Dkt. Mugisha Clement Mazoko wa Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) (kushoto), Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Bw. Assaa Rashid (mwenye tai) na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Bw. James Mbatia (wa pili kulia) pamoja na ndugu na jamaa wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi wakiangalia wakati Mjumbe huyo akipandishwa ndani ya ndege kusafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Dkt. Mvungi alivamiwa na kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.
 Mke wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, …(kulia) pamoja na marafiki wakiomba dua leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere dakika chache kabla na Dkt. Mvungi hajasafishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia. Dkt. Mvungi alivamiwa na kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.
--------------------------------------------------------------------
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) amesafirishwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) saa 5:45 asubuhi kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Akiwa nchini Afrika Kusini, Dkt. Mvungi atapata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg.

Itakumbukwa kuwa Dkt. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013. Tukio hilo la uvamizi linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Tangu siku alipojeruhiwa, Dkt. Mvungi alikuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI). Hata hivyo, Madaktari waliokuwa wakimtibu MOI, walishauri afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi. 

Dkt. Mvungi ameondoka na ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink na ameambatana na Dkt. Mugisha Clement Mazoko kutoka MOI; Muuguzi Bi. Juliana Moshi; na mtoto wa kaka yake Bw. Deogratias Mwarabu. Serikali inagharamia gharama zote za matibabu ya Dkt. Mvungi.

Tume inawaomba wananchi wote waendelee kumuombea kwa Mungu Dkt. Mvungi ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida na hatimaye kuendelea majukumu yake.

Imetolewa na:
Ndg. Assaa A. Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam
Alhamisi, Novemba 7, 2013
0757 – 500800 /  0714 662482 / 0717 084 252 /

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa


  1. Poleni sana wanafamilia, ninajua mioyo yenu imejeruhiwa mnoo kwa tukio hili, Mungu wetu wa mbinguni awatie nguvu na amjalie afya njema mzee wetu.
    Hili pia ni changamoto kwa jeshi letu la polisi jinsi ya kurespond kwa haraka na kuwatia nguvuni wahalifu.
    Changamoto nyingne ni kwa serikali kuongeza vituo vya polisi na kuimarisha doria ktk maeneo ya pembezoni mwa dsm (mbezi, kimara,bunju, kibamba na kwingneko). Maboresho pia katika barabara za pembezoni maana Dsm inapanuka kwa kasi, hii itasaidia wananchi kufikiwa kwa urahisi wakati wa dharura.

    ReplyDelete
  2. Napenda kuwashauri watu wote Tanzania, Tanzania ya leo siyo ile ya wakati wa Nyerere, nawaomba kuweni na Bunduki ili mjitetee.

    ReplyDelete
  3. Poleni Ndugu na jamaa. Kuwa na bunduki si kuzuia maafa maana Dr alikuwa na Bastola na majambazi waliingia na mapanga na kuiba bastola yake pamoja na vingine.

    ReplyDelete
  4. Mimi swala la kumiliki silaha bado siliafiki,kama nchi kama marekani inaruhusu wananchi kuwa na silaha, na bado ina mauaji ya hali ya juu yanayo tokana na matumizi mabaya ya silaha, na tena ina ulinzi wa hali ya juu , je sisi Tanzania ambao ulinzi wetu ni legelege, watu wakiruhusiwa kumiliki silaha itakuwaje? matatizo si ndio yataongezeka badala ya kupungua?

    Mimi nashauri ufumbuzi mwingie, jeshi letu la polisi ndio lina hitaji mabadiliko ya hali ya juu, ili liweze kulinda wananchi.

    ReplyDelete
  5. Mungu ndie anajua ukweli wa tukio hili lakini binadamu tukumbuke kuwa kuna kiama na dhambi kama hizi zinawasubiri kwa hukumu.

    ReplyDelete
  6. ZANZIBAR HIYEEEE

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...