Na Mdau Ughaibuni
Tangu JPM aingie madarakani amekuwa akifanya maamuzi ya haraka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanyonge wa Tanzania. Naamini amekuwa akifanya hivyo ili kuwaonyesha  njia   viongozi wengine wa chini yake  ili nao  wawe wabunifu, wenye uthubutu,  na waweze kufanya maamuzi ya  haraka ili kuwapunguzia shida watanzania wanyonge.
Swali ninalojiuliza, Je viongozi wa chini yake wanaliona hilo na kufuata mfano wake. Tumewaona wachache wanaojitahidi lakini wengine  sina uhakika  kama watafikia matakwa ya Rais wetu mpendwa. Nachelea kusema haya kwani viongozi wasio wabunifu, wanaofanya kazi kwa mazoea na wasio na uthubutu wataendelea kumchosha Rais na Waziri mkuu wetu na kuchukua muda wake mwingi kufanya maamuzi ambayo yangefanywa nao katika ngazi zao. Ni vyema Rais na Waziri mkuu   waachwe  wafanye mambo makubwa zaidi  katika ngazi yao.
Je, Viongozi wa Wizara ya Afya walikuwa hawaoni kuwa wakina Mama wanalala chini mpaka Magufuli aje? Kama waliona walichukua hatua gani?  Ni jambo la wazi Kwamba hali ilivyo kuwa Muhimbili ni hivyo ilivyo katika   hospitali nyingine mikoani na wilayani na viongozi wapo. Unategemea Rais au Waziri mkuu  watembelea  hospitali za wilaya  zote ndio  mambo yabadilike.   Ni vyema viongozi wa ngazi hizo  waende na spidi ya JPM na kama hawawezi basi , ameshasema mwenyewe kwamba wampishe.
Muda wa kufanya kazi kwa mazoea umekwisha. Mfano mzuri  ni kuhusu  askari wa usalama barabarani, wanaona dhahiri  vijana  wa bodaboda wanavunja  sheria kwa kuvuka taa nyekundu, hawafuati  miongozo ya taa za barabarani  na mara nyingi wanasababisha ajali. Akari polisi wanasubiri mpaka ajali itokee na sio kuzuia ajali isitokee. Kuna siku moja niliwauliza askari wa usalama barani kwa nini hawawakamati waendesha bodaboda wanaovunja sheria kwa kuvuka kwenye taa nyekundu? Kwa mshangao askari huu alinijibu hawa hatuwawezi labda tuwapige risasi. Utaona kabisa  ubunifu katika utendaji kazi wake hakuna kabisa. Siku moja nilitembelea chuo kikuu kimoja jjini DSM katika idara inayoshughulikia maji na mazingira. Idara hii ndio unayofundisha wahandisi wa maji na mazingira, Lakini cha kushangaza  katika ofisi yao hakuna maji ya bomba wana weka maji kwenye ndoo kwa ajili ya  chai na kutumia maliwatoni. Kwa kweli kilinishangaza kidogo, hawa ndio wataalam wenyewe wanaofudisha taaluma  za maji  lakini wenyewe wanashindwa kujiwekea maji  ya bomba  yanayofanya kazi ndani za ofisi zao, sasa wanafundisha nini? Utaona hapa ni kufanya kazi kwa mazoea na kukosa ubunifu. Mifano ni mingi. Mheshimiwa JPM  una kazi kubwa sana ya kubadilisha  mfumo. Ikiwezekana baadhi ya wafanyakazi wa serikali wastaafishwe mapema ili uweke damu mpya  yenye ubunifu na uthubutu. Kuna watanzania wengi wako nje wameajiriwa na mashirika ya kimataifa wako tayari kuja kuijenga nchi chini ya uongozi wako imara. Ikiwezekana  nao warudishe nyumbani waje wachangie uchumi wa taifa. Naamini ukijenga mfumo wa uwajibikaji na ukaweka damu mpya katika ngazi zote ma DC, RC, Wakurugenxzi wa wilaya na idara za serikali utaivusha Tanzania   haraka kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Mungu ibariki Tanzania

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Maoni matamu kabisa yamejaa uzalendo.

    ReplyDelete
  2. Wahenga walisema "Mgeni njoo wenyeji wapone", hao waliozowea kufanya kazi kwa mazowea kubadilika kwa leo na kesho sidhani kama itakuwa rakhisi, maana siku zote mazowea yana tabu, mazowea hujenga tabia na tabia haina dawa. Lakini kwa juhudi, jitihada na kasi ya Mh. Rais wetu JPM aliyoanza nayo, itabidi tu wachaguwe moja, kusuka au kunyowa kwa manufaa ya watanzania na Taifa zima kwa jumla. Mungu ibariki Tanzania na watu wake, ibariki Afrika na dunia kwa jumla.

    ReplyDelete
  3. Hilo la bodaboda huwa linanishangaza sana. Wako juu ya sheria, yaani hili ni jipu lingine.
    Swala lingine ni uhalifu, nilishawahi kulisema huko nyuma wakati wa JK, likapita sikio moja likatokea upande wa pili. Kwa JPM naamini wataliona hili. Nilishauri hivi, mabalozi wa nyumba kumi warudishwe na wapewe posho. Wasiwe viongozi wa CCM kama zamani bali bali sehemu ya serikali ya mtaa. Kila mgeni anayekuja eneo lake kwa zaidi ya siku tatu lazima ajulishwe. Akiona watu wa ajabuajabu eneo lake atoe taarifa. Itasaidia sana kama ilivyokuwa enzi za Nyerere.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...