyo barabara muda mrefu kidogo na mara ya mwisho nilipopita ujenzi wa RBT ulikua unaendela na njia hizo zilikua zinaingiliana. Nilijaribu kumwambia kuwa, kwa mtu yeyote anayeijua DSM ni ngumu kuwaza kuwa kuna hayo mabadiliko katika eneo kama lile. Sikujua kuwa nilikua najielezea uzembe wangu wa kutokutazama vibao vipya...kumbe kuna vibao viwili pale vyenye alama ya kutokukunja kulia na kukuelekeza usonge mbele. Alinikatalia na kunipeleka kulipa faini.
Nilishangaa kujua kuwa lile lilikua eneo mkakati la askari kwani wamejenga hadi kibanda pembeni kwa lengo la kukamata watu pale na kulikua na askari kama watano hivi. Kwa kuwa ndani mwangu sikua kabisa na mpango wa kuvunja sheria wala makusudi yoyoye niliona halali kulipa ile pesa. Hivyo niliamua kuongea nao wote kwa muda kama dakika tano kwanza kueleza ugumu wa kuelewa yale mabadiliko na pili kuomba msamaha maana ningekosa pesa za kununua tena bamia iwapo ningelipa faini. Ninamshukuru Mungu na ninawashukuru wao kuwa nilipokubali kosa la kutokujua mabadiliko ya njia na kuomba msamaha; walinielewa na wakaniruhusu kuondoka bila kulipa...ingawa hawakauniacha bure kwani walisema kutokulipa faini kumetokana na “upare wangu”...tukacheka wote.
Nikiwa pale kwa zile dakika chache nilithibitisha kile nilichokua nawaeleza wale askari kuwa ni ngumu sana kwa mgeni wa mjini/njia ile kutokosea pale kwani ndani ya dakika kama tano nilishuhudia watu kadhaa wakikamatwa kwa kosa kama langu ambalo limetokana na yale mabadiliko kutokujulikana na ni ngumu sana kujua njia imefungwa kwani hata vibao vya alama za maelekezo ni vidogo.
Niwashauri wale wanaoendesha magari kuwa ukiwa unatokea Posta na barabara ya Bibi Titi hakuna ruhusa kuingia Barabara ya Morogoro. Kama una huo mpango, inakulazimu kunyooka hadi Mnazi Mmoja ndio utafute namna ya kugeuza urudi tena na Bibi Titi kuipata Morogoro au ukapitie barabara ya Lumumba kurudi Morogoro. Hakuna kuingia Morogoro kwa upande wa kuelekea Fire wala kuelekea Samora..Unapitiliza. Kwa maelezo ya wale watumishi wa umma (askari) niliowakuta pale walianiambia kuwa ile junction ni njia ya kupita mabasi ya RBT kwenda na kurudi katikati ya mji na sio kwa gari linguine lolote lile.
Pia nashauri badala ya kutumia hiyo nafasi kama mahali pa kuwatoza faini kubwa wakosaji wasio na hatia kama ambavyo ingekua kwangu, pawekwe vibao vikubwa zaidi na itafutwe namna nyingine ya kufanya yale mabadiliko ya njia zile kuu kujulikana na watu wengi zaidi.
Nimeona nikutaadharishe wewe usomaye ili usipate usumbufu na kulipa faini kubwa kwa kutokujua kama mimi ilivyonikubwa leo.
Mdau wa Bunju.
Mdau usifanye mambo kwa mazoea kuwa makini ukiwa barabarani kuangalia alama za vibao, alama za punda milia, matuta, spidi n.k
ReplyDeleteKukaa sana kwako DSM haina maana uendeshe chombo cha moto kwa mazoea kumbuka ajali husababisha kifo, majeraha na harasa kwako na Taifa.
Mdau
Mtoto wa Mjini
kwa kweli asante sana mdau wa Bunju kwa hayo maelekezo. Kiukweli hata mimi nisingejua maana nina karibu miezi 5 kama sio sita sijafika mjini, maana naishi Mbezi kazi nafanya ubungo, sokoni naenda mabibo kabla sijarudi home!
ReplyDeleteHuduma za benk zimejaa kibao pembezoni, tigo pesa, Mpesa na hata Beach zipo hukuhuku, mjini naenda kufanyaje tena? asante kwa moyo wako wa kizalendo!!!
ila Police wawaelekeze watu na si kusubiri wakosee ndipo wawatoze faini lol! wamepata pa kula pesa!!
Pole sana mdau na asante kwa kutoa habari hii kwenye blog kwani, wengi tufanyao kazi pembezoni ya jiji ha2fahamu kufungwa kwa njia hii. Na uongozi wa jiji letu kama kawaida hauoni sababu ya kutoa matangazo angalau kwenye vyombo vya habari licha ya kuhakikisha vibao ashiria vinawekwa kwa muonekanao na mahali pafaapo kabla mtumiaji wa barabara hajaathirika. Nami kabla ya kusoma hii habari hapa ningeingia kwenye mtego huo2. Pole sana. Mheshimiwa Slaa kazi kwako, 2nakutumainia ww ni jembe, fanyia kazi. Ili kamhogo kasiendelee kuchomwa hapo.
ReplyDeleteNdugu yangu una bahati!Mimi na wenzangu kama wanane hivi tulikamatwa hapohapo na baada ya maelezo nikaruhusiwa kumpeleka Mgonjwa wangu Regency Hospital kwa masharti ya kuwaachia Leseni yangu.Nilipotoka Hospital na kumuona Askari wa kike niliyemuachia Leseni alinielekeza kwa mtu aliyevaa kiraia na alikuwa mita chache tu kutoka kwenye Banda lao hilo ambaye niliambiwa nimpatie Pesa ili nichukue Leseni nami "NILITII BILA SHURUTI" ili kumuwahisha Mgonjwa wangu nyumbani kupumzika.
ReplyDeleteSasa Mdua ,Mabao makubwa yawekwe kuelekeza watu njia , wewe unao mshahara mzuri je wenzako wakale wapi?
ReplyDeleteAsante sana kaka kwa kutujuza. Hongera ujakutana na vijana wa yono nao ni noma now days. wanavizia kama wanataka kumnasa kobe.
ReplyDeleteMdau CM
We mdau sijui nikuweke katika kundi gani lakini inaonekana ulitoa rushwa! Hili nitatizo la serikali zetu! Kama umetenda kosa ungea'appeal' na ungelipa faini ya punguzo! Inaonekana na umesema kabisa ni uzembe wako kutosoma alama na maelekezo ya barabarani au pengine ulitumia ubabe wa kibongo!
ReplyDeleteTanzania na 'law enforcement' hatutafika! Yaani hakuna uzalendo wa Taifa
Hapa ndo wabongo fulani ndo wanaponichoshaga. Jamaa ameandika hii habari vizuri sana kama nilikua nasoma kitabu vile. Ametuelewesha yaliyomptata na kututahadharisha wengine tusiojua. Unafikiri kuna wangapi wameeingia kwenye mtego huo na hawakua na muda wa kutuelimisha hapa kwa Michu.
ReplyDeleteLakini lazma wabongo fulani wana akili ya kukosoa kila kitu na kujitia kutoa fundisho kwa mwandishi as if huyo mwandishi hayajui hayo.
Mtu anatoa maoni hapa kuwaelimisha watu, comments zenu zinatakiwa kua na nia ya kushukuru au kuwaelimisha watu zaidi ya mtoa maoni na sio ku critisize
Asante mdau mpare. Mie hapo nililipa shs 100,000/= ama nipelekwe polisi . na siku ile ilikuwa ijumaa jioni hivyo kutoka ingekuwa j3 kwa dhamana. Kwa kuwa nilikuwa nashughulikia harusi ilibidi nizite hizo baada ya kuniambia kuwa leo mzee si unajua ni ijumaa?
ReplyDelete